The House of Favourite Newspapers

Huyu Ndiye Mwanamke Anayemnyima Idris Usingizi

0

NI mshindi wa Big Brother Africa mwaka 2014. Ni mchekeshaji. Ni mtangazaji. Ni mshereheshaji (MC).

Huyu si mwingine ni Idriss Sultan. Mwamba ameendelea kujipatia umaarufu tangu alipoibuka kidedea kwenye shindano hilo lililofanyika nchini Afrika Kusini na kuondoka na kitita cha shilingi milioni 500 za Kitanzania.

Idris amewahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Tanzania Sweetheart, Wema Isaac Sepetu na kuamua kuishi pamoja kama mtu na mpenzi wake.

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limefanya mahojiano maalum (exclusive interview) na Idris kuhusu maisha yake na kazi zake ambazo zinadaiwa kumuingizia mkwanja mrefu licha ya kwamba watu wanadai hapendi kujionesha;

IJUMAA WIKIENDA: Kwa kuwa wengi wanakufahamu kama mchekeshaji, unawezaje kuigiza filamu zenye maudhui ya ‘siriazi’?

IDRIS: Ni kipaji tu nilichonacho pamoja na kufanya mazoezi mara kwa mara. Nina uwezo wa kufanya filamu za ‘siriazi’ na za uchekeshaji.

IJUMAA WIKIENDA: Kwenye filamu yako ya kwanza ya Karibu Kiumeni umecheza kama nani?

IDRIS: Nimecheza kama jambazi na kijana anayefanya biashara haramu ya dawa za kulevya.

IJUMAA WIKIENDA: Umewahi kutumia dawa za kulevya kwenye ujana wako au kufanya biashara ya dawa za kulevya?

IDRIS: Sijawahi kutumia dawa za kulevya za aina yoyote na wala sijawahi kufanya biashara ya namna hiyo tangu nizaliwe.

IJUMAA WIKIENDA: Unatoa ushauri gani kwa jamii na watu wanaotumia dawa za kulevya?

IDRIS: Dawa za kulevya ni hatari kwa afya zetu na Watanzania wanajua, lakini kuna baadhi ya watu ni ving’ang’anizi bado wanaiga tabia za nje ya nchi na kutumia dawa za kulevya. Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana kama tutakubali kubadilisha mfumo wa maisha yetu na kufanya kazi kwa bidii ili kujenga Taifa letu kwa kutumia akili na vipaji tulivyojaliwa.

IJUMAA WIKIENDA: Vipi kuhusu uhusiano wako wa kimapenzi na mwanadada Wema Sepetu?

IDRIS: Uhusiano wa kimapenzi mimi na Wema Sepetu umekwisha muda mrefu na kila mtu anafanya mambo yake, lakini ni marafiki wazuri sana. Tunapenda kutaniana mno kila tunapokutana. Ni rafiki mzuri.

IJUMAA WIKIENDA: Tangu mlipoachana ni muda gani umepita?

IDRIS: Kwa kweli muda ni mrefu mno. Ina maana hata wewe hukumbuki!

IJUMAA WIKIENDA: Vipi kuhusu kupigiana simu na kupeana ushauri wa mambo mbalimbali?

IDRIS: Kuhusu kupigiana simu na kupeana ushauri hapana, lakini kama tukikutana sehemu tunaongea kawaida na maisha yanasonga mbele.

IJUMAA WIKIENDA: Vipi kuhusu mpenzi wako wa sasa ni nani, mbona hatukuoni naye kama ilivyokuwa zamani wewe na Wema Sepetu?

IDRIS: Nimeamua kuishi tofauti na maisha ya zamani, sitaki kuweka wazi uhusiano wangu kwa sasa.

IJUMAA WIKIENDA: Kwa nini hutaki kuweka wazi uhusiano wako, ni kitu gani unaogopa au unaogopa kuibiwa mpenzi?

IDRIS: Aaah! (kicheko) kitu ambacho kinanifanya nisiweke wazi uhusiano wangu wa sasa ni kutokana na watu kufuatilia maisha yangu ya uhusiano kuliko kazi zangu, kila mara utasikia Idris leo kafanya vile na kesho vile kuhusu mapenzi tu.

Sipendi kuzungumzwa zaidi kuhusu maisha yangu ya kimapenzi, napenda mashabiki wazungumzie zaidi kuhusu maisha ya kazi zangu.

IJUMAA WIKIENDA: Kwenye maisha ya uhusiano kuna vitu ambavyo unavizingatia kama mwanaume ili kuwa na mpenzi, je, ni vitu gani?

IDRIS: Napenda kuwa na mwanamke mwenye mvuto zaidi, tena anayejua kupendeza, nikisema kupendeza namaanisha kuanzia mavazi hadi ‘make up’ zake.

Tena awe mdada mzuri kwa sababu napenda kuwa na watoto wazuri, hata ikitokea nimempa mimba tuzae watoto wazuri. Mwanamke wa aina hiyo ndiye ananinyima kabisa usingizi.

IJUMAA WIKIENDA: Ni kitu gani ambacho msichana asipoweza kukifanya huwezi kuwa naye kwenye uhusiano?

IDRIS: Msichana ambaye hawezi kuongea lugha ya Kingereza siwezi kuwa naye kwenye uhusiano, napenda kuwa na mtu ambaye anajua kuongea lugha hata mbili, ikiwamo Kiswahili na Kingereza au zaidi ya lugha hizo.

IJUMAA WIKIENDA: Unapendelea kufanya nini pindi ukiwa na mawazo?

IDRIS: Mara nyingi nikiwa na mawazo napenda kuendesha gari muda wa usiku wa manane au kufanya kazi za nyumbani, ikiwamo kupika.

IJUMAA WIKIENDA: Unaweza kuwa na uhusiano wa kimapenzi na zaidi ya msichana mmoja?

IDRIS: Hapana, siwezi kuwa na uhusiano na zaidi ya msichana mmoja, kwani ninayaheshimu mapenzi.

IJUMAA WIKIENDA: Ni sahihi kushikiana simu na mpenzi wako?

IDRIS: Sina jibu sahihi, lakini sipendi kushika simu ya mpenzi wangu kwa sababu kila mtu ana uhuru na simu yake.

IJUMAA WIKIENDA: Ni kitu gani unakikosa kutokana na ustaa wako?

IDRIS: Watu wanashindwa kuniamini. Kwa mfano, nikimtaka mdada nikimwambia nampenda yeye anahisi ninamtania au ninachekesha kutokana na kazi yangu ya uchekeshaji kuna kipindi ninajikuta nakosa hadi mtu wa kuwa naye kwenye uhusiano.

IJUMAA WIKIENDA: Idris mashabiki zako wategemee nini kutoka kwako?

IDRIS: Mashabiki wangu na wapenzi wa kazi zangu wakae mkao wa kula, kwani kuna kazi nyingi kutoka kwangu zinakuja.

IJUMAA WIKIENDA: Asante Idris.

IDRIS: Asante pia, karibu tena kwa sababu ninyi ni wadau muhimu katika kukuza kazi zangu.

MAKALA: IMELDA MTEMA, BONGO

Leave A Reply