The House of Favourite Newspapers

Harmonize: Kajala Ana Damu Yangu Kwenye Moyo Wake

0

IJUMAA SHOWBIZ inatambua jinsi muziki wa Bongo Fleva unavyozidi kukua na kutanua mbawa kadiri siku zinavyokwenda.

 

Kuna wadau wengi wa kupongezwa kwa kufanikisha kukuza Bongo Fleva, lakini huu si mjadala kwa sasa. Tutazame kuibuka kwa Harmonize ambaye kwa sasa ni miongoni mwa wasanii wanaovuma zaidi Tanzania na Afrika Mashariki kwa sasa.

 

Taarifa ikufikie kwamba Harmonize aliibuka kwenye sanaa mwaka ule wa 2011, lakini hakupata mafanikio hadi mwaka 2015 pale kwenye Ukumbi wa Dar Live jijini Dar alipokutana na Diamond Platnumz kisha akaachia Ngoma ya Aiyola chini ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB).

Kwa mujibu wa WCB, Harmonize alikuwa msanii wa kwanza kusimamiwa na lebo hiyo kubwa ya muziki Tanzania na Afrika Mashariki. Baada ya kuachia Aiyola, Harmonize aliendelea kufanya vizuri ndani na nje ya Tanzania kwa ngoma kali kama Bado, Kwangwaru, Kainama na nyingine nyingi akiwa chini ya WCB.

 

Amepata kufanya kolabo na wasanii maarufu barani Afrika akiwemo Yemi Alade, Eddy Kenzo, Skales, Burna Boy na wengine.Akiwa chini ya WCB, Harmonize alianzisha lebo yake binafsi ya Konde Music Worldwide (Konde Gang) kwa lengo la kusimamia wasanii wengine. Muziki na jina lake vimeendelea kukua siku baada ya siku na kumfanya kutengeneza mashabiki wengi.

 

Harmonize au Konde Boy alishayakubali mafanikio yake chini ya WCB na akaona umuhimu wa kuongoza jahazi lingine la mafanikio ya muziki.Agosti 2019 ilikuwa mwaka wa mapinduzi kwa Harmonize baada ya kuamua kuikacha WCB na kuamua kuendeleza muziki wake binafsi.

 

Habari hii ilipokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa mashabiki, wengine waliona ni hatua mbaya huku wengine wakiiona ni hatua chanya kwa mustakabali wa kazi yake ya muziki.

 

Konde Boy ameshakua mkubwa na mwenye uwezo, mbinu na rasilimali za kuanzisha lebo yake na kuweza kusaidia vipaji vingine vilivyopo mtaani ili kuweza kusogeza muziki wa Tanzania mbali zaidi.

Harmonize ameshakua na kujipanga vya kutosha hadi kuanzisha lebo yake ya Konde Music Worldwide na zaidi ameshatengeneza mtandao wa kuweza kumuunga mkono tayari kujisimamia.

 

Hili limedhihirishwa na Harmonize mwenyewe kwani mara baada ua kujiengua WCB tena kwa amani bila mikwaruzo ameendelea kufanya vizuri kwa kutoa ngoma zilizobamba kama Uno, Bedroom, All Night, Wife na nyingine nyingi zinazofanya poa.

 

Zaidi, Harmonize ameachia albam yake ya Afro East; albam ambayo ilimtambulisha Harmonize mpya baada ya kung’atuka WCB. Sambamba na kujisimamia binafsi, tayari lebo ya muziki ya Konde Music Worldwide imewatambulisha wasanii kama Ibraah, Country Wizzy, Cheed, Killy, Angella na kumsimamia Skales wa Nigeria kwa upande wa Afrika Mashariki.

Sasa, wakati akifanya vizuri kwa kiwango hicho, mambo yamechanganyana. Wapo wanaosema sisimizi amebeba tembo. Ndivyo hivyo mambo yanakwenda kasi mno kwenye mitandao ya kijamii baada ya kapo mpya ya Harmonize na Kajala Masanja.Lakini mwenyewe Harmonize au Jeshi anasema kuwa, ameingia mzimamzima kwa Kajala ambaye ni staa wa Bongo Movies.Harmonize anamtahadharisha Kajala kwamba kama ataleta mambo yasiyoelewa kwenye mapenzi yao hayo, basi ajue anatembea na damu ya moyo wake hivyo kuendelea kuishi itakuwa ni ngumu. Katika mahojiano maalum (exclusive interview) na I

 

JUMAA SHOWBIZ, Harmonize au Tembo anafunguka mengi;

IJUMAA SHOWBIZ:Mambo vipi Jeshi, naona unapambana tu…

HARMONIZE: Mambo safi tu, kupambana ni muhimu, naona kwa sasa mambo ni mengi sana.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Hongera, naona video ya ngoma yako na Angella ya All Night imeingia kwenye trending namba moja…

HARMONIZE: Asante sana, kila kitu dua na kutengeneza kitu ambacho mashabiki wanakitaka, lakini yote kwa yote tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Zile shoo zako za mikoani mbona umezikatisha, kwa nini?

 

HARMONIZE: Nilikuwa na changamoto za kiafya hivyo nikashindwa kuendelea, lakini huko mbele kila kitu kitakaa sawa na ratiba zitakwenda kama kawaida.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Naona jina la Jeshi linazidi kushika kasi siku hadi siku, uliwaza nini hadi ukajipa jina hilo?

HARMONIZE:Lakini si ni kweli mimi ni jeshi la mtu mmoja? Niliamua tu mimi na uongozi wangu tukapenda jina hilo na kweli kama unavyoona ni jeshi hasa.

 

IJUMAA SHOWBIZ:Kule maeneo ya Coco-Beach jijini Dar wanapouza mihogo, wafanyabiashara wengi wamevaa vizibao vyeupe vilivyoandikwa Jeshi; hawa una uhusiano nao au ni watu wako umewaweka kukutangaza?

 

HARMONIZE: Hapana na hata siwajui kabisa. Ila juzi nilipita nikiwa na mamaaa kununua mihogo, nilishangazwa sana, sikujua nina watu wengi wenye mapenzi hivi na ndipo nilipogundua wamevaa Jeshi, nilifurahi sana na hata wao walifurahi sana. Mwisho wa siku ndivyo tunavyotakiwa tuishi hivyo.

 

IJUMAA SHOWBIZ:Umezungumza kuwa ulikuwa na mamaaa, je, ni Kajala au ni nani?

 

HARMONIZE: Ndiyo, sasa atakuwa nani tena kama siyo yeye?

 

IJUMAA SHOWBIZ: Kapo yenu imekuwa gumzo sana mitandaoni. Je, ni kweli mpo siriaz au ni mambo ya kiki tu?

 

HARMONIZE:Kwa nini kiki? Siwezi kufanya kiki ya mapenzi na tunawaombea wote wanaofurahia kapo yetu, maana hata sisi tunawapenda kila kukicha.

 

IJUMAA SHOWBIZ:Kuingia kwenye uhusiano na Kajala na kuweka wazi kwa upande wako haikuleta ukakasi au kuogopa?

 

HARMONIZE:Ningekuwa ninaiba ingekuwa shida, lakini ni wangu peke yangu, kwa nini nipate shida.

MAKALA: IMELDA MTEMA

Leave A Reply