The House of Favourite Newspapers

Ibrah Afunguka Kupoteza Mkwanja Mrefu Kinoma

0

MWEZI mmoja tu baada ya kutambulishwa rasmi kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), siku ile ya Aprili 8, mwaka huu, tayari Zuchu chini ya Diamond Platnumz alikuwa ameanza kuweka rekodi zake kwenye muziki huu mtamu wa Bongo Fleva.

 

Halikuwa jambo la kulichukulia poa hata kidogo kwa sababu hata wasanii wakubwa unaowajua huwa wanahaso sana kuweza kupenya kwenye muziki. Ukubwa huo wa mapema wa Zuchu, hata Diamond au Mondi mwenyewe hakuupata wakati akichomoka kimuziki.

 

Ndivyo ilivyokuwa kwa msanii Ibraah ambaye alitoka kwa wakati mmoja na Zuchu baada ya kusajiliwa kwenye Lebo ya Konde Music Worldwide ambayo wengi wanaitambua kama Konde Gang ya Harmonize.

 

Ngoma ya kwanza ya Ibraah chini ya Konde Gang ilikuwa ni Nimekubali. Naye ndani ya mwezi mmoja tu tangu asajiliwe Konde Gang chini ya Harmonize au Harmo, alifanikiwa kupenya kirahisi kinoma kwenye msitu wa vijana kibao ambao wanazunguka mitaani na CD zao wakitafuta namna ya kutoboa kimuziki. Hayo hayakuwa mafanikio madogo kwa msanii mpya kama Ibraah.

 

Mafanikio ya Zuchu na Ibraah, kwa asilimia 99 yanachangiwa kwa kiasi kikubwa mno na mabosi wao, Mondi na Harmo. Ikumbukwe kwamba ni vigumu mno kwa msanii mpya kuweza kutoboa kirahisi kwenye muziki.

 

Zuchu na Ibraah wamebahatika kutembelea nyota za Mondi na Harmo ambao wanataka kuona wasanii wao wakiingiza mkwanja mrefu kama wao. Zuchu na Ibraah wanapaswa kukumbuka kwamba, kila wanachofanya kinafuatiliwa na mashabiki wa Mondi na Harmo.

 

Utangulizi huo unatosha! Makala hii inamhusu Ibraah. Huyu dogo amesikika mno ndani ya miezi yake sita ya mwanzo tangu apate zali la kuchukuliwa na Harmo pale Konde Gang.

 

Ibraah amesikika na ngoma nyingi zilizokubalika kama Nimekubali, One Nighty Stand akiwa na Harmo, Nitachelewa, Wa Ndoto, Nani, Sawa, My Queen, Nakosa Raha na nyingine zilizojikusanyia mamilioni ya wasikilizaji na watazamaji kwenye mitandao ya muziki duniani. Majina yake halisi yanayosomeka kwenye kitambulisho cha Nida ni Ibrahim Abdul.

 

Ila kwa mashabiki wa muziki wake wanamtambua kwa jina la Ibraah au Chinga. Wakati Zuchu akitoboa kwa kasi ya ajabu na kuzidi kumuacha Ibraah maili nyingi, kama utakumbuka vizuri, mwezi mmoja uliopita kulikuwa na habari mbaya kwamba akaunti au chaneli yake ya Mtandao YouTube ilipotea ghafla ikiwa na wafuasi zaidi ya laki 170 kwa sababu ambazo hazikuwa wazi sana. Ila kwa sasa imerejeshwa na inakimbiza kama zamani.

 

Tunavyojua ni kwamba, wasanii wengi wa Bongo Fleva wanategemea YouTube kupiga mkwanja na maisha mengine yanaendelea hata pale msanii anapokuwa hana shoo, japokuwa malipo yake inasemekana ni ya kawaida mno. Sasa zimepita siku nyingi bila Ibraah kuposti ngoma zake kwenye akaunti hiyo na kujizolea watazamaji kama alivyofanya Zuchu.

 

OVER ZE WEEKEND imefanya mahojiano maalum (exclusive interview) na Ibraah ambaye anafunguka juu ya ishu hiyo na dizaini alivyopoteza mkwanja mrefu kionoma;

OVER ZE WEEKEND: Pole kwa kufungiwa YouTube yako kwa muda mrefu…

IBRAAH: Ahsante sana, nashukuru…

OVER ZE WEEKEND: Tumeona imerudishwa kwa sasa, unajisikiaje baada ya kurudishwa kwake?

IBRAAH: Nimefurahi sana kurudishwa kwake. Kwa sasa kazi zitaendelea kama kawaida, mashabiki wangu ninawapa pole na pia wanisamehe kwa hilo kwa sababu najua walinimisi sana.

OVER ZE WEEKEND: Kufungiwa kwa chaneli yako ya YouTube, kulisababishwa na nini hasa?

IBRAAH: Kwa kweli mimi siyo mtaalam sana wa hayo mambo, ila ninachoshukuru ni kwamba imeweza kurejeshwa kwa mara nyingine, ninawahisi mashabiki wangu waendelee kupata vitu vizuri zaidi.

 

OVER ZE WEEKEND: Kufungiwa kwa muda wote huo imekupa hasara kiasia gani, maana tunafahamu wasanii wanalipwa kwenye YouTube?

IBRAAH: Imenipa hasara sana, siwezi hata kueleza kwa kweli, maana kazi yangu mpya ndiyo ilikuwa imetoka na ilikuwa inafanya vizuri, imenikata stimu sana, si unajua mimi ni msanii mchanga na ninahitaji kufika mbali zaidi hivyo ikiwa hivyo tunarudishana nyuma.

 

OVER ZE WEEKEND: Kwa harakaharaka ni kiasi gani cha pesa ambacho umepoteza kwa kuondolewa kwa chaneli yako kwa muda wote huo?

IBRAAH: Kiukweli ni nyingi japokuwa siwezi kukuambia ni kiasi gani kwa sababu haijaonesha ni kiasi gani zilizopotea.

 

OVER ZE WEEKEND: Tukirudi kwenye muziki wako, juzikati ulisema unakwenda nchini Nigeria kufanya kitu na msanii Joe Boy, kwa nini yeye na Nigeria kuna wasanii wengi?

 

IBRAAH: Ni kweli kule kuna wasanii wengi. Nimesema Joe Boy tu kama mfano, ila ninaahidi kwamba nikifika kule nitafanya na wasanii wengine pia.

 

OVER ZE WEEKEND: Umeshatoa EP (albam fupi) yako, labda mpaka sasa mafanikio yakoje?

IBRAAH: EP yangu imekuwa ni kubwa na imeweza kufika mbali hivyo ninamskuru Mungu kwa hilo. Nilichofanya watu wamekipenda na wamekipokea vizuri.

OVER ZE WEEKEND: Imekuingizia kiasi gani cha pesa?

IBRAAH: Pesa zimeingia za kutosha, ila siwezi kusema kwa sababu hayo ni mambo ya pesa, yanapaswa kuwa mambo binafsi.

 

OVER ZE WEEKEND: Kuhusiana na mipango ya kuachia album imekaaje?

IBRAAH: Tuombe Mungu kwa sababu mimi ni binadamu, siwezi kujua kesho yangu itakuwaje.

OVER ZE WEEKEND: Mipango ya shoo za nje ya nchi imekaaje?

 

IBRAAH: Mipango iko poa kabisa, ni muda tu unasubiriwa mambo yaanze.

OVER ZE WEEKEND: Unajiona wapi kwa miaka ijayo?

IBRAAH: Ninajiona msanii kubwa sana na ni ndoto yangu ya siku zote.

OVER ZE WEEKEND: Wasanii wengi wanarudisha heshima kwa jamii kwa kutoa misaada, lakini kwako hatujaona ukifanya hivyo…

 

IBRAAH: Hicho ni kitu kizuri sana, lakini siyo lazima tufanya kwa pamoja. Kila mtu ana wakati wake wa kufanya hayo.

OVER ZE WEEKEND: Sasa hivi unaonekana ukifanya mazoezi ya mwili hasa ya ‘gym’ kwa kasi ya ajabu, kuna nini nyuma ya pazia? IBRAAH: Hakuna siri yoyote ni kiasi cha kuweka mwili sawa tu…

Makala: KHADIJA BAKARI 

Leave A Reply