The House of Favourite Newspapers

Heri Niwe Peke Yangu – 02

0

“Sitaki kusikia chochote kwani nimeshadanganywa vingi sitaki naomba uniache,” alijibu Abigail. “Sasa nisikilize vizuri, mimi ndiye baba mzazi wa huyu unayemuita mwanao,” Felix alizungumza kwa msisitizo.

 

Abigail aliacha kulia na kunyanyua kichwa kisha alimwangalia Felix usoni kwa kustaabu. “Umesemaje wewe? Naomba usinivuruge kabisa. Umenijua mimi nikiwa tayari nina huyu mtoto kwa hiyo inakuwaje unasema huyu mtoto ni wako? Naomba tuheshimiane Felix,” alijibu Abigail kwa jazba. Felix alikaa kimya kwa dakika nzima bila kujibu neno lolote kisha alitoka nje na kuwasha gari lake na kuondoka kuelekea nyumbani kwake na kumuacha Abigail chumbani akiwa na mwanae kitandani.

 

“Mungu wangu ni nini hiki mbona sielewi? Maisha yangu yamekuwa ni kitendawili kisichoteguka, naomba unisaidie Mungu wangu nisaidieee,” aliongea Abigail huku akilia kwa sauti ya juu. Alitoka chumbani na kwenda sebuleni kumwangalia Felix, hakumkuta na alipotoka nje hakuliona gari lake.

 

“Honey! umekwenda wapi?” Abigail alimpigia simu Felix. “Sipo sawa pia, nimeamua kuondoka nikifika nyumbani nitakujulisha,” Felix alijibu na kisha alikata simu. Abigail alizidi kupata maumivu kifuani mwake kwa msongo wa mawazo uliozidi kumuumiza kichwa.

 

Ilikuwa ni siku ya nne toka mwanae Abigail aliyejulikana kwa jina la Elizabeth aanze kuhudhuria hospitalini kwa ajili ya mazoezi. Siku hiyo Abigail akiwa amezama katika dimbwi la mawazo, alipata wazo la kumfata yule daktari aliyewahudumia siku ya kwanza baada ya ajali kutokea.

 

“Tafadhali daktari naomba unieleze ukweli. Usiponijibu leo, mimi najiua kwani ninayachukia maisha yangu sasa. Kila siku zinavyozidi kwenda nazidi kuvurugika likiisha hili leo, kesho linakuja jingine. Naomba uniambie yule mwanaume uliyemuita ofisini kwako siku ile alienda wapi?

 

Ni baba wa mwanangu naomba unisaidie kwani nilimpenda sana na kabla sijafunga ndoa hivi karibuni nahitaji nimuone nimpe ujumbe wake kisha nifunge ndoa kwa amani,” Abigail aliongea huku akibubujikwa machozi. Daktari alimuonea huruma na kuamua kumueleza ukweli. “Binti yangu, huyo mwanaume ndiye chanzo cha ajali iliyopelekea mtoto wako kuwa hapa leo.”

 

Daktari aliendelea kumuelezea kila kitu hadi mahali alipoishi yaani mtaa na namba ya nyumba aliyoishi Jonathan kisha alimpatia namba ya simu ya Jonathan. “Nashukuru sana daktari Mungu akubariki,” Abigail alishukuru.

 

Baada ya mtoto kupatiwa huduma, Abigail hakutaka kupoteza muda, aliwasha gari na kuelekea moja kwa moja nyumbani kwa Jonathan. Aliifuata kwa makini sana ramani aliyocholewa na daktari na hatimaye alifanikisha kufika nyumbani kwa Jonathan. Kabla hajabisha hodi simu yake iliita na alipoitoa kuitazama, alishangazwa sana kuona ni namba ya Jonathan ndiyo inaita. Macho yalimtoka asiamini kile anachokiona. “Mmmh! amejuaje kama nipo hapa? Au hapa nje kuna kamera?”

 

Kumbe bado ana namba yangu ya simu!” Abigail alijiuliza huku macho yake yakiangaza huku na kule akichunguza kama mahali pale palikuwa na kamera. Simu iliita mpaka ikakata.

 

Baada ya sekunde chache, Abigail aliona geti la nyumba hiyo likifunguliwa na gari aina ya Prado lilitoka nje kuelekea mahali alipokuwa amesimama. “Huyu siyo Jonathan kweli na hilo siyo gari lake alilonieleza daktari kuwa ndiyo lilisababisha ajali?” Abigail aliwaza. “Ni macho yangu au naona vibaya? Huyu siyo Abigail kweli? Hata Jonathan ndani ya gari alishangazwa kumuona Abigail.

 

Alitoa gari mpaka nje kisha aliliegesha pembeni na kushuka. “Mama Elizabeth, mbona upo hapa?” Katika hali ya kushangaza mtoto Elizabeth alimkimbilia Jonathan na kumkumbatia.

 

“Babaa…babaa…tumekuja kukutembelea unakwenda wapi?” Aliongea mtoto. “Eliza, nani amekwambia huyu ni baba yako?” Abigail aliuliza kwa mshangao kwani toka yeye na Jonathan waachane na kumuacha Elizabeth akiwa mdogo sana, hakuwahi kumwambia ukweli kuhusu baba yake mzazi na kila alipouliza kuhusu baba yake, yeye alimwambia kuwa hayupo alisafiri ila ipo siku atarudi.

 

“Kipindi nimelazwa hospitalini, alikuwa anakuja kunisalimia wakati wewe haupo na kuniambia kuwa yeye ndiye baba yangu pia alinionyesha picha akiwa amenibeba kipindi niko mdogo sana,” alijibu Elizabeth.

 

Jibu hilo halikumshangaza sana Abigail kwa sababu alikwisha ambiwa kila kitu na daktari japo Jonathan alishituka kidogo akihofia huenda Abigail angetahamaki. “Basi karibuni ndani jamani…. eeh! Mlinzi ingiza hilo gari ndani.” Jonathan aliongea huku akiwaongoza Elizabeth na mama yake ndani.

 

Wakiwa wameketi sebuleni, Abigail alizungusha macho yake huku na kule akitazama samani za kifahari zilizoipamba sebule ile. “Mama Elizabeth karibu na pia hujanijibu mbona upo hapa?”

 

Aliuliza Jonathan huku akiwa ametawaliwa na hofu. “Asante baba Elizabeth, nipo hapa kwa ajili yako kuna jambo nimekuja kukueleza na ile siku niliyokuona pale hospitalini nilifurahi sana kwani toka tuonane ni muda mrefu sana na isitoshe hukuwa unapatikana kwa namba yako ya mwanzo,” alijibu Abigail.

 

“Kabla hujanieleza hilo jambo lililokuleta naomba nikwambie kuwa huyu mtoto, siyo mtoto wangu. Najua nitakuwa nimekupa maswali mengi sana lakini naomba hilo ulijue kwanza pia umenikuta natoa gari nje, hiyo safari ilikuwa ni yako. Nilikupigia simu hukupokea nilitaka unielekeze unapoishi kwani nakumbuka kipindi tunaachana ulikuwa unaishi na wazazi wako,” aliongea Jonathan kwa kujiamini.

 

“Hahahahaa…. usinichekeshe mimi, eti huyu mtoto siyo wako, hivi ulichokizungumza umekielewa kweli? Au unadhani sijui kama wewe ndo chanzo cha ile ajali? Kwa hiyo unatafuta njia ya kujilinda nisilijue hilo?” Alijibu Abigail huku akicheka kwa dharau.

 

Wakiendelea na mazungumzo, ghafla moja ya milango ya pale sebuleni ulifunguliwa na binti mrembo mwenye umbo namba nane aliyejulikana kwa jina la Magreth akiwa amevalia khanga moja alitokea.

 

“Ooh! Hubby mbona hukuniambia kama umerudi? Tena umerudi na mgeni? Karib….” aliongea dada huyo na kabla hajamaliza, Jonathan alidakia.

 

“Aaammh! imekuwa ghafla tu kwani mgeni mwenyewe kanifanyia sapraizi na istoshe…” kabla hajamaliza kuongea, simu yake iliita. “Halo, tajiri samahani nimetumia namba ngeni, mimi ni yule Mac mfanya biashara mwenzako. Naomba ufanye haraka uwezavyo tukutane maeneo ya Usagara najua ni mbali lakini jitahidi kwani nimeua ndege wawili kwa jiwe moja.”

Ilisikika sauti ya mfanya biashara mwenzake aliyemfahamu vizuri. “Sawa tajiri nakuja sasa hivi,” alijibu Jonathan.

 

Jonathan alimuomba Abigail asiondoke na alimhakikishia kuwa angewahi kurudi. “Samahani mama Eliza natoka kidogo imekuwa ni dharura lakini naomba usiondoke narudi muda si mrefu. Tafadhari Magreth naomba uwahudumie wageni narudi sasa hivi,” Jonathan aliondoka na kuwaacha Abigail na mwanae pamoja na Magreth wakiwa wameketi palepale sebuleni. Magreth alimuagiza dada wa kazi awaletee juisi wageni.

 

Wakiendelea kumgoja Jonathan, Abigail alionekana kukosa raha kabisa na kuonekana kuwa mwenye mawazo mengi sana. “Mami karibu juisi mbona unaonekana mwenye mawazo sana?”

 

Magreth alimuuliza Abigail. “Kwani wewe ni nani hapa,” Abigail aliuliza. “Mimi ni mwenza wake Jonathan na mahusiano yetu yana muda mrefu sasa zaidi ya mwaka mmoja kwani wewe ni nani kwake?”

 

Magreth alijibu kisha alimuuliza Abigail. Swali hilo lilimfanya Abigail aanze kutoa machozi mfululizo. “Mbona unalia? Swali langu limekukwaza,” alihoji Magreth. “Hapana hujanikwaza naomba unielezee kwanza wewe ni nani kisha nitakueleza kuhusu mimi,” alijibu Abigail.

 

Heri Niwe Peke Yangu – 01

 

******************IITAENDELEA*********************

Jalia Yusuph
Simu: 0622 216 238
@kalamu_na_karatasi

Leave A Reply