The House of Favourite Newspapers

Hofu Yatanda Hali ya Trump!

0

RAIS wa Marekani, Donald Trump, anaendelea kupewa uangalizi wa karibu akiwa hospitali ambako anapokea matibabu ya Covid-19. Kuna tashwishi kuhusu uwezekano wa Trump kutolewa hospitali – kama walivyokuwa wamesema madaktari wake kwamba huenda akatoka Jumatatu huku maswali yakiibuliwa kuhusu hali yake.

 

Kiwango cha oksijeni yake kilishuka mara mbili na pia anafanyiwa tiba ya steroid. Siku ya Jumapili, aliushangaza umma alipoonekana hadharani akiendeshwa kwenye gari kuwasalimu wafuasi wake, hatua ambayo ilikosolewa vikali.

 

“Zaidi ya Wamarekani 205,000 wamefariki. Tunataka uongozi. Siyo picha na video,” aliandika kwenye Twitter yake, Hakeem Jeffries, mwenyekiti wa Democrats katika Bunge la Wawakilishi.

 

Akiwa amevalia barakoa, rais alipunga mkono kutoka ndani ya gari muda mfupi baada ya kuandika ujumbe kwenye mtandao wake wa Twitter akisema kwamba atafanya “ziara ya kushtukiza”. Trump, ambaye amekosolewa kwa jinsi alivyoshughulikia janga la corona, pia alisema amejifunza mengi kuhusu virusi hivyo.

 

Rais aliongezewa oksijeni ya ziada mara moja baada kuthibitishwa kuwa na virusi, alisema Dk Conley, ambaye pia alifafanua mkanganyiko uliosababishwa na taarifa tofauti kuhusu hali ya Trump.

 

Katika ujumbe wa Twitter, rais – aliyekuwa amevalia suti, koti na shati bila kufunga tai – alisema: “Nimejifunza mengi kuhusiana na Covid.  Nimejifunza kwa kwenda shule hasa. Hii ni shule halisi. Hii siyo shule ya njoo tusome vitabu. Sasa naona na nimeelewa. Ni jambo la kuvutia sana, hivi karibuni nitawafahamisha.”

Kuugua kwa rais, kulikotangazwa hadharani na yeye mwenywe kwenye mtandao wa Twitter mapema Ijumaa, kumevuruga ratiba yake ya kampeni. Trump atakabiliana na mpinzani wake wa chama cha Democratic, Joe Biden, katika uchaguzi wa urais wa Novemba tatu.

 

Madaktari wake walisema nini?

Akizungumza na wanahabari katika kituo cha kitaifa cha matibabu karibu na Washington DC, Dk Conley alisema kiwango cha hewa ya oksijeni ya Trump kilishuka kwa mara ya kwanza akiwa Ikulu ya White House. Rais alikuwa na homa kali, alisema, na kuongeza kuwa kiwango cha oksijeni cha mtu mzima kinatakiwa kuwa asilimia 95 au zaidi na chake kilikuwa asilimia 94%.

 

Tukio la pili lilifanyika siku ya Jumamosi, wakati kiwango chake cha oksijeni kilishuka chini ya asilimia 93. Alipoulizwa kuhusu hilo, Dkt. Conley hakusema ikiwa rais aliongezewa hewa ya oksijeni lakini akaongeza, ikiwa hilo, lilifanyika, “ilikuwa kwa kiwango kidogo sana”.

 

Rais mwenye umri wa miaka 74,  anaorodheshwa miongoni mwa watu waliyo na uzani mkubwa kuliko kiasi, yuko kwenye kundi la watu walio kwenye hatari zaidi kuugua maradhi ya Covid-19.

 

Siku ya Ijumaa alipewa dawa ambayo inafanyiwa majaribio ambayo inajumuisha mchanganyiko wa dawa inayopatiwa mgonjwa kwa njia ya sindano na pia ameanza kutumia dawa ya remdesivir kwa siku tano.

 

Madaktari wamesema rais hajapatikana na homa tangu siku ya Ijumaa na ini na figo zake zinafanya kazi kama kawaida.

 

Hali ya kisiasa iko vipi?

Timu ya kampeni ya rais siku ya Jumamosi ilisema kuwa itaendelea mbele “kwa kasi” na kampeni hadi Bw. Trump atakapojiunga nayo tena.

Inatoa wito kwa ”washirika wakuu” miongoni mwao wana wa kiume wa Trump, Donald Jr na Eric, na makamu wa rais Mike Pence “kuendelea mbele na kampeni” kwa sasa.

Hakuna shughuli yoyote iliyopangwa kufanyika katika Ikulu ya White House Jumatatu ya leo.

 

Joe Biden, ambaye ameendelea na kampeni yake, anatarajiwa kuzuru Miami, Florida siku ya Jumatatu – licha ya kutumia jukwaa moja na Bw. Trump Jumanne iliyopita wakati ambapo huenda tayari alikuwa ameambukizwa virusi. Kampeni ya Bw. Biden siku ya Jumapili ilisema kuwa vipimo vimeonesha kuwa hana virusi hivyo.

 

Katika mahojiano na kituo cha CBS kipindi cha Face the Nation, Spika wa Bunge Nancy Pelosi, ambaye pia ni mwanachama wa Democratic, alisema wabunge wa Republican na rais “kwa muda mrefu …wamepinga sayansi” na kuongeza kuwa anatumai kupatikana kwa Bw. Trump na virusi vya corona kutabadilisha mtazamo wake kuhusu virusi hivyo.

 

Leave A Reply