The House of Favourite Newspapers

Jini Mauti-12

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Ndugu yangu, haya ninayokuandikia hapa yalinitokea, uchawi upo, uchawi unaua na katika miaka mingi ya kufanya uchawi, sikuona faida yake zaidi ya kupewa Jini Mauti ambalo liliyagharimu sana maisha yangu.
SASA SONGA NAYO…

Siku hiyo nilipelekwa makaburini, japokuwa niliogopa sana kufika huko hasa nyakati za usiku lakini kitu cha kushangaza, siku hiyo sikuwa nikiogopa chochote kile.

Tulifika kwenye makaburi hayo, wachawi wakasimama juu ya kaburi moja la mtoto na kuanza kuongea maneno ambayo kwa kipindi hicho, sikuwa nikiyafahamu, ghafla nikaanza kuliona kaburi lile likianza kujifukua na sauti kali za paka kusikika na baada ya dakika kadhaa maiti ya mtoto ikatoka kaburini.

Sikuwa na hofu, moyo wangu ulibadilishwa na kuwa wa kichawi, kila kitu kilichotokea, nilionekana kukizoea japokuwa ndiyo ilikuwa siku yangu ya kwanza.Hiyo ndiyo ikawa safari yangu ndefu ya kuwa mchawi, nikaanza kuzoea na kuzoea, nikafundishwa mambo mengi likiwemo la kupaa na ungo, kuwaroga watu na hata kupanga mapambano dhidi ya wachawi wengine, yaani kwa kifupi, nilikuwa hatari kwenye uchawi.
****
Miaka saba ikapita, nilikuwa mchawi kamili, katika kipindi chote hicho sikutaka kumuoneshea mama kitu chochote kile, sikutaka ajue kwani nilijua namna alivyokuwa akimchukia bibi mara baada ya kuniingiza kwenye uchawi.
Alilalamika sana kuhusu bibi, lakini kitu cha ajabu, kila alipokuwa akinifuatilia, hakubaini kama nilikuwa mchawi. Nilimaliza darasa la saba na hatimaye kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Mkuyuni iliyokuwa Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Katika kipindi hicho nilikuwa nimepevuka, nilivunja ungo na kwa kweli nikajiona kuwa kwenye nafasi ya kuwa na mpenzi wangu. Marafiki zangu wa kike akiwemo Anita na Maria, kila mmoja alikuwa na mpenzi wake, waliniambia kwamba na mimi nilitakiwa kuwa na mpenzi lakini kwangu nililiona suala hilo kuwa gumu.

Ulipofika mwezi wa sita ndipo macho yangu yakatua kwa mvulana mmoja, alikuwa mzuri wa sura, shuleni alikuwa msafi sana, kila alipokuwa akitabasamu, uzuri wake ulionekana dhahiri, mvulana huyu alikuwa akiitwa Thomas.
Ninaposema mzuri wa sura, ninamaanisha kwamba Thomas alikuwa mzuri hasa.
Wasichana wengi walimtaka kimapenzi lakini hakuwa mtu wa namna hiyo, hakuwa mtu wa kupenda wasichana kabisa.

Naye alikuwa kidato cha kwanza kama nilivyokuwa mimi lakini kitu cha kushangaza, hata wasichana wa kidato cha nne walimtaka kimapenzi. Niliogopa kumwambia ukweli, kila nilipopishana naye, nilijisikia kitu cha tofauti moyoni mwangu, mapenzi yaliukaba moyo wangu.

Kwa kuwa nilikuwa mchawi, nyakati za usiku nilimfuata Thomas chumbani kwake, nilisimama pembeni yake, nilikaa kitandani kisha kuanza kumwangalia. Japokuwa pamoja na uchawi wote huo lakini Thomas alikuwa kipenzi cha moyo wangu.

“Thomas, ninakupenda mno, kuwa wangu,” nilisema kila nilipomfuata chumbani usiku.
Kwa mwaka huo wa kwanza shuleni hapo, moyo wangu uliteseka sana, mpaka mwaka unakwisha na kuingia kidato cha pili, sikuwa nimemwambia ukweli. Naomba niwaambie kitu kimoja.

Nilikuwa na uwezo mkubwa wa kumfanya Thomas anipende sana, asilale kwa ajili yangu lakini kilichonifanya kutokufanya hivyo ni kwamba nilihitaji anipende kwa moyo wa dhati kwa hiari yake na si kwa kutumia uchawi.
Nilimuogopa Thomas, labda kwa sababu alikuwa mvulana mwenye akili nyingi darasani zaidi ya mwanafunzi mwingine. Nilivumilia na kuvumilia lakini mwisho wa siku nikaona kwamba uvumilivu wangu unakwenda mwishoni, nilichokifanya ni kumfuata huku nikiwa nimeupiga moyo konde.

“Thomas,” nilimuita mvulana huyo, alikuwa akiondoka kuelekea kwao, aliposikia nimemuita, akasimama na kugeuka nyuma, akaniangalia usoni.“Davina…” alilitamka jina langu, nikashtuka kuona kumbe alikuwa akinifahamu.
Je, nini kiliendelea? Usikose wiki ijayo.

Nikamsogelea pale aliposimama, mapigo yangu ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu, kwa mbali kijasho chembamba kikaanza kunitoka, mwili wangu ulisisimka kupita kawaida. Thomas akaachia tabasamu pana, tabasamu lililouburuza vilivyo moyo wangu, nikajiona kama nimekutana na malaika.

Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply