Kartra

Ishu ya Metacha Kwenda Simba Ipo Hivi

BAADA ya tetesi nyingi kuzagaa za kipa namba moja wa Yanga, Metacha Mnata kuwa njiani kujiunga na Simba kwa ajili ya msimu ujao, meneja wa kipa huyo, Jemedari Said ameibuka na kufunguka kila kitu.

Tetesi hizo zilianza kuzagaa juzi Jumanne zikimuhusisha kipa huyo kwenda Simba kumpa changamoto Aishi Manula.

 

Metacha hivi karibuni alizua sintofahamu katika klabu yake baada ya kutupia picha kwenye mtandao wa kijamii na kuandika ujumbe wa kuwaaga mashabiki na viongozi wake.Akizungumza na Spoti Xtra, Jemedari alisema kuwa anachofahamu mchezaji wake bado mali ya Yanga mwenye mkataba wa kuendelea kuichezea timu hiyo.

 

Jemedari alisema kuwa, hicho kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii ni kumchafua mchezaji wake huku akisisitiza hakuna klabu yoyote iliyomfuata kufanya mazungumzo naye.

 

Aliongeza kuwa, upo uwezekano mkubwa wa mchezaji huyo kuendelea kubakia kuichezea Yanga katika msimu ujao, kwani hivi sasa anaipa nafasi ya mazungumzo klabu yake pekee wakati mkataba wake ukielekea ukingoni.

 

“Nimechukizwa na hizo taarifa za Metacha kusaini Simba, kiukweli mchezaji wangu wanamuondoa mchezoni na kikubwa wafahamu hivi sasa yupo katika majukumu ya timu ya taifa, hivyo nishauri kuachana na tetesi hizo.

 

“Tetesi hizo zitazidi kumtoa mchezoni mchezaji wangu, kikubwa Wanayanga wafahamu kuwa Metacha bado kipa halali wa Yanga ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu.“

 

Na kama mazungumzo yakienda vizuri basi ataongeza mkataba mwingine wa miaka miwili ya kuendelea kubaki Yanga na niwatoe hofu mashabiki wa Yanga kwa kuwaambia kuwa Metacha hajafanya mazungumzo na klabu yoyote,” alisema Jemedari


Toa comment