The House of Favourite Newspapers

Heri Niwe Peke Yangu – 01

0

ABIGAL ni mwanamke mrembo aliyehitimu masomo yake ya uhasibu katika Chuo Kikuu cha SAUT kilichoko jijini Mwanza. Akiwa masomoni alibahatika kupata mtoto ambaye baba yake alijulikana kwa jina la Jonathan. Wawili hawa haikuwachukua muda mrefu katika mahusiano yao kwani baada ya Abigail kujifungua mtoto, Jonathan alianza kuonyesha utofauti ambao ulipelekea malumbano yasiyokoma kati yao. Kila kukicha, kwao ilikuwa ni siku mbaya hatimaye waliachana. Kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwa Abigail kwani alimpenda sana mwenza wake huyo.

 

Baada ya Abigail kuhitimu masomo yake, alibahatika kupata kazi kitengo cha uhasibu katika benki ya CRDB iliyopo jijini Mwanza. Siku moja akiwa kazini, alipokea ujumbe mfupi kwenye simu yake uliomshitua kidogo. “Itabidi umwambie ukweli kuwa mimi ndiyo mkeo kwa sababu nimechoshwa na ahadi zako zisizotimia.”

 

Ujumbe huu ulimpa maswali mengi yaliyokosa majibu kwa sababu alishindwa kuelewa ulikuwa una maana gani na aliyeutuma ni nani. Alichukua maamuzi ya kuipiga namba ile. “Hey sikia nikwambie nimechoshwa na maneno yako ya ulaghai ni bora uwe mkweli kuliko kunichosha na hayo maneno yako,” ilisikika sauti ya mdada akiongea kwa ukali na kwa kulalamika kisha aliikata simu bila hata ya kumpa nafasi Abigail kusema neno lolote. “Hivi huyu dada ana akili kweli? Au kavurugwa! Nadhani atakuwa amekosea namba,” Abigail alijiongelesha kisha aliiweka simu yake pembeni na kuendelea na kazi.

 

Baada ya dakika tano alipokea ujumbe mwingine kutoka kwa namba ileile. “Huwezi kunipotezea muda wangu ni zaidi ya miaka miwili sasa unaniambia hadithi ileile. Sasa leo utakapokuwa unarudi nyumbani naomba uje na jibu linaloeleweka,” huu ujumbe ulimfanya Abigail aache shughuli zake na kuanza kutafakari. Kadri alivyoendelea kujiuliza ndivyo alivyozidi kukosa majibu.

 

Aliamua kutoka ofisini kwake na kuelekea ofisini kwa rafiki yake aliyeitwa Mary ambaye alikuwa kitengo cha afisa wa benki. “Vipi Abigail mbona unaonekana kutokuwa sawa?” Aliuliza Mary. “Hebu tazama huu ujumbe kisha uniambie umeelewa nini,” Abigail alimpa Mary simu yake ili asome ule ujumbe uliotoka kwa mdada asiyejulikana. Kwa mshangao Mary aliuliza “Mbona sielewi! Kwani huyu aliyekutumia ujumbe huu unamfahamu?” “Hapana mimi simfahamu na hata nilipojaribu kumpigia hakunipa nafasi ya kuzungumza neno lolote labda ningemuuliza yeye ni nani,” alijibu Abigail. “Shoga yangu siku hizi matapeli wana njia nyingi za wizi achana nae endelea na kazi zako mdogo wangu,” aliongea Mary.

 

Abigail alirudi ofisini kwake akiwa na maswali mengi kichwani. Baadae aliona anapoteza muda kwa kitu asichokijua aliamua kuendelea na kazi zake. Siku hiyo haikuwa nzuri kabisa kwa Abigail, ilipofika saa nane mchana alipokea simu kutoka shuleni alipokuwa anasomea mwanae akihitajika kufanya haraka na kuelekea hospitali ya rufaa ya Bugando iliyoko jijini Mwanza kwani mtoto wake alipelekwa hapo baada ya kupata ajali ya gari. Gari aina ya Prado lilikosea njia na kuligonga gari la shule. Abigail alitoka ofisini akiwa amechanganyikiwa kabisa huku machozi yakimlenga lenga machoni pake.

 

Aliwasha gari yake aina ya Rav 4 na kuliendesha kwa kasi kuelekea Bugando. Alipofika wodini alipigwa na butwaa baada ya kumuona mpenzi wake wa zamani ‘Jonathan’ akiwa amesimama pembeni ya binti yake ambaye alikuwa amelazwa kitandani huku amefungwa bandeji kichwani na mikononi. Jasho lilikuwa linamtiririka Jonathan kwa hofu. “Na wewe umefata nini hapa,” Abigail alimuuliza Jonathan. “Abigail is it you? (Abigail ni wewe?) Aliuliza Jonathan kwa mshangao.

 

Daktari aliyekuwa zamu siku hiyo, alishangazwa na mazungumzo yao na kugundua kuwa huenda wawili hawa wanafahamiana. “Samahani kijana nakuomba ofisini mara moja muache dada amuone mwanae na istoshe mgonjwa anahitaji utulivu na hapo mnampigia kelele,” daktari alimtaka Jonathan amfuate ofisini kwake.

 

Wakiwa ofisini, daktari alimtaka Jonathan afunguke na kumueleza ukweli. Jonathan hakusita alimueleza daktari mkasa mzima uliomuhusu yeye na Abigail jambo lililomfanya daktari kumshauri aondoke haraka iwezekanavyo bila kumpa taarifa yoyote Abigail kwani laiti angemruhusu Abigail kujua kuwa yeye ndiye chanzo cha ajali ile, basi lazima angemrudisha kituo cha polisi pasipo huruma yoyote.Jonathan ndiye mwenye ile Prado iliyosababisha ajali. Aliusikiliza ushauri wa daktari na kuondoka haraka mahali pale kisha aliendelea kutoa huduma zote za matibabu kama alivyoahidi katika kituo cha polisi mara baada ya kukamatwa.

 

 

Baada ya siku tatu mtoto aliruhusiwa japo hali yake haikuwa nzuri sana na alihitajika kuhudhuria mazoezi pale hospitalini ndani ya siku saba.Maswali yalizidi kuongezeka kichwani mwa Abigail kwani tangu siku ile aonane na Jonathan pale hospitalini hakuwahi kumuona tena na alipomuuliza daktari kuhusu yeye, daktari alimueleza uongo kuwa; Jonathan alikuwa ni moja ya watu waliozoea kutembelea wagonjwa hospitalini pale na kutoa misaada kwa hiyo siku hiyo alikuja kuwasalimu wagonjwa tu na kisha aliondoka.

 

Jibu hilo halikumridhisha Abigail kwa hiyo aliamua kumtafuta mwalimu ambaye alimpa taarifa ya ajali siku ile, ampeleke katika kituo cha polisi ambapo walichukulia ‘PF3’ kabla ya kwenda hospitalini. Mwalimu hakusita alimpeleka Abigail katika kituo hicho cha polisi. Baada ya Abigail kufanya upelelezi aligundua kuwa kesi ilifunguliwa na kisha kufutwa baada ya mtuhumiwa kukiri kosa na kutoa faini na kisha kuahidi kutoa huduma zote za matibabu mpaka mtoto atakapo kuwa amepona.

 

“Mama jukumu hilo lipo mikononi mwetu na ndo maana toka siku ile mtoto wako anapata huduma nzuri bila wewe kutoa gharama yoyote,” afisa polisi alitoa maelezo kwa Abigail. “Sawa afisa lakini nahitaji kumjua aliyesababisha ajali hiyo,” Alijibu Abigail. “Itakusaidia nini ukimjua mamaa? Wewe mshukuru Mungu mwanao anaendelea vizuri,” askari aliongea kwa ukali. Abigail aliamua kuondoka kwa hasira huku akijisemea kwa sauti ya chini, “Hapa kuna jambo wanajaribu kunificha ila nitaujua ukweli.”

 

Ilikuwa imebaki miezi miwili tu ili Abigail afunge ndoa kwa kijana aliyejulikana kwa jina la Felix. Kijana ambaye alitokea kumpenda sana mda mfupi tu baada ya yeye kuachana na Jonathan. Mahusiano ya Abigail na Felix yalianza kama mzaha huku Felix akionyesha kumpenda zaidi Abigail wakati huo Abigail akionyesha kumpenda mwenzake kawaida tu.

 

Dosari iliingia pale Abigail alipotamani muda wa maandalizi ya ndoa yao usogezwe mbele pasipo kutoa sababu yoyote. Ilikuwa ni jioni moja Abigail na Felix wakiwa wametulia nyumbani kwa mrembo huyo wakijadiliana kuhusu maandalizi ya ndoa yao. Abigail alionyesha kutokuwa na furaha kabisa huku akimshawishi Felix wasogeze mbele tarehe ya siku ya ndoa yao. “Abigail mpenzi mambo mazuri hayacheleweshwi, hutakiwa kufanyika kwa haraka na siyo kurudishwa nyuma. Sitakubali hilo lifanyike kama hutanipa sababu za msingi,” aliongea Felix.

 

“Naomba unielewe mpenzi sipo tayari kwa sasa kwani akili yangu haipo sawa na sihitaji kuingia kwenye ndoa nikiwa sina raha,” alijibu Abigail. “Basi nishirikishe hicho kinachokusumbua eeh? Mimi ni mume wako mtarajiwa kama utaanza kunificha hisia zako mapema hivi si itakuwa shida huko kwenye ndoa sasa?” Aliendelea kuzungumza Felix kwa hasira. “Nahitaji kujua baba wa mwanangu alipo kisha tutafunga ndoa na istoshe nilimpenda sana Jonathan,” alijibu Abigail. “Whaaat! (Niniii!) hivi umejisikia ulivyozungumza kweli? Are you out of your mind?” (Umechanganikiwa?) Alihoji Felix kwa jazba.

 

Abigail aliondoka kwa hasira na kuelekea chumbani huku akilia kwa kigugumizi kutokana na hasira iliyokuwa imejaa kifuani mwake. Felix alimfata na kuanza kumbembeleza. “Nyamaza mke wangu, najua ulimpenda sana Jonathan na pia tukio la ajali bado linakuvuruga akili lakini leo nataka nikwambie ukweli uliojificha kwa zaidi ya miaka mitano, kwa hiyo nyamaza na unisikilize vizuri.”

 

******************IITAENDELEA*********************

Jalia Yusuph
Simu: 0622 216 238
@kalamu_na_karatasi

Leave A Reply