The House of Favourite Newspapers

Hatari ya Simu za Mkononi Kimaisha

0

Simu ya mkononi ni kifaa kidogo chenye athari kubwa kwa maisha yetu lakini kwa wanaokitumia vizuri manufaa yake ni makubwa.

Ulimwengu wa teknolojia unamaanisha kwamba matumizi ya simu ya mkononi ni jambo la kawaida na kila mwaka mamilioni ya watu wanaingia katika kundi la wanaoanza kutumia simu za mkononi.

 

Hilo limerahisisha mawasiliano na huduma kote duniani .

Hata hivyo matumizi ya simu za mkononi yanakuja na madhara yake ambayo mwanzoni watu wengi hawakuwa wakijua yanaweza kuvuruga maisha yao sio tu kiafya bali pia kisaikolojia na hata kuhatarisha maisha yao .

 

Iwapo hukujua kwamba simu hiyo ya mkononi unayotumia kila siku inaweza kuyavuruga maisha yako -hizi hapa njia nne ambazo unaweza kujipata pabaya endapo hutakuwa muangalifu au makini kuhusu matumizi yako ya simu .

Kuna ushahidi wa wazi ambao wanasaikolojia wanasema matumizi ya simu yanaweza kuleta kwa tabia ya mtu hasa kijamii .

 

Sio jambo la ajabu kujua kwamba kwa sasa kuna watu hasa vijana ambao matumizi ya simu yameathiri sana uwezo wao hata kuweza kutangamana kwa njia ya kawaida.

 

Wamezoea kutumia simu na wakati wasipokuwa na simu zao mkononi maisha kwao yanakuwa sio ya kawaida na hata wanaweza kujihisi wagonjwa. Macho yake na umakini wake wote huelekezwa kwenye simu yake.

 

Basi kuna watu wasioweza kuendelea na shughuli zao kamwe bila kuwa na simu zao mikononi.

Visa pia ni vingi vya watoto majumbani kuachwa hoi wakati wazazi wanapojishughulisha na simu zao za mikononi na kukosa kuwapa hata muda wa kuwasikiza au kucheza nao.

 

Umewahi kusikia kuhusu ajali za barabarani zinazosababishwa na madereva ambao wanaendesha gari wakitumia simu za mkononi .Takwimu ni nyingi kuhusu idadi ya maafa yanayosababishwa na ajali kama hizo  zipo na watu wengine wamepoteza maisha kwa sababu ya simu wakati wa kiendesha gari au chombo cha moto kama pikipiki.

Kumekuwa na kampeni kote duniani na hasa kutoka kwa polisi kuhusu hatari ya kuendesha chombo cha moto huku ukitumia simu .

 

Visa pia vipo kuhusu watu ambao wanafanya kazi zinazoweza kutajwa kama ‘hatari’ ambao wanajitia hatarini hata zaidi kwa kutumia simu kama vile wanaoendesha mitambo ya moto .

 

Iwapo utajipata katika hali kama hizo,unashauriwa kuiweka kando simu yako mpaka ufike hatua unayoweza kuitumia.

Umewahi kusikia kuhusu watu kuzitumia simu vibaya kwa kutoa fedha wanazotumiwa kimakosa. Kwa muda mrefu watu wamekuwa wakitumia simu kama kinga ya kufanya maovu na uhalifu .

 

Sheria zinabadilika na kuboreshwa na usije ukadanganyika kwamba unaweza kutekeleza uhalifu kutumia simu yako ukifikiri uko salama.

Nchini Kenya kwa mfano mwanamke mmoja yupo mashakani kwani huenda akafungwa jela kwa kutoa shilingi 271,200 alizotumiwa kimakosa katika akaunti yake ya mpesa kupitia simu.

 

Elizabeth Karimi inaripotiwa na vyombo vya Habari nchini humo alitumiwa fedha hizo kwa bahati mbaya na mtu aliyekosea nambari ya akaunti . Wakati kampuni husika zilipojaribu kuzirejesha fedha hizo ,Bi.Kirimi alikuwa ameshazitoa fedha hizo kutoka kwa akaunti yake .Baadaye kesi hiyo ilifikishwa polisi na akasakwa ,kukamatwa na kufikishwa kortini.

Hilo linafaa kukupa mwamko kwamba usiwahi kutumia simu yako ya mkononi kutekeleza uhalifu ukifikiria kwamba mkono wa sheria hautokupata.

Iwapo ulifikiri unaweza kuinunua simu ya mkononi kwa yeyote kwa sababu umeipata kwa gharama ya chini ,basi itabidi uwaze tena suala hilo. Kuna hatari kubwa sana kununua simu kutoka kwa mtu yeyote kwa mifano wapo a watu waliofungwa jela kwa makosa makubwa hata ya mauaji kwa kuuziwa simu ambazo zilipatikana kupitia uhalifu.

Elvan Stambuli na BBC

Leave A Reply