The House of Favourite Newspapers

Kushindwa Kupata Mimba (Infetility)

0

pregnant_2176694b.jpgMoja ya matatizo yaliyoko katika jamii zetu na yamesababisha wanandoa wengi au wanawake wengi kukosa furaha ni baada ya mama kushindwa kupata ujauzito kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja ndani ya ndoa licha ya kuingiliana, hili huitwa Primary Infertility.

Hata hivyo, suala la mwanamke kupata ujauzito linahusisha pande zote mbili, yaani upande wa mwanamke na mwanaume, wote wawili wanapokuwa katika afya nzuri ndipo ujauzito unaweza kupatikana kwa mwanamke.

Tatizo hili limegawanyika sehemu mbili, moja ni la wale ambao hawajawahi kupata mimba kabisa katika maisha yao licha ya kufikia umri na pili ni wale ambao wamewahi kupata mimba au kuzaa, lakini ikapita miaka kadhaa bila kupata ujauzito tena, kundi hili huitwa Secondary Infelitity.

Kuna wengine huweza kupata mimba baada ya mzunguko mmoja wa hedhi. Utafiti unabainisha kuwa asilimia 80 ya wanandoa huwa wanapata mimba wakati wowote wakitaka kupata ndani ya mwaka mmoja na asilimia 10 hushindwa kupata ujauzito kwa sababu mbalimbali.

Asilimia 10 nyingine hushindwa kupata mimba bila sababu yoyote ya msingi. Vitu muhimu vinavyochangia akina mama kupata ujauzito ni kuwa na afya njema kwa mbegu za wanaume ambazo huweza kusafirishwa kwa kasi sana kwenda kwenye vifuko vya mayai kupitia ukeni huku zikiwa zimebadilika umbo na kuwa lijulikanalo kama Capacitation Acrosome Reaction.

Mbegu za kiume hutakiwa kuwa na uwezo wa kuogelea na kuingia kupitia mlango wa kuzuizi Cervix kwenda kwenye mji wa uzazi yaani uterine Cavity na hatimaye kufika kwenye mirija ya uzazi kitaalam huitwa Fallopian Tubes.

Miongoni mwa sababu zinazoweza kumfanya mwanamke ashindwe kupata ujauzito ni kama zifuatazo:

Matatizo katika homoni, hii ni kutokana na kwamba, mzunguko Menstrual cycle katika mwili wa mwanamke hutawaliwa na hizi kemikali asilia ndani ya mwili ambapo mabadiliko madogo yakitokea katika uzalishaji wa hizi homoni au homoni kuzalishwa katika wakati ambao siyo muafaka huweza kusababisha mwanamke akashindwa kupata ujauzito, pia tatizo la kuwa na uzito wa mwili mdogo sana au mkubwa sana pia huathiri hali nzima ya homoni na kusababisha kushindwa kupata ujauzito.

Umri, kwa wanawake uwezo wa kupata ujauzito unapungua kwa kadiri umri unavyoongezeka, hii inatokana na kupungua kwa uzalishaji wa homoni husika wakati umri unavyoongezeka. Kuanzia miaka 35 na kuendelea huwa kunakuwa na tatizo la kushindwa kupata ujauzito kwa wanawake wengi.

Kuziba kwa mirija Fallopian Tubes, hii husababisha mbegu za kiume Sperms zishindwe kulifikia yai na kulirutubisha ili ujauzito utokee. Kuziba kwa mirija huweza kusababishwa na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana, matatizo katika kizazi au upasuaji. Mara nyingi wanawake ambao mirija yao ya uzazi imeziba, hawahisi dalili zozote.

Ute ute katika kizazi Mucus Problems, ute unaopatikana katika kizazi cha mwanamke huwa na sifa ya kuruhusu mbegu za kiume ziweze kusafiri kwa urahisi na kulifikia yai ili kulirutubisha.

Kwa baadhi ya wanawake ute huu unakuwa na uzito na kemikali ambazo ni vigumu kwa mbegu za kiume kuweza kupita na wakati mwingine mwili wa mwanamke huzalisha sumu ambazo huziua mbegu za kiume, haya yote husababisha kukutana kwa yai na mbegu za kiume kusitokee na hivyo ujauzito kutopatikana.

Uvimbe katika kizazi Fibroids, hii huchangia asilimia tatu katika mwanamke kutopata ujauzito. Uvimbe huu ambao hutokea katika kuta za mji wa mimba, kwa namna moja au nyingine huweza kuzuia yai lililorutubishwa lisikae sehemu yake na hivyo kuathiri kizazi.

Matibabu ya kansa, kwa kutegemeana na aina ya matibabu, aina ya dawa au njia ya mionzi, hizi huweza kumuathiri mwanamke na kumsababishia kushindwa kupata ujauzito.

Ukomavu katika kizazi, kwa baadhi ya wanawake wanayo matatizo ambayo kizazi chao huwa hakijakomaa vizuri au katika kuzaliwa kwao walizaliwa na tatizo hili ambalo, kizazi hakiko sawa Abnormally Developed uterus.

Asilimia kubwa ya matatizo ya mwanamke kushindwa kupata ujauzito yanayo tiba, kama unalo tatizo katika kupata ujauzito usikate tamaa, onana na wataalam wa afya ili uweze kujua chanzo cha tatizo lako na kupatiwa msaada unaostahili.

Dk. Marise anapatikana Marise Dispensary, njia panda ya Mabibo mkabala na kituo cha mafuta.

Leave A Reply