The House of Favourite Newspapers

Jide; Tajiri wa Kolabo Bongo!

0

UNAPOZUNGUMZIA wasanii waliofanya kolabo nyingi ndani na nje ya Bongo, kamwe huwezi kuliweka pembeni jina la Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ au ukipenda unaweza kumuita Jide.

 

Mwanamke huyu wa shoka kutokana na uwezo wake, kupitia mishale mingi ndani ya muziki wa Bongo Fleva, amepewa majina mengi tu ikiwemo Binti Machozi, Anakonda na Komando.

 

Kwa takriban miaka 20 sasa ndani ya Bongo Fleva, amefanya vizuri na mpaka sasa hakuna msanii wa kike ambaye amevunja rekodi ya kushirikiana na wasanii wengi kimuziki kama yeye.

Twende tukazitazame kolabo zake moja baada ya nyingine:

 

NA SUGU…

Mambo ya Fedha, huu ni wimbo ambao mkali huyu alishirikiana na mkali wa Hip Hop Bongo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.

Wimbo huo ulibamba sana na bado mpaka sasa ukipigwa, bado ni mkali.

 

NA PROF JAY…

Lady Jaydee amefanya nyimbo kadhaa na msanii Joseph Haule ‘Profesa Jay’; Mbunge wa Mikumi na nyimbo hizo ni pamoja na Bongo Dar es Salaam, Ndio Mzee na Niamini.

 

NA AY…

Wimbo mwingine ambao ulibamba sana, ulikuwa ni ‘Machoni Kama watu’ ambao aliufanya na mkali ya Bongo Fleva, Ambwene Yesaya ‘Ay’. Wimbo huu ulibamba sana na kufanya mashabiki wa Bongo Fleva kupata ladha tofauti kutoka kwa wawili hao.

 

NA MANDOJO NA DOMOKAYA…

Cheche za Jide zimesikika pia kwenye Wanoknok, ngoma inayomilikiwa na wakali wa kurap; Mandojo na Domokaya. Hawa ni wasanii ambao walikuwa wakifanya kazi pamoja na wimbo huo ulikimbiza sana kwenye game miaka ya nyuma.

 

NA MR. BLUE

Kichupa kingine ambacho alikifanya akiwa na mwanamuziki wa Bongo Fleva ambaye hadi sasa anatamba katika Bongo Fleva ingawa ana familia yake, Herry Sameer ‘Mr Blue’ wimbo unaitwa ‘Sema’.

 

NA CHEGE

Mke huyu wa zamani wa mtangazaji Gadna G. Habash, aliwahi pia kufanya ngoma ya Mambo Bado, akishirikishwa na mtoto wa Temeke; Chege Chigunda a.k.a mtoto wa mama Said.

 

NA MIKE TEE

‘Hali Halisi’ ni wimbo ambao aliufanya akiwa na mwanamuziki wa Bongo Fleva; Mike Mwakatundu ‘Mike Tee’ au Mnyalu, wimbo ambao sauti yake ilipenya na kuleta utofauti.

 

NA KIBA

Kuonesha kuwa Jide ni hatari, alisikika pia kwenye ngoma ya ‘Single Boy’ ambayo alishirikishwa na Ally Saleh Kiba ‘Ally Kiba’ na kufanya wimbo uvutie.

 

Na Q CHIEF

‘Zamani’ ni moja kati ya nyimbo bora kuwahi kutokea kwenye Bongo Fleva. Wimbo huu unamilikiwa na Abubakar Katwila ‘Q-Chief’ lakini humo ndani, Jide naye alihusika.

 

Na MATONYA

Anita uliwahi kuwa wimbo wa taifa kwa wakati huo. Kwenye kiitikio cha wimbo huo unaomilikiwa na Matonya, sauti tamu ya Jide ilisikika lakini kama hiyo haitoshi, aliua na vesi kabisa. Aliunogesha kwelikweli wimbo huo, ukapanda sana kwenye chati za Bongo Fleva.

 

Na EAST COAST TEAM…

‘Ama Zangu Ama Zao’ ni moja kati ya nyimbo nzuri sana za makundi kuwahi kutokea kwenye ramani ya Bongo Fleva.

Hii ilifanywa na kundi la muziki la East Coast Team ambao walikuwa ni muunganiko wa wanamuziki AY, FA, GK, O-Ten na Snare.

 

NYINGINE KIBAO…

‘Nimpate Wapi’ ngoma hii alishirikishwa na msanii Rich Longomba. Wimbo wa ‘Nitafanya’ hii alishirikiana na msanii kutoka Kenya; Kidum.

 

‘Sirimba’ alifanya akiwa na Ngoni. Wimbo wa Njalo- Zumba ambao umeibwa na Mina Nawe kutoka Afrika Kusini.

Sikiliza na Mapenzi Gani, alishirikiana na aliyekuwa mkali wa Bongo Fleva kutoka Morogoro, Albert Magwea ‘Ngwair’.

 

Kuna Pesa ambao alishirikiana na msanii wa Hip Hop, marehemu Langa Kileo ‘Langa’. Kuna Kilimanjaro alioshirikiana na Joh Makini.

Kama hiyo haitoshi, Kadi na Ua Rose alishirikiana na Fareed Kubanda ‘Fid Q’.

Usisahau kuhusu Sifai aliyoshirikishwa na mkali wa Bongo Fleva; Khaled Mohamed ‘TID’.

Juzikati ametokelezea kwenye wimbo wa Wife ambao ameshirikishwa na Harmonize.

Leave A Reply