The House of Favourite Newspapers

IBRAAH: Nimesota Sana kwa Harmonize

0

JINA halisi ni Ibrahim Abdallah almaarufu Ibraah. Huyu ni kijana mwenye kipaji kikubwa cha muziki katika uandishi wa mashairi matamu na uimbaji. Hizi ndizo sifa kuu ziliyomshawishi CEO wa lebo ya muziki ya Konde Gang Music Worldwide, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ kumsajili na kumtambulisha rasmi kama msanii wa lebo hiyo.

 

Ni msanii wa kwanza kusajiliwa katika lebo hiyo. Nimekubali ni ngoma mpya ya Ibraah ambayo imepita kwenye mikono ya Producer Kapipo. Inafanya poa sana kwenye Mtandao wa YouTube kwa kuwa na watazamaji zaidi ya laki tano.

Leo ndiyo anazindua EP (Extended Playlist) yake inayokwenda kwa jina la STEPS yenye mjumuiko wa nyimbo zake na kolabo na wasanii wengine.

 

Gazeti la IJUMAA limekusogeza karibu na Ibraah baada ya kubonga naye kwenye mahojiano maalum (exclusive) ambapo amefunguka mengi ikiwemo ishu nzima ya kusota sana kwenye Lebo ya Konde Gang kwa muda mrefu bila kukata tamaa hadi akafanikiwa. Ungana naye;

 

IJUMAA: Mashabiki wako wangependa kufahamu wewe ni mzaliwa wa mkoa gani?

IBRAAH: Mimi ni mzaliwa wa Mtwara Wilaya ya Tandahimba.

IJUMAA: Ni mwaka gani ulianza muziki?

 

IBRAAH: Nimeanza rasmi muziki mwaka 2011 ila kabla ya hapo nilikuwa naimba tangu nikiwa darasa la pili.

IJUMAA: Ni nani aliyegundua kipaji chako?

IBRAAH: Aliyegundua kipaji changu ni mjomba wangu aitwaye Duke ambaye kwa sasa ndiye meneja wangu.

IJUMAA: Je, ulipataje nafasi ya kuingia Konde Gang?

 

IBRAAH: Ukweli kabisa nafasi ya kuingia Konde Gang haikuwa rahisi kwa sababu nilikuwa nafuatilia sana shoo za Harmonize, muda mwingine nilikuwa nakosa hata nafasi ya kumuona ili nimuoneshe kipaji changu ila mjomba wangu, Duke yeye ni sehemu ya familia ya Harmonize, ndiye akanambia niwe nakwenda studio za Harmonize. Kama siku tatu hivi nakumbuka kuna siku Harmonize aliniambia anataka kunisikiliza nikiwa naimba, basi aliponisikiliza, akaniuliza baadhi ya maswali nikajibu vizuri ndiyo akanipenda hadi sasa niko Konde Gang.

 

IJUMAA: Mashabiki wangependa kufahamu ni muda gani sasa tangu umekuwa karibu na Harmonize?

IBRAAH: Uhusiano wangu na Harmonize ni mwaka mmoja na miezi mitatu sasa. Nimesota sana kwa Harmonize hadi hapa ninamshukuru Mungu nimefanikiwa kuwa chini yake.

 

IJUMAA: Ulijisikiaje siku ya kwanza Harmonize anakuita na kukusajili rasmi Konde Gang?

IBRAAH: Nilijisikia faraja sana kwa sababu ni kitu ambacho nilikipigania kwa muda mrefu sana.

IJUMAA: Unamzungumziaje Harmonize kama kiongozi wako?

 

IBRAAH: Kwanza nimpe asante, namshukuru sana kwa kunipokea kama msanii wake, kikubwa ninachopenda kumzungumzia, bosi ni mtu ambaye anapambana na anapenda maendeleo kwa kila mtu. Ni mtu ambaye ukikosea anakurekebisha unakaa sawa.

 

IJUMAA: Unaizungumziaje menejimenti ambayo upo kwa sasa?

IBRAAH: NI menejimenti ambayo ina upendo, maana ni kati ya watu ambao waligundua kipaji changu.

IJUMAA: Je, umesaini mkataba wa muda gani pale Konde Gang?

 

IBRAAH: Masuala ya mikataba bado sijapewa mamlaka ya kuyazungumzia. IJUMAA: Gemu la sasa la muziki ni gumu na kuna ushindani mkubwa ndani yake, je, umejipanga vipi?

 

IBRAAH: Najua wasanii tunatofautiana. Kwa upande wangu ninacheza na pati yangu kupitia kipaji nilichopewa na Mungu. Hivyo nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu ili kuhakikisha siwaboi mashabiki wangu. IJUMAA: Vipi kuhusiana na kolabo kati yako na Harmonize?

 

IBRAAH: Hiyo ni mipango ya Mungu, lakini kwenye wimbo wangu wa Sawa yeye ni video model wangu na naamini kila kitu kitakaa sawa, kolabo zitakuwepo tu.

IJUMAA: Hadi sasa una jumla ya ngoma ngapi?

IBRAAH: Ngoma ni nyingi na watu wakae mkao wa kula.

IJUMAA: Neno kwa mashabiki wako?

IBRAAH: Nahitaji sana sapoti yao, maana bila wao mimi siyo kitu, nawapenda sana.

Makala:Khadija Bakari

Leave A Reply