The House of Favourite Newspapers

Jini Mauti-14

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Aliponiachia na kugeuka, moyo wangu ukapiga paaa, alikuwa Thomas. Uso wake ulitawaliwa na tabasamu pana, alionekana kuwa mwenye furaha mno, nilipoyaangalia macho yake yalionesha ni jinsi gani alifurahi kuniona. Endelea…

“Thomas…” niliita.
“Niambie mpenzi,” aliniambia, kwa kweli nikashtuka sana, Thomas huyuhuyu ambaye alikuwa akinikataa, leo hii eti aliniita mpenzi.
“Mpenzi?” niliuliza.

“Ndiyo! Naomba unisamehe Davina,” aliniambia huku akiniangalia kwa jicho la mahaba.
“Nikusamehe kwa lipi?”

“Nilikuwa kipofu, sikugundua uzito wa penzi lako kwangu, nimekaa na kujifikiria, huu ni muda wa kuwa nawe Davina, ninakupenda mno,” aliniambia huku akionekana kumaanisha.

“Kweli?” niliuliza huku nikionekana kutokuamini.
“Haki ya Mungu tena! Ninakupenda mno Davina,” aliniambia Thomas.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa kila kitu, penzi jipya likafunguliwa katika maisha yetu.

anafunzi wengi walishangaa kwamba iliwezekanaje mvulana mwenye sura nzuri kama Thomas ababaike nami na wakati kulikuwa na wasichana wengi wazuri waliomtaka?
Wengi walijua kwamba Thomas alichanganyikiwa kutokana na umbo langu la kujazia nyuma.

Hapo ndipo nilipoanza kupata maadui wengi, wa kwanza kabisa alikuwa Agape. Msichana huyu alinichukia mno, alimpenda sana Thomas lakini mwisho wa siku, akaona nimemzidi kete kwa kuwa na mvulana huyo.

Si mimi peke yangu niliyechukiwa bali hata kwa Thomas ilikuwa hivyohivyo. Mudi, kijana aliyekuwa akinipenda mno naye akaanza kuonesha chuki kwa Thomas, hakumpenda kwa kuwa alinichukua.

“Davina, yaani unanikataa mimi?” aliniuliza Mudi.
“Ndiyo! Sikutaki Mudi.”
“Davina! Ninakupenda mno jamani, hebu nionee huruma, machozi yote haya kwa ajili yako bado haunipendi?” aliuliza Mudi.

“Najua Mudi, ila samahani, huna nafasi kwangu.”
Maumivu ya Mudi niliyaona machoni mwake, moyo wake uliumia mno ila hakuwa na jinsi, alitakiwa kukubaliana na ukweli kwamba sikutakiwa kuwa naye kwa kuwa sikuwa nikimpenda.

Mapenzi yangu na Thomas yakawa makubwa, tulipendana kiasi kwamba mpaka shuleni walituita KIMNYE wakiwa na maana ya Kim na Kanye.
Baada ya siku chache nikamwambia twende nyumbani nikamtambulishe, akakubali, tukaelekea huko na kumtambulisha kwa mama.

Hatukuishia hapo, tulichokifanya ni kwenda na nyumbani kwao pia, akanitambulisha kwa wazazi wake kama rafiki yake pekee, wakanikaribisha kwa furaha mno.

Dawa ile ikamfanya kuchanganyikiwa mno, akawa hali wala halali, wakati mwingine aliondoka kwao usiku na kuja nyumbani wakati nimelala, anagonga dirishani, natoka nje na kuzungumza naye, nikimuuliza kwa nini usiku, ananijibu kwamba alinikumbuka mno na asingeweza kulala.

Baada ya kukaa kwa muda wa wiki mbili katika uhusiano huo ndipo Thomas akaniambia kwamba kama tulivyokuwa wapenzi basi lingekuwa jambo la maana kudhihirisha kwamba sisi ni wapenzi.

“Kivipi?”
“Tufanye mapenzi?”
“Unasemaje?”
“Tufanye mapenzi!”

Kiukweli niliogopa mno lakini sikuwa na jinsi. Thomas alikuwa kila kitu kwangu, kufanya kitu hicho kiliashiria kwamba lingelikomaza penzi letu, tupendane zaidi na kuwa zaidi ya tulivyokuwa.

Tukapanga siku, kwa Thomas aliona kama siku zikichelewa kufika ila kwangu siku zilionekana kwenda kwa kasi zaidi ya siku nyingine.

Siku ya tukio ilipofika, Thomas akaniambia niende kwao kwa kuwa siku hiyo alijifanya anaumwa na hivyo hakwenda shuleni, kisingizio hichohicho ndicho nilichomwambia mama.

Nyumbani kwao alikuwa yeye na mfanyakazi wa ndani tu, hakukuwa na mtu mwingine. Kweli nikaenda. Akanipokea kwa furaha, mabusu mfululizo, kilichofuata ni kwenda chumbani kwake. Mapigo ya moyo yalinidunda kwa nguvu, niliogopa mno.
Je, nini kitaendelea?

Nini kitatokea wakifanya mapenzi?
Tukutane wiki ijayo

Leave A Reply