The House of Favourite Newspapers

Hatua za Kuanza Kujitegemea na Kuachana na maisha ya kula kulala bure

0

UCHUNGUZI unaonesha kuwa kila mtu anapenda kujitegemea, lakini wengi wanashindwa kufanya hivyo kwa sababu ya kukosa kitu wanachokiamini, nacho ni kutokuwa na uwezo wa kufanya hivyo!
“Napenda sana kujitegemea lakini sina uwezo,” wengi hutamka hivyo unapowauliza kwa nini wanazeekea kwenye maisha ya utegemezi. Sababu ya kukosa uwezo imewafanya baadhi ya watu kuwa tayari kupokea kila aina ya manyanyaso na mwisho wa yote wanajipoza kwa kulia.
Swali la kujiuliza: Ni nani aliyezaliwa anajitegemea? Jibu ni hakuna, hapa ndipo penye msingi wa mada hii ambayo naamini kupitia vipengele vifuatavyo msomaji wangu utajifunza jinsi ya kuanza maisha ya kujitegemea.

MTAZAMO
Kikwazo cha kwanza kinachowafanya watu waishi maisha ya utegemezi ni mtazamo. Wengi wanaamini wana haki ya kulelewa na wazazi/ndugu, lakini wanashindwa kujiuliza wataishi katika utegemezi mpaka lini na wanaowategemea wakifariki dunia wataishije?
Kazi ya kwanza katika kuyaelekea maisha ya kujitegemea ni kubadili mtazamo wa maisha tegemezi na kuona umuhimu wa kujitegemea. Maana yangu hapa ni kuyachukia maisha ya kumtegemea mtu na kutamani maisha ya kujitegemea ambayo ni huru na yenye raha.

KUJITEGEMEA NDANI YA UTEGEMEZI
Baada ya kubadilisha mtazamo, mhusika ni lazima aanze maisha ya kujitegemea ndani ya utegemezi. Msingi wa kipengele hiki ni huu; kuna baadhi ya watu wanabweteka mno na kutaka wafanyiwe kila kitu na walezi wao ambapo hata andazi la shilingi 300 wanataka wanunuliwe! Kisingizio ni kilekile, kwamba hawana uwezo ingawa fedha kama shilingi mia tano wanazipata.
Kujifunza kujitegemea lazima kuanzie ndani ya maisha ya kujitegemea. Mfano kama jukumu la baba ni kununua mboga na wewe umebahatika kupata kiasi cha fedha kwa njia yoyote hata ya kupewa, usizifiche, badala yake lichukue jukumu la baba na kulifanya wewe. Tabia hii inajenga msingi wa uwajibikaji ambao ndiyo nguzo ya maisha ya kujitegemea.
Chukia maisha ya kufanyiwa kila kitu, jihangaishe kwa kazi ya aina yoyote, jiwekee utaratibu wa kuhudumia familia yenu, weka msingi wa kuheshimu fedha, usiendekeze tabia ya kupata fedha na kuacha kufanya jambo la maana nyumbani kisa unamtegemea baba au mama atakununulia hiki na kile na kuzifanya fedha zako ziwe za kutapanya ovyo. Ukijizoeza hivyo hutaweza kujitegemea.
Kabla ya kuingia kipengele kingine hebu nikuulize msomaji wangu ni mara ngapi umekuwa ukimsaidia mlezi wako kukabiliana na changamoto za kuendesha maisha kwa kipato kidogo unachopata katika kazi zako ndogondogo?
Kama unafanya hivyo tambua umeanza mazoezi ya kujitegemea, endelea kufanya hivyo lakini kama umebweteka tu nyumbani unakula na kulala bure; tambua uzee utakukuta ukiwa ‘mtumwa’ wa wazazi au walezi wako na hutakuwa na mafanikio yako hadi unaingia kaburini.

KUJIAMINI
Vikwazo au shaka juu ya kuweza kumudu maisha ya kujitegemea vimewafanya wengi wasijiamini. “Kwa kipato hiki nitaweza kweli kuendesha maisha yangu, nilipe kodi ya nyumba, chakula, mavazi na mahitaji mengine?” Maswali ya aina hii mara nyingi yamekuwa na majibu ya HAITAWEZEKANA!

Itaendelea wiki ijayo!

Leave A Reply