The House of Favourite Newspapers

HATARI YA KUKOSEKANA KWA FURAHA KWENYE PENZI LAKO!

KARIBU kwenye ulimwengu wa elimu ya mapenzi na maisha. Tukubaliane kwamba wote tunazaliwa tukiwa safi ‘watakatifu’ kabla ya kukutana na mikikimikiki ya kimaisha inayotufanya tuwe tulivyo leo. Katika maisha, furaha ni nguzo muhimu mno. Usikubali mtu akuondolee furaha yako. Ni bora kuwa mwenyewe kuliko kuungana na mtu kisha ukawa unalia kila kukicha.

Wiki iliyopita nilieleza kiundani namna ambavyo ushauri mbovu unavyoweza kukutumbukiza shimoni na kukukosesha kabisa furaha. Kuwa makini! Katika ulimwengu huu, baadhi ya watu wanadhani mapenzi ni kuambatana wawili na kuwa mwili mmoja bila kujua ndani yake kuna shughuli pevu.

Fikiria wewe umezaliwa kwenye familia duni kijijini, unakula mlo mmoja kwa siku, tena kwa kubahatisha halafu unakutana na mwenzi ambaye amezaliwa ushuani kwenye mboga saba na milo mitatu kwa siku, achilia mbali ‘bites’ na matundamatunda. Kama hakutakuwa na mapenzi ya dhati yaliyowaunganisha bila kujali mmetokea familia gani, basi itakuwa ni migogoro kila kukicha.

Wengine wanadhani kuwa wawili ni mwanzo wa maisha mazuri na ya kifahari, yanapokosekana ndipo kunakuwa na mushkeli kwenye penzi lao. Kumbuka ninyi ni muunganiko wa watu wawili wenye hulka na tabia tofauti kutokana na malezi mmoja aliyopewa na wazazi wake. Mnajikuta mnatakiwa muungane kimwili, kiroho na kiakili.

Wengine hudhani kuwa na mwenza ni tendo la ndoa tu na hapa ndipo kwenye kiini cha ukosefu wa furaha kwenye maisha yako. Tendo la ndoa linapokosekana kutokana na sababu mbalimbali zinazofaa na zisizofaa, kunakuwa na tatizo kubwa ambalo ndilo huzaa usaliti, dharau, kejeli, matusi na mwisho wake ni kufarakana. Mnapaswa kuvumiliana.

Kuridhishana kimapenzi si jambo lelemama, ni ishu kubwa kati ya wenza hivyo kujikuta wakishindwa kujizuia na kutafuta kuridhika nje ya uhusiano wao. Je, mmoja anapogundua kwamba mwenzake anaridhishwa nje ya uhusiano kunaweza kuwa na furaha. Sahahu!

Majadiliano juu ya tendo la ndoa yanapaswa kufanyika mara kwa mara na wenza ili kila mmoja apate nafasi na uhuru wa kueleza hisia zake za namna anavyolichukulia penzi lake. Hapa suala la aibu hakuna na ni mwendo wa kufunguka tu.

Tafiti zinaonesha kuwa wengi hutoka nje ya uhusiano kama wenzi walio nao hawakuwa chaguo sahihi hivyo tunapaswa kujiridhisha na wapenzi wetu kabla ya kuingia kwenye uhusiano.Yapo mambo mengi yanayoweza kukufanya uwe na furaha daima kwenye penzi lako;

ZINGATIA MANENO AU LUGHA

Unapozungumza na mpenzi wako zingatia maneno au lugha unayotumia, toni ya sauti yako na mtazamo unaomuonesha. Hakikisha mambo haya hayamuondolei furaha na kumsababishia msongo.

ONESHA USHIRIKIANO

Jifunze kuwa sehemu ya furaha ya mpenzi wako kwa kuonesha ushirikiano katika mambo yanayomfurahisha. Usimkejeli wala kumpuuza anapokushirikisha kwenye furaha yake badala yake jaribu kuungana naye hata kama huna furaha kwa wakati husika.

MPE ZAWADI

Kama unajua kabisa kwamba mpenzi wako anapenda zawadi, basi uwe wa kwanza kumpa zawadi kabla yeye hajakupa. Na kama wewe umempa halafu yeye hajakupa, usiwe mwepesi kukasirika au kulalamika kuwa hakupi zawadi. Wewe endelea kumpa kwani kama kweli anakupenda, kuna siku atajitutumua na kukupa zawadi.

KIKOMO CHA KAZI

Lazima ujue kikomo cha mpenzi wako cha ufanyaji kazi. Hii itakusaidia kumfariji pale anapochoka na matokeo yake utafanikisha furaha yake.

Kwa hayo machache, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine motomoto. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwenye namba hapo juu. Pia usikose kutembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda kwenye Facebook.

Comments are closed.