The House of Favourite Newspapers

Heche Ahoji Mkataba wa Madini Kati ya Tanzania na Barrick – Video

0

 

WAZIRI Kivuli wa Madini nchini Tanzania, John Heche amehoji mambo manne kuhusu mikataba tisa ambayo Serikali ya Tanzania imesaini na kampuni ya Barrick Gold Ijumaa ya Januari 24, 2020.

 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Januari 29, 2020 mjini Dodoma, Heche ambaye ni mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), amesema katika makubaliano hayo mambo mengi yamefichwa.

 

Makubaliano kati ya Serikali na Barrick yaliyoshuhudiwa na Rais John Magufuli ni matunda ya mazungumzo kati ya Serikali na kampuni hiyo tangu mwaka 2017 yaliyozaa kampuni ya Twiga itakayosimamia migodi mitatu iliyokuwa chini ya kampuni ya Acacia.

 

Mgogoro kati ya Serikali na kampuni ya Acacia iliyokuwa inasimamia migodi ya Buzwagi, North Mara na Bulyanhulu ulianza mwaka 2017 na Magufuli akaunda tume kuchunguza mwenendo wa biashara ya madini.

 

Tume hiyo ilibaini ukiukwaji wa sheria, utaratibu na kanuni zilizopo hivyo kuikosesha Serikali mapato inayostahili. Kutokana na hilo, Serikali iliipiga faini ya Dola 190 bilioni jambo lililosababisha kuanza kwa mazungumzo baina ya pande hizo mbili.

 

Kwenye mazungumzo hayo, Acacia ambayo ni kampuni tanzu ya Barrick iliwekwa pembeni na majadiliano yakafanywa na Barrick, mwisho wa siku, Acacia imefutwa sokoni na badala yake, Twiga ikachukua nafasi yake.

 

Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari, Heche amesema Chadema watailazimisha Serikali kupeleka mikataba yote tisa ili ukweli ujulikane.

 

“Faida za kiuchumi katika mkataba huu ni zipi na kwa nini haziwekwi wazi. Uwazi kuhusu asilimia 16 za hisa za Tanzania ni upi. Ziko wapi Sh426 trilioni walizokuwa wanadaiwa hao Barrick na kwa nini wameruhusu Serikali kushtakiwa nje wakati walishakataa,” amesema Heche.

 

Leave A Reply