Hatimaye Stamina Ataja Kilichovunja Ndoa Yake

STAA wa Bongo Fleva anayetikisa na ngoma yake ya Asiwaze, Bonaventure Kabogo ‘Stamina’ amefunguka sababu ya kuachia ngoma hiyo ambayo imeonekana kumponda aliyekuwa mke wake, Veronica Peter.

 

Baada ya ngoma hiyo inayotrendi kinoma, kumeibuka ishu kibao ikiwemo kusalitiwa na mkewe huyo ambaye ndoa yao ilifungwa Mwezi Mei, 2018 mjini Morogoro na kutawaliwa na shamrashamra kama zote.

 

Katika mahojiano maalum na Over Ze Weekend, Stamina au Shorwebwenzi anayeunda Kundi la Rostam akiwa na Ibrahim Mussa ‘Roma Mkatoliki’ amekiri muziki na simu kuwa chanzo kikubwa cha kuvunjika kwa ndoa yake kutokana na muda mwingi kuutumia studio.

 

“Muziki kwa kiasi kikubwa ni chanzo cha mtafaruku uliosababisha mimi na mke wangu tutengane kwa sababu kuna muda nakuwa studio mpaka saa 8:00 usiku, kiasi kwamba nasinzia, nikija kushtuka saa 12:00 alfajiri na nikiangalia simu nakuta missed calls zaidi ya kumi.

 

“Pia muda mwingine ninapokuwa kwenye shoo kawaida tu siwezi kupanda na simu stejini, lakini utakuta mke anakosa imani na mimi na ugomvi unaanzia hapo,” anafunguka Stamina.

Stamina amefunguka mengi, ungana naye hapa chini ujue kinagaubaga kuhusiana na muziki wake pamoja na ishu ya ndoa yake kuvunjika;

 

Over Ze Weekend: Umesema muziki ndiyo sababu kubwa ya ndoa yako kuvunjika, kivipi?

Stamina: Naweza kusema tu mwanamke niliyebahatika kumuoa hakuwa na ujuzi sana kwenye masuala ya muziki, ninamaanisha ishu nzima ya mzunguko wa kazi hii na mambo yote yanayohusiana na biashara ya muziki.

 

Pamoja na hilo pia tatizo lingine lilitokana na kufuatwafuatwa kwenye mitandao na muda mwingine meseji zinakuwa nyingi kutoka kwa watu tofautitofauti, jambo ambalo ni kawaida kwa watu maarufu, lakini kwa mwanamke niliyemuoa hakuwa akielewa kabisa juu ya hilo.

 

Over Ze Weekend: Unaona wanawake wanakosea wapi hasa?

Stamina: Wanakosea jambo moja tu, yaani wanataka kama mmeoana, basi mwanaume sitakiwi kuongea na mtu yeyote yule zaidi yake, jambo ambalo si zuri na halifai kwa kweli.

 

Over Ze Weekend: Wewe kama msanii unachukua hatua gani kuyakwepa hayo?

Stamina: Tasnia yetu ya muziki haitaki mambo ya kubanwabanwa hivyo kwa sababu naweza kujikuta nakosa kazi nyingi sana, kitu ambacho ninatambua na sitakiwi kukifanya ni kutokubali mtu ambaye ananitaka kimapenzi tu, lakini siyo kutokuongea naye.

 

Over Ze Weekend: Sababu gani nyingine hasa iliyosababisha ndoa yenu kuvunjika?

Stamina: Kikubwa kingine ni simu, unajua simu ni siri ya mmiliki na ndiyo maana hata Fid Q aliimba ule mstari uliosema; ‘ni ruhusa kushikana ila siyo kushikiana simu’ sasa mwenzangu alikuwa hataki kulikubali hili na ndiyo sababu mtafaruku ukawa mkubwa.

 

Over Ze Weekend: Nini ushauri wako kwa vijana ambao bado hawajaingia kwenye ndoa?

Stamina: Vijana waingie tu kwenye ndoa ila wajue kabisa kuwa ndoa siyo kama kwenda kununua jeans Kariakoo, ni maisha ambayo hakuna anayeyajua kama siyo mhusika mwenyewe.

 

Mbali na maelezo ya Stamina, Over Ze Weekend ilizungumza na mwanamuziki mwenzake ambaye ndiye msimamizi wa ndoa yao, Roma Mkatoliki ambaye alifungukia ndoa ya jamaa yake huyo kuvunjika.

“Aaah kwa muda mrefu sasa mke wa Stamina hayupo nyumbani, yaani kuanzia Machi, mwaka jana na tulishajaribu kuwasuluhisha na mambo bado hayajawa sawa.

 

“Nadhani majibu hasa anayo mwenyewe Stamina kuhusiana na nini hasa kilichomsibu, naomba niishie hapo,” alimaliza Roma.

Mei, 2018 Stamina alifunga ndoa na mkewe, Veronica katika Kanisa Katoliki mjini Morogoro na hawakujaliwa kupata mtoto hadi wanatengana.

AMMAR MASIMBA


Loading...

Toa comment