The House of Favourite Newspapers

Haya Ndiyo Niliyoyaona Baharini-6

0

ILIPOISHIA KWENYE GAZETI LA AMANI, JANA:
Nahodha alivaa nguo zake, akamshukuru Mungu kisha akatangaza kuanza safari. Safari hii tulitakiwa kwenda kisiwa kinaitwa Papua New Guinea, lakini safari yenyewe sasa, ndani ya dakika arobaini na tano tu baada ya kutoka bandarini, jambo kubwa sana likatutokea.
SASA ENDELEA MWENYEWE…

Ghafla meli ilisimima. Ikaanza kuzunguka kama vile pangaboi linavyozunguka ila yenyewe ikawa inazunguka polepole.
“Ni nini Nurdin. mbona kama tunasukwasukwa na bahari kuchafuka? Mimi nahisi tunapinduka Nurdin?” nilisema katika hali ambayo sikujua nini kinaendelea.
“Hapo ni lango jingine la kuzimu Tolu, nahodha amejisahau. Au hayupo kwenye mashine yake nini? Maana anapajua palivyo…bwana Tolu shikilia mahali lolote linaweza kutokea,” Nurdin aliniambia na kuniongezea wasiwasi zaidi, afadhali asingesema, angenipa matumaini tu.
Nilishika bomba la juu yangu ambalo tunatumia kutundika nguo kama maovalori au makoti ya kazi.

Ghafla meli ikawa kama inapaa, ikaenda kutua mbele na safari ikaendelea. Nurdin alichomoka tulipokaa akaenda kumchungulia nahodha. Aliporudi alisema:
“Nahodha yupo, alikuwa akipambana sana. Inabidi kumshukuru Mungu. Nahodha amenionesha dole gumba kwamba mambo yote yako sawa lakini tulikuwa kwenye hatari.”
Nilijishika kifuani upande wenye moyo. Ulikuwa ukidunda sana. Bado nilikuwa na neno lile la Nurdin kwamba lolote linaweza kutokea. Hapo sasa tunaelekea Papua New Guinea.
Hii ni nchi tofauti kabisa na ile Guinea ya Afrika. Hii ipo Asia. Kwa hiyo kuna Guinea kama tatu hivi. Kuna Guinea yenye mji wake mkuu Conakry kuna Guinea Bissau ambayo mji wake mkuu ni Bissau. Hizi zote zipo Afrika. Halafu kuna hii ya Papua ambayo mji wake mkuu ni  Port Moresby.
Nurdin muda mwingi alikuwa yuko na mimi kwa maana ya ukaribu. Alionesha kwamba, alikuwa akitilia shaka kujiamini kwangu katika hali ile.

Kama nilivyosema awali, meli ile ilikuwa ina wafanyakazi wengi, kwa hiyo misukosuko yote hiyo ilikuwa inatupata tukiwa wote ila mimi na Nurdin tuliondokea kuwa marafiki wakubwa katika meli hiyo.
Tulitembea umbali mrefu kidogo, tukaanza kushika mwelekeo kama tunakwenda Kisiwa cha Timor ya Mashariki (East Timor) na kuipita kwa kusini. Nurdin alishangaa, akamfuata nahodha akidai huo si mwelekeo wa Papua New Guenea.
Aliporudi alisema kuwa, nahodha alipokea simu ya upepo ikimtaka aende kwenye kisiwa kimoja kinaitwa Tasmania, kipo Australia Bara la Australia.

Hapo sasa ni siku ya pili na jua lilikuwa limetoka. Nurdin akaniambia kuwa, hapo tunapokwenda kuna maajabu nitayaona lakini hayatokani na majini bali kazi ya Mungu. Aliniambia huku akicheka. Nilimuuliza ni maajabu gani hayo, akasema hataniambia mpaka nione mwenyewe.
Basi, nilikuwa naangalia kila kitu katika uhalisia wake ili niweze kuona hayo maajabu ya Mungu.
“Nimeshaona,” nilimwambia Nurdin.
“Umeona nini?” aliniuliza.

“Nimeona mpaka sasa meli imekuwa nzito kutembea maana muda mrefu tangu nimeliona jua likitoka naliona kama linatembea kwenda kulia kwetu na halipandi juu kuja utosini.
Nurdin alicheka sana, akasema hayo ndiyo maajabu ya Mungu. Nilibaini kuwa, jua kule linapita kama ule mshale wa mvua (rain bow). Kwa hiyo jua nililiona likitoka kushoto kwangu na kwenda kuzama kulia kwangu bila kupita utosini kama nyumbani Tanzania. Nilishangaa sana.

“Nchi zote za kusini kama vile Austarlia, New Zealand, Visiwa vya Falkland na zile zilizopo kaskazini kama vile Sweden, Denmark, Visiwa vya Barafu (Ice Land) na nyinginezo, hawalioni jua kama Afrika Mashariki. Wao huliona jua kwa saa nne au mpaka nane tu kisha linazama. Afrika Mashariki mnaliona jua kwa saa kumi na mbili.

“Mfano tunakokwenda kuna wakati jua halionekani hata kwa siku tatu. Lakini ndani ya siku tatu kuna usiku na mchana kwa mujibu wa saa. Pale dunia inakuwa imehama katika kusimama kwake, hivyo jua linaonekama sana kaskazini ambapo wao sasa wanaweza kuliona jua hata siku mbili bila usiku. Wanalala kwa kutumia saa tu kwamba muda huo ni wa kulala haijalishi jua linawaka,” aliniambia Nurdin.
Basi, kwa sababu jua lilikuwa likichukua muda mfupi sana kuchomoza na kutua, hata kabla hatujafika kwenye bandari ya Tasmania, likawa limezama.

Pale Tasmania tulipakia mzigo mwingine wa kwenda Papua lakini kwa akili zangu za harakaharaka mzigo ule ulikuwa si halali na ilitakiwa iwe usiku na kuondoka usiku.

Usiku huo ulikuwa mrefu sana kwani mpaka tunaondoka bandarini, ilitakiwa iwe saa nne asubuhi ya jua kuwaka lakini bado giza lilitanda angani. Ina maana ilikuwa wakati wa usiku kuwa mrefu.
Tuliondoka na giza bado kuelekea Papua. Meli ilikuwa ikikata maji huku ikionekana kuwa nzito sana kiasi kwamba nilijaribu kumuuliza Nurdin kama hali ile ilitokana na mzigo mkubwa au nini, akasema si mzigo.
Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply