The House of Favourite Newspapers

Mafanikio ni kwa kila mtu, kwa nini umri uwe kikwazo kwako?

0

Ni wiki nyingine tena tunakutana kupitia safu hii nikiamini kwamba umzima na unaendelea vyema na mishemishe za kimaisha. Kwa wale Wakristo najua wako kwenye shamrashamra za Sikukuu ya Pasaka, niwatakie sikukuu njema!
Mpenzi msomaji wangu, katika maisha ya sasa, kila mtu anatamani kuwa na mafanikio makubwa. Kila mtu anatamani kuwa tajiri. Hata kama siyo utajiri mkubwa kama walivyo wale mabilionea wanaotikisa duniani lakini angalau mtu awe na pesa za kutosha benki huku akiwa na miradi yake inayomuingizia kipato kila siku.

Hiyo ndiyo ndoto waliyonayo wengi ndiyo maana unashuhudia baadhi ya watu wakiwa hawalali, wanafanya kazi usiku na mchana kusaka pesa kwa njia halali wakiamini ndizo zitakazowafanya waishi maisha mazuri.
Cha kushangaza sasa, wapo watu wenye dhana potofu juu ya utafutaji wa mafanikio. Kuna vijana huko mtaani ambao wana nguvu za kutosha huku wakiwa wamejaaliwa maarifa lakini eti wamekata tamaa na maisha wakihisi hata wafanyeje hawawezi kufanikiwa.

Hivi nani kasema mafanikio ni kwa ajili ya watu f’lani tu? Mafanikio ni kwa kila mmoja wetu bila kujali jinsia yake, umri wake, kabila lake wala anapoishi.
Ndiyo maana kuna watu wako vijijini lakini wana mafanikio makubwa. Wapo watu walikulia kwenye familia maskini lakini leo hii wanaogelea kwenye utajiri.
Hiyo inadhihirisha kuwa, mafanikio yanapatikana popote, kwa mtu yeyote, mwenye umri wowote aliyedhamiria kuyapata. Kikubwa ni kujua kanuni za kufuata kwenye kuelekea mafanikio.
Lakini sasa, katika makala haya naomba niweke kitu kimoja wazi kwamba, usije ukakata tamaa ya kutafuta mafanikio kwa kikwazo cha umri wako.

Hili lipo kwa baadhi ya watu. Unakuta mtu alianza kupambana kusaka mafanikio akiwa na umri wa miaka 20, anafikisha miaka 40 akiwa bado hajafanikiwa kivile, anakata tamaa.
Hebu msikie huyu kijana ambaye anaonesha wazi ameyapa kisogo mafanikio kwa sababu tu anaamini kwa umri alionao, hata afanyeje hawezi kufanikiwa tena.
“Mimi nilianza kutafuta pesa baada ya kumaliza darasa la saba, nilikuwa nafanya biashara ya kuuza mitumba. Niliifanya biashara hiyo kwa muda mrefu kabla ya kufungua duka langu Kariakoo. Kusema ukweli ni muda mrefu nimeifanya biashara hiyo lakini mpaka leo hii siyaoni mafanikio niliyoyatamani
“Ni kama nacheza ngoma ya Kimasai kwani nikienda mbele kidogo, narudi nyuma. Inafika wakati nakata tamaa, sasa naelekea miaka 45. Hebu fikiria tangu nina miaka 19, mpaka leo sina mafanikio ya kueleweka, navunjika moyo kwa kweli,” anaeleza Juma Shabani wa Buguruni jijini Dar.

Kuna kitu cha kujifunza kutoka kwa mfanyabiashara huyu. Kwamba unaweza kuwa umepambana kwa muda mrefu katika kusaka mafanikio lakini mpaka leo hujafika unapopataka. Usife moyo, endelea kupambana.
Huenda pia ulizembea huko nyuma, ukawa umebweteka ila ukaja kujishtukia wakati umri umekwenda, kumbuka mafanikio hayaangalii umri. Hata mzee anaweza kupata mafanikio kama kweli amedhamiria.

Leave A Reply