The House of Favourite Newspapers

Rais Magufuli ‘Alivyowaaga’ Watanzania Kabla ya Kifo

0

SAFARI ya mwisho ya maisha ya Rais wa Tanzania John Magufuli aliyefariki dunia jana, imeibua majonzi na mshtuko wa kitaifa ikiwa ni siku chache baada ya kuagana na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kupitia ziara yake ya mwisho aliyozindua miradi kadhaa huku akiahidi kuboresha zaidi miundombinu ya jiji hilo.

 

 

Akitangazia Taifa jana Jumatano 17, 2021 kupitia Shirika la Taifa la Utangazaji(TBC1), Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa masikitiko na hali ya majonzi alisema siku 12 kabla ya umauti wake, Rais Magufuli alilazwa Machi 6 mwaka huu katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam kwa matibabu.

 

 

Hata hivyo, siku tisa kabla ya kuanza matibabu yake Rais John Magufuli alikutana na wakazi jiji hilo la Dar es Salaam Februari 26, akishiriki uzinduzi huku akitoa ahadi zake kwa Watanzania ambazo zilikuwa za mwisho kabla umauti kumkuta.

 

 

Akiwa katika manispaa ya Temeke, Rais John Magufuli aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza mkopo wa Sh12 bilioni uliotolewa na benki ya CRDB kwa halmashauri ya Temeke.

 

 

Siku mbili kabla ya tukio hilo, Rais John Magufuli alizindua daraja la juu la Ubungo alilolitambulisha rasmi kuitwa Daraja la Kijazi Interchange ili kutambua utumishi uliotukuka wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Marehemu Balozi Mhandisi, John William Kijazi ambaye pia alifariki dunia Februari, 17 mwaka huu.

 

 

Siku ya uzinduzi huo, Rais John Magufuli aliwahakikishia wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuwa dhamira yake ya kuliboresha jiji hilo ipo palepale na kwamba baada ya kazi nzuri ya kuzijenga barabara kuu.

 

 

“Serikali itajielekeza kujenga barabara za mitaani kwa kiwango cha lami, kujenga barabara za juu katika makutano 10 ya barabara na kuimarisha huduma nyingine za kijamii,” alisema John Magufuli akiwa katika ziara hiyo.

 

 

Alisema anakusudia kuivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na badala yake halmashauri mojawapo ya Manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam itapandishwa hadhi na kuwa Jiji ili kuondoa hali ya sasa ambapo kuna halmashauri ya jiji inayotumia maeneo ya utawala ya halmashauri za Manispaa ambapo baadaye alikuja kufanya hivyo na kuifanya Ilala kuwa halmasahauri ya jiji.

 

 

Baada ya kufungua daraja hilo, Rais John Magufuli pia alifungua Kituo cha Mabasi cha Kimataifa kilichopo Mbezi Luis jijini Dar es Salaam huku akiridhia ombi la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo aliyependekeza kituo hicho kuitwa Kituo cha Mabasi cha Kimataifa cha Magufuli kutokana na kutambua mchango wake katika uboreshaji wa jiji la Dar es Salaam na nchi nzima.

 

 

Rais Magufuli alitoa ombi kwa Waziri Jafo kwa sharti kuwa hataki kituo hicho kitumike kuwanyanyasa baadhi ya Watanzania hasa wa hali ya chini.

 

 

Aliagiza wafanyabiashara wadogo (Machinga) na Mama Lishe kuruhusiwa kufanya biashara zao badala ya kutumiwa na wafanyabiashara wakubwa pekee.

 

Leave A Reply