The House of Favourite Newspapers

Je, unazijua sifa za mwanaume anayefaa kuwa mwenza wako-2?

0

Heri ya Jumatatu ya Pasaka, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa pumzi na upendo wake kwetu. Mpenzi msomaji wiki iliyopita nilianza kuiangalia mada hii ya Je, Unazijua Sifa za Mwanaume Anayekufaa Kuwa Mwenza Wako?’ Niliishia kwenye kipengele cha asiwe mtu wa kupayuka hasa mnapokuwa mmekosana. Busara, utulivu na kujizuia ziwe sifa za kipekee kwa mwanaume unayehitaji kuwa naye kwenye maisha haya.

MCHA MUNGU
Ukibahatika kumpata mwanaume mwenye hofu ya Mungu, mara nyingi hofu hiyo ndiyo huwa muongozo katika kufanya yaliyo mema. Ni dhahiri kwamba kwa mwenye hofu ya Mungu ni vigumu kuingia kwenye dhambi ya kuzini, kusaliti, kudhulumu, kusengenya na uovu mwingine wowote dhidi ya maagizo ya Mwenyezi Mungu. Ukimpata mwanume mwenye hofu ya Mungu mtaishi kwa raha, amani, upendo na furaha na kama akikosea basi atakuwa ameteleza tu.

AWE NA MALENGO
Mwanaume mwenye malengo anastahili kuwa mwenza wako kwa sababu mtaanza katika maisha duni lakini baada ya muda, mtakuwa sehemu f’lani na malengo ya kufikia kile alichokikusudia.

AJUE KUTAFUTA MBADALA WA TATIZO
Mwanaume anayekufaa ni yule anayejua kutatua tatizo na si kulalamika. Mara nyingi imezoeleka kuwa wanaolalamika ni wanawake.

ASIKATE TAMAA
Awe mwanaume asiyekata tamaa katika misukosuko anayokutana nayo kwenye maisha na hata uhusiano wake wa kimapenzi.

AWE MBUNIFU
Mwanaume anayekufaa lazima awe na uwezo wa kubuni mbinu za kujikwamua katika maisha magumu.

AJUE KUJITUMA
Mwanaume anayekufaa ni yule mwenye uwezo na nguvu za kujituma kuhakikisha mpenzi wake anapata anachokitaka.

AJUE MAJUKUMU YAKE
Ni vizuri umpate mwanaume anayeyajua majukumu yake ipasavyo kwa maana ya majukumu ya kifamilia na majukumu ya faragha au kukuridhisha.
Lazima ajue nini mkewe anahitaji. Anapaswa kuhakikisha mkewe anapata kile anachostahili, kama malazi, mavazi, chakula nakadhalika.

KIUHUSIANO
Mwanaume wako lazima awe ni yule mwenye uwezo wa kukuridhisha wewe mwanamke mnapokuwa faragha, hakuna kitu kizuri katika uhusiano kama mtu kufurahia utamu wa uhusiano wake. Kuridhika ni moja ya vitu vizuri na vitamu mno katika uhusiano. Na kama mwanaume ana uwezo wa suala hilo, hata kuvumiliwa baadhi ya mambo yake ni rahisi sana kwa mwanamke kuamini labda pengine atabadilika.
Kwa wapenzi kufahamiana ni jambo jema kwani litasaidia kubadili au kutengeneza baadhi ya tabia zao.
Kujitengeneza huko kunahitaji dhamira ya dhati kutoka ndani ya mioyo yako, asili ya vile walivyoumbwa na msaada mkubwa wa Mungu.
Usikose wiki ijayo kwenye mada nyingine tamu, pia tembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Insta:mimi_na_uhusiano au kwenye group letu la WhatsApp kwa kutuma ujumbe wa jina lako, umri na ulipo kwa namba zilizo hapo juu.

Leave A Reply