Hatari ya maambukizi ya UTI kwa mjamzito

NJIA ya mkojo inajumuisha figo, mishipa ya figo, kibofu cha mkojo na urethra (mrija ambao hutoa mkojo nje ya mwili).  Zote zimeshikamana na hufanya kazi pamoja ili kuondoa uchafu kutoka kwenye damu. Kwanza figo husafisha damu na kugeuza uchafu kuwa mkojo. Halafu mkojo huteremka kwenye mishipa ya figo hadi kwenye kibofu cha mkojo ambapo hapo hutunzwa na baadaye kutolewa nje ya mwili kupitia mrija wa urethra. Maambukizi kwenye njia ya mkojo hutokea baada ya vimelea vyenye madhara (bakteria) kuingia katika urethra. Maambukizi yanaweza kuenea kwa urahisi kwenye kibofu cha mkojo au figo. Mama anaweza kupata maambukizi kwenye njia ya mkojo wakati wa ujauzito kuliko nyakati zingine zote.

Maambukizi kwenye njia ya mkojo hasa yanayofika kwenye figo, yanaweza kuwa hatari sana na pia kusababisha kuanza kwa leba mapema isipotibiwa mara moja. Ndio maana ni muhimu kuchunguza ishara za maambukizi katika kila ziara ya kliniki kwa mjamzito.

Ili kuzuia maambukizi kwenye njia ya mkojo, kinamama wakienda haja kubwa wajipanguze kutoka mbele kuelekea nyuma. Iwapo watajipanguza kutoka kwenye njia ya haja kubwa kuelekea njia ya mkojo, wanaweza kuweka vimelea katika sehemu za siri na vinaweza kuingia kwenye urethra.

Kina mama wanapaswa pia kukojoa mara tu baada ya kufanya tendo la ndoa. Kutumia kondomu pia husaidia kuzuia kuenea kwa maambukizi katika njia ya mkojo kutoka kwa mwanaume kwenda kwa mwanamke. Mama aliye na njia ya mkojo yenye afya si kawaida kuripoti maumivu, kuwashwa au uchungu wakati wa kukojoa. Hata hivyo, wakati mwingine mama anaweza kuwa na maambukizi kwenye njia ya mkojo lakini akakosa kuwa na dalili hizo.

Ni muhimu kutambua kuwa ikiwa maambukizi yamefikia kibofu cha mkojo au ikiwa yamekwenda zaidi katika njia ya mkojo na kufikia figo ni hatari kubwa kwa mama na mtoto ambaye hajazaliwa. Maambukizi kwenye njia ya mkojo yanaweza kutambuliwa kwa kuchunguza mkojo wa mama katika kituo cha afya. Uchunguzi unahitaji sampuli ya mkojo ‘wa katikati unapokojoa’. Wakati wa uchunguzi mwanamke achukue mkojo kwa chombo safi.

Kuwashwa au kuhisi uchungu unapokojoa inaweza pia kuwa ni ishara ya maambukizi ukeni au magonjwa ya zinaa. Dalili za maambukizi ya kibofu cha mkojo kwa mjamzito ni hizi zifuatazo: Kuhisi haja ya kukojoa, kukojoa kila mara, maumivu au uchungu unapokojoa au pindi tu baadaye maumivu katika fumbatio la chini, nyuma na mbele ya pelvisi.

DALILI ZA MAAMBUKIZI YA FIGO

Maumivu ya upande wa mgongo yanaweza kuwa ya kawaida katika ujauzito, au kuwa ishara ya maambukizi ya figo. Mkojo huwa na kama mawingu au damu na mjamzito kuhisi joto sana na kutokwa na jasho lingi.

Dalili nyingine ni mjamzito kuhisi mdhaifu, kuwa na maumivu ya upande wa mgongo (upande mmoja au pande zote mbili), kutapika mara kwa mara au kutetemeka sana. Dalili nyingine ni maumivu upande wa chini ya mgongo. Lakini kumbuka kwamba maumivu ya mgongo ni kawaida wakati wa ujauzito na huenda yasiwe ishara ya maambukizi ya figo hadi pale vipimo vitakapothibitisha.

TIBA NA USHAURI

Mjamzito anywe kikombe kimoja kikubwa cha kinywaji safi mara moja kila saa kabla hajalala. Vinywaji husaidia kuondoa maambukizi kutoka kwenye njia ya mkojo. Maji ya kawaida na yale ya matunda ni mazuri hasa kwa kunywa. Ale matunda ambayo yana vitamini C nyingi, kama vile machungwa, mapera, zeituni na maembe.

Maambukizi yasipopona haraka au mama akiwa na dalili yoyote ya maambukizi ya figo, aende kuonana na mtaalamu wa afya ili akachunguzwe na kuthibitisha maambukizi na kuanza matibabu yanayofaa ya antibiotiki (dawa za kuua bakteria) hasa Amoxicillin.

Mjamzito akiwa na maambukizi kwenye njia ya mkojo mara kwa mara, anaweza kupatiwa matibabu ya kinga pamoja na antibiotiki ili kuzuia maambukizi zaidi wakati wa ujauzito. Mjamzito usinywe dawa bila maelekezo ya mtaalamu wa afya.

Na Dk. Marise Richard


Loading...

Toa comment