The House of Favourite Newspapers

Mwezi Mtukufu; Mwenye Kupata Heri Anapata, Mwenye Kukosa Anakosa

0

ASALAM Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh! Kila sifa njema ni zake Allah subhanahu wataala na rehema na amani ziwe juu yake Mtume Muhamad (S.A.W). Enyi Waislam wenzangu, siku za Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani zinaendelea.

 

Je, ndugu yangu, Muislam mwenzangu umejiuliza suala moja; Je, umefaidika kiasi gani na siku zilizopita? Kuwa mkweli na nafsi yako na ujifanyie hesabu ya vitendo vyako kabla hujafika siku ya kufanyiwa hesabu.

 

Ndugu Muislam mwenzangu, bado wakati upo na fursa ya kufanya mambo ya heri bado kwa ajili ya Mola wetu.

Mfungo wa Ramadhani ni muhimu katika umri wa mwanadamu, ndani yake kuna usiku mtukufu. Mwenye kuafikiwa usiku huo, basi amepata heri ya duniani na akhera.

 

Na mwenye kukosa usiku huo, basi amekosa heri ya duniani na akhera.

Ni hasara iliyoje mtu kuishi duniani miaka mingi kisha aondoke duniani patupu bila ya kupata heri ya duniani wala heri ya akhera.

 

Tafakari na uzingatie, hujui kama utafika mwakani ili uweze kufunga tena Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Watu wema walikuwa wakimuomba Allah mwaka mzima awaafikie kuweza kuzifikia siku kama hizi za heri.

Na wakifikiwa nazo huwa na furaha nyingi, kwa kupata bahati ya kuishi hadi kuweza kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

 

Ndugu Muislam mwenzangu, Mtume Muhammad Swalla Llahu ‘alayhi wasallam ametufundisha mambo mengi na ibada nyingi ambazo Muislam anaweza kuzifanya kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allah Subuhaanahu wa Taala.

Katika ibada hizo ni kama ifuatavyo; kufanya bidii katika kusali swala ya usiku na kuwahimiza watu wake nyumbani kwake kuamka kusali pamoja.

 

Kusamehewa dhambi zilizotangulia. Amesema Mtume Swalla Llahu ‘alayhi wasallam; mwenye kusimama usiku katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa Ikhlasi na kutarajia malipo kwa Allah, atasamehewa dhambi zake zote zilizotangulia.

Usiku wa ibada; katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Mtume Muhammad alikuwa akigura matandiko yake na akijitahidi kusimama usiku na kuamsha wake zake na familia yake kwa ajili ya kuswali.

 

Katika mwezi huu, zidisha juhudi kutafuta usiku wa cheo. Usiku huu ni bora kuliko miezi elfu moja. Pia ni bora kushinda vitu vyote vilivyomo duniani.

 

Mwenye kuafikiwa kupata usiku huu, basi kwa hakika amefaulu na kupata heri ya dunia na akhera. Katika mafundisho ya Mtume Swalla Llahu ‘alayhi wasallam kuhusu usiku mtukufu; Ni Sunna kuzidisha kusoma Qur’an kwa wingi, kumsifu Allah na kumtukuza na kumsalia Mtume Muhammad, pamoja na kutoa sadaka.

 

Na ni sunna kuomba dua kwa wingi. Bibi Aisha alimuuliza Mtume; Je, niombe dua gani katika usiku huu? Akamwambia sema; “Ewe Mola hakika yako wewe ni mwenye kusamehe waja wako na unapenda kusamehe. Nakuomba unisamehe.

Kwa leo naishia hapa, tutaendelea wiki ijayo kwa uwezo wake Allah.

Niwatakie Ijumaa Adhwiim. Kwa mafundisho zaidi juu ya dini ya Kiislam, ingia YouTube Chaneli ya Global TV Online na IrshaadTz.

Leave A Reply