The House of Favourite Newspapers

Hivi utaishi maisha ya kuungaunga hadi lini?

0

young-couple-arguing-on-a-sofa-136381366849303901-130702114836Wiki hii msomaji wangu nataka kuzungumzia tabia ya wale ambao wapowapo tu, hawafanyi chochote kuyaboresha maisha yao badala yake wamekuwa ni watu wa kuishi kwa kuungaunga.

Kama utakumbuka katika moja ya makala zangu niliwahi kueleza madhara ya kuishi kwa kumtegemea mtu mwingine nikitolea mfano ule usemi wa Kiswahili usemao; ‘Mtegemea cha ndugu hufa maskini.’

Usemi huu una maana kubwa sana hasa ukiangalia jinsi baadhi ya watu huko mtaani ambao wamekosa muelekeo wa maisha kutokana na ukweli kwamba kipindi cha nyuma walikuwa wakitegemea watu f’lani wawasaidie lakini watu hao walipoondoka maisha yao yakabaki yananing’inia.

Kwa mfano, wapo vijana ambao sasa hivi wamekuwa watumiaji wa madawa ya kulevya, wamegeuka watu wa kupiga mizinga lakini ukifuatilia utaambiwa walikuwa wakiwategemea wazazi wao waliokuwa na uwezo na sasa hawapo.

Vijana hao walikuwa na nafasi nzuri za kusoma lakini wakagoma kwenda shule na hatimaye kukosa kazi za msingi za kufanya licha ya kwamba wazazi wao walikuwa na ndoto za kuwaandalia maisha mazuri.

Matokeo yake sasa wamekuwa ni tegemezi kwenye jamii halafu walalamishi sana pale ambapo wataomba msaada halafu wasipewe.

Ndiyo manaa leo nikaona nilizungumzie hili la kwamba, kabla ya kufikiria nani wa kukusaidia, unatakiwa kujiuliza wewe kwa akili, maarifa na nguvu alizokujaalia Mungu unafanyaje ili usiishi kimagumashi?

Je, ni kweli huwezi kufanya lolote la kuyaboresha maisha yako na badala yake unategemea ndugu zako au marafiki wakupe sapoti?

Ukijaribu kufuatilia maandiko matakatifu utaona yanaeleza kwamba, miongoni mwa yale yanayomchukiza Mungu ni pamoja na kitendo cha mtu ambaye ana uwezo wa kutafuta na akapata kwa kufanya kazi lakini akabweteka na kutegemea msaada.

Wewe msomaji ni shahidi kwamba huko mtaani wapo watu ambao eti kwa sababu mmoja kati ya ndugu zao ana uwezo kifedha basi hawataki kabisa kujishughulisha huku wakiweka akilini kwamba; ‘f’lani atanisaidia’.

Ni sawa huyo f’lani kama anao uwezo ana haki ya kusaidia ndugu zake pale inapobidi lakini si vibaya kwanza wewe ukajiuliza, umejisaidiaje kwa nguvu na akili ulizopewa na Mungu na ukashindwa wapi?

Usikae tu ukabweteka na kutegemea huyo f’lani atakusadia. Fahamu naye ana majukumu yake. Si kwamba kwa sababu ana uwezo basi kila siku atakuwa akiangalia nani ana tatizo amsaidie, kuna kipindi atakuwa hana uwezo wa kukusaidia, je utaishije?

Waliobahatika kuwa katika nafasi nzuri kimaisha ni mashahidi wa usumbufu wanaoupata kutoka kwa watu wa karibu yao ambao hawataki kujituma kufanya chochote katika maisha yao.

Wao wanategemea tu kusaidiwa licha ya kwamba wakiamua kujituma kwa bidii wanaweza kuondokana na hali duni waliyo nayo.

Utawasikia wakisema; ‘Ooh! Maisha ni magumu sana’. Hivi nani kasema maisha ni magumu? Ugumu wa maisha tunautengeneza sisi wenyewe na kama tukitaka maisha yawe rahisi inawezekana kabisa.

Kwani hao ambao maisha yao yamejawa na mafanikio wana akili ya aina gani kukushinda wewe ambaye kutwa kushinda ukiombaomba kana kwamba ni mlemavu? Je, hao unaowaona wanajiweza kimaisha wana tofauti kubwa na wewe?

Hapana! Naamini waliofanikiwa katika maisha ni watu wa kawaida tu kama mimi na wewe. Kikubwa ambacho kilichowafikisha hapo walipo ni kuuchukia utegemezi na kutotaka maisha ya kuungaunga.

Leave A Reply