The House of Favourite Newspapers

Imevuja! ‘Nandy Ametupiwa Jini’

0

DUNIA ina mambo mengi sana! Unaweza kusema hivyo kutokana na aliyoyasema Mchungaji wa Kanisa la The World of Reconciliation Ministries (WRM) lililopo Kivule, Matembele ya Pili, Ukonga jijini Dar, Nabii Nicholaus Suguye kwamba mwanamuziki wa Bongo Fleva, Faustina Charles ‘Nandy’ ametupiwa jini. 

 

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, Nabii Suguye alisema Nandy alipofika kanisani hapo aligundua alikuwa ametupiwa jini na maadui zake akiwa jukwaani ili safari yake ya maisha ya kimuziki isiwe na mafanikio ambapo alijikuta akiishiwa nguvu.

AMEJUAJE?

Nabii Suguye alitoa siri hiyo hivi karibuni ambapo alisema Nandy alifika kanisani kwake na kutaka amuombee, hivyo wakati wa maombi hayo ndipo akagundua kwamba Nandy ametupiwa jini ili limmalize akiwa jukwaani, lakini Mungu akamnusuru.

 

Aliendelea kusema kuwa, Nandy alipatwa na mkasa huo kwenye moja ya shoo zake akiwa jukwaani, hivyo aliamua kufika kanisani hapo kwa maombi. “Kwanza mimi Nandy nilikuwa simjui. Nilikuwa ninaendelea na ratiba zangu, lakini ghafla niliona watu wakitaharuki, nilipouliza ni nani nikaambiwa ni Nandy. Nilipouliza Nandy ni nani, ndipo nikaambiwa kuwa ni mwanamuziki wa Bongo Fleva.

“Sasa Nandy mwenyewe nilikuwa simfahamu, nilipouliza ana shida gani, niliambiwa alifika kanisani kwangu na kuomba nimuombee. “Sasa wakati ninamuombea, ndipo nikagundua alikuwa ametupiwa kitu kibaya na maadui zake akiwa jukwaani alipokuwa akitumbuiza na kuishiwa nguvu. “Kweli, baada ya maombi alitoa ushuhuda kuwa amepata uponyaji.

 

“Nyota ya Nandy ni kali sana na kuna watu wanaitafuta sana ili waipate, mwanzo walishindwa kwa sababu ya Neema ya Mungu iliyo ndani yake, lakini mpaka anaishiwa nguvu ujue hicho kitu kilichomuingia kilikuwa hatari. “Baada ya maombi niliyomfanyia, kilitoka,” alisema Nabii Suguye.

 

NANDY AZUA TAHARUKI

Kwa upande mwingine habari zilieleza kuwa Nandy, baada ya kutinga kanisani hapo, alizua taharuki kubwa na ya aina yake kutokana na waumini kubaki wakimshangaa na kumvaa nabii wao wakimuuliza imekuwaje mwanamuziki huyo kufika kanisani hapo wakati anaimba nyimbo za kidunia”

 

Nabii Suguye alisema jibu lake lilikuwa ni rahisi kwa waumini wake kuwa mwanamuziki huyo alikwenda mwenyewe, hakumuita na siku zote wanatakiwa kujua kuwa yupo kwa ajili ya waliopotea na wenye shida mbalimbali na siyo kwa ajili ya watakatifu.

 

“Yesu alikuja duniani kwa ajili ya wenye dhambi, nami kanisani kwangu napokea wenye matatizo ili wakombolewe na wapate uponyaji, sipo kwa ajili ya walio wasafi, bali nafuata mfano wa Yesu. “Huyu Nandy nilikuwa simfahamu kabisa maana sifuatilii Bongo Fleva, nilikuja kumfahamu baada ya kuja kanisani kwangu na amekuwa akinitumia meseji sana akiniomba nimuombee kila wakati na ninamuombea kwa kweli,” alisema Nabii Suguye.

NANDY ANASEMAJE?

IJUMAA WIKIENDA lilimtafuta Nandy ili kuzungumzia suala hilo, lakini simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (SMS) hakujibu chochote.

SIYO NANDY TU

Nabii Suguye alieleza kuwa katika kanisa lake wanakwenda mastaa wengi wakihitaji maombi kutokana na mambo mbalimbali wanayopitia, hivyo watu watambue kuwa siyo Nandy tu bali wapo wengi. “Wapo mastaa wengi sana wanaokuja kwa ajili ya kutaka niwaombee, siwezi kuwataja hapa maana wapo wengi akiwemo pia mwanamuziki Barnaba. Hivyo nawapa ushirikiano kwa kuwa nimetumwa na Mungu kwa ajili ya kuwasaidia watu,” alisema Nabii Suguye

STORI: GLADNESS MALLYA, DAR

Leave A Reply