The House of Favourite Newspapers

Idd Mosi ndani ya Dar Live… Sikinde, Msongonani zaidi?

0

msondo ngoma music bandMsondo Ngoma Music Band

Na Elvan Stambuli

UKIWAULIZA wapenzi wa Bendi ya Mlimani Park Ochestra au wana Sikinde Ngoma ya Ukae ni nani nguli wa sauti katika kuimba Rhumba, hawatasita kusema kuwa ni Hassan Rehani Bitchuka ‘Super Sterio’.

Nguli huyo mwenye sauti nyembamba inayopaa angani yenye uwezo wa kughani na vionjo vingine kadhaa vya muziki ndiyo iliyosababisha aitwe jina hilo.

Lakini kwa upande wa Msondo Music Band ukiwauliza swali hilohilo watakuambia ni Shaaban Dede ‘Kamchape’, mwimbaji mwenye uwezo mkubwa na mkongwe katika tasnia hiyo.

Cha kufurahisha ni kwamba ubishi wa swali hilo utamalizika kirahisi wakati wawili hao ambao ni moto wa kuotea mbali, watakapokutana jukwaa moja la Dar Live, Mbagala Zakhem Sikukuu ya Idd Mosi mwaka huu.

sikinde Sikinde ‘Ngoma ya Ukae’.

Je, nani zaidi kati ya miamba hiyo ya muziki? Meneja wa Ukumbi wa Dar Live, Juma Mbizo akijibu swali hilo alisema jibu litapatikana usiku wa Idd Mosi mwaka huu wakati bendi hizo zitakapooneshana umahiri wao, wakisindikizwa na Msaga Sumu, East African Melody na Wakali Dancers kwa kiingilio cha Sh.6,000 tu.

Kiongozi wa Sikinde, Abdallah Hemba amesema wataonesha umahiri mkubwa Idd Mosi katika ukumbi huo na watawapa mashabiki wao wimbo unaotamba sasa unaoitwa ‘Jinamizi la Talaka’ ambayo ni albamu yao mpya iliyo na vibao vinane.

“Nyimbo zote za zamani zitakumbukwa siku hiyo zikiwemo Kasimu wa Kustarehe, Selina, Talaka Rejea, Tui la Nazi,” anasema Hemba ambaye ni muimbaji atakayesaidiana na wapiga magitaa mahiri, Mjusi Shemboza, Steven Kaingilila Maufi, Tony Bass na mpiga tumba Ally Jamwaka huku drums zikipigwa na Habib Jeff.

Nyimbo zingine zilizovuma zamani ambazo nazo zitapigwa ‘laivu’ ni Hiba, Fikiri Nisamehe, Barua Kutoka Kwa Mama, Neema na kadhalika.

Msondo nao licha ya Dede, imesheheni wanamuziki mahiri kama vile Roman Mng’ande ‘Romario,’ Salehe Bangwe na bila kuwasahau Huruka Uvuruge na mzee mzima Said Mabera, mpiga solo mahiri ambaye tangu ajiunge katika bendi hiyo zaidi ya miaka 20 iliyopita hajathubutu ‘kuikimbia.’

Baadhi ya nyimbo ‘zilizogongwa’ na bendi hii na zitakazopigwa siku hiyo Dar Live ni pamoja na Kicheko, Mawifi Mnanionea, Ndoa Ndoana, Nimezama Katika Dimbwi, Mti Mkavu na Mizimu.

Mbizo amethibitisha kuwa nyimbo nyingine za Msondo zitakazochemsha mashabiki ni Wabakaji, Tabu, Pricila, Penzi la Mlemavu, Piga Ua Talaka Utatoa, Tuma, Wapambe, Asha Mwana Sefu, Ajali, Mtanikumbuka, Barua ya Kusikitisha, Mwana Mkiwa, Kalunde, Kaza Moyo, Jesca, Kwenye Penzi, Binti Maringo na nyingine nyingi.

Kwenye safu ya uimbaji Dede atasaidiana na akina Juma Katundu, Hassan Moshi William ‘TX Junior’ na Hussein Kalembo.

Kiongozi wao Saidi Mabera ataongoza safu ya wapiga magitaa ya solo na Rhythm ambao ni Ridhiwani Pangamawe na Huruka Uvuruge, Ramadhani Zahoro Bangwe na Mustafa Hamis ‘Pishuu’.

Kwa upande wa gitaa zito la besi wapo Ally Lindunga na Saad Ally ‘Sure Boy’ na Arnold Kang’ombe.

Tarumbeta zitapulizwa na kijana machachari Roman Mng’ande na Hamis Mnyupe. Dorice George atapiga tumba, drums atazikung’uta Amiri Said Dongo.

Ukikosa kuhudhuria shoo hii, utajilaumu kwani bendi hizi ni dira kwa muziki wa Kitanzania na nadra kukutana pamoja.

Leave A Reply