The House of Favourite Newspapers

Jini Mauti-8

0

Siku hiyo mama alikuwa na mawazo mno, hakuamini kama tayari alikuwa amefika jijini Dar, sehemu aliyoipenda mno. Usiku ulipoingia, mama hakutaka kulala, aliogopa sana kwa kuwa alitishwa na uchawi aliokuwa nao bibi.

Endelea sasa…Ilipofika saa sita usiku, ghafla akaona moshi mzito ukianza kuingia ndani ya chumba kile kutokea nje kupitia dirishani, hakujua ule moshi ulikuwa wa nini, hakujua ni nani alikuwa akiunguza kitu.

Akaanza kukohoa, alichohisi ni kwamba, inawezekana kule nje kulikuwa na mtu aliyekuwa akiunguza kitu, alichokifanya ni kusimama kwa lengo la kutoka nje, alipokishika kitasa na kutaka kuufungua mlango, haukufunguka.

Alichanganyikiwa, moshi ule ulizidi kuingia ndani ya chumba kile kiasi kwamba mpaka kitu kilichokuwa jirani hakuweza kukiona kutokana na wingi wa moshi huo. Ghafla, huku hali ikiwa hivyo, akaanza kusikia sauti za paka chumbani humo na sauti za watu waliokuwa wakitoa vicheko vya kejeli.

Mama aliogopa mno, sauti za paka wale na vicheko vile viliendelea kusikika kwa juu zaidi.

Huku akionekana kuchanganyikiwa kabisa, mara akasikia mtu akikohoa, alipoangalia, bibi alisimama mbele yake, japokuwa kulikuwa na moshi mkubwa lakini alishangaa ni kwa namna gani aliweza kumuona bibi, tena akiwa ameshika uleule mkoba.

“Chukua mkoba wangu Stellah,” alisema bibi huku akimwangalia mama kwa macho yaliyojaa ghadhabu.

“Sitaki kuchukua, sitaweza kuuchukua, sitaki kuwa mchawiiiii,” alipiga kelele mama.

“Nimesema chukuaaaaa….”

“Sichukuiiii,” alipiga kelele mama.

Bibi akapata ghadhabu zaidi, hapohapo akamshika mama mkono, ghafla akapotea naye. Walipotokea ni sehemu fulani iliyokuwa na mwanga hafifu, mbele yao kulikuwa na shimo kubwa lililokuwa likifoka moto mkubwa huku sauti za watu wakilia zikisikika, walikuwa wakiunguzwa katika moto ule.

Akamchukua mama na kumsogeza karibu na shimo lile kubwa na kumwambia aangalie ndani. Kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa wakihangaika huku na kule, walikuwa wakipiga kelele huku wakiomba kutolewa ndani ya shimo lile lililoonekana kuwa na mateso makali.

Mama aliogopa mno, akaanza kumuomba msamaha bibi japokuwa hakujua kama alifanya kosa lolote lile, alidhani kwamba naye angeingizwa ndani ya shimo lile.

Bibi akamwangalia kwa dharau kisha kumchukua na kumpeleka sehemu moja iliyokuwa na vyumba vingi, akafungua mlango wa chumba kimoja na kumuingiza ndani. Mule kulikuwa na kiumbe kimoja cha ajabu sana, kilikuwa kikimchapa mtu fulani fimbo za mgongoni.

Mgongo wote ulikuwa ukitoka damu, mtu yule alipiga kelele za maumivu lakini kiumbe kile cha ajabu hakikuacha, kiliendelea kumchapa mfululizo.

“Yule mpumbavu ni kama wewe,” alisema bibi na kuendelea:

“Alikataa kuchukua mikoba ya baba yake, sasa hivi anaiona joto ya jiwe,” alisema bibi.

Mama aliogopa zaidi, kila alipokuwa akimwangalia mtu yule kwa jinsi alivyokuwa akiteswa kwa kuchapwa fimbo, moyo wake ulimwambia ni lazima akubaliane na bibi kuchukua mikoba ile, yaani awe mchawi.

Kweli awe mchawi? Aroge kama wachawi wengine? Apae na ungo? Akusanyike kwenye umati wa watu akiwa uchi wa mnyama? Aende kwenye makaburi usiku? Kila alipokuwa akijiuliza maswali hayo, jibu lake la mwisho ni kwamba isingewezekana kuwa mchawi.

Bibi hakutaka kukaa naye sana, akamrudisha chumbani mule, mama akashtuka, akajiona akiwa kitandani, jasho lilimtoka, kilichomshangaza, moshi ule, sauti zile za paka na vicheko vya watu, vyote havikuwepo.

***

Mzee yule alirudi katika chumba kile, alimkuta mama akiwa kwenye hali ya huzuni mno huku macho yake yakiwa mekundu sana. Alijaribu kumbembeleza na kumtaka anyamaze kwani alikuwa na mipango ya kumsaidia maishani mwake.

Mama alikuwa msiri, hakutaka kumwambia mzee yule kilichokuwa kimetokea, alikubali kubembelezeka na mwisho wa siku kuanza kuongea mambo mengine kabisa.

Mzee yule aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah alimwambia mama ukweli kwamba alimpenda mno na alitaka kuwa naye kimapenzi.

 

 

 

 

“Una mke?”

“Ndiyo! Ila ninakupenda, nipo tayari kwa lolote,” alijibu mzee Abdallah huku akionekana kumaanisha.

“Sawa! Nipangishie chumba na unifungulie biashara,” alisema mama.

“Hakuna tatizo.”

Mapenzi ni mapenzi tu, mzee Abdallah alitekwa sana na mama, akajikuta akifanya kama alivyoambiwa, baada ya siku tatu, mama akahamia katika chumba kimoja kilichokuwa Tandale kwa Mtogole huku akimfungulia biashara ya kuuza madela.

Mama alifurahi mno, katika kipindi chote hicho hakuwa amemwambia kama alikuwa mjauzito na hicho ndicho kitu kilichomuumiza sana kichwa chake. Alihisi kwamba kama angemwambia basi huo ndiyo ungekuwa mwisho wake.

Kitu kilichokuja akilini mwake ni kuitoa mimba ile. Hakutaka kujifikiria, akajipanga vilivyo, akapanga siku ya kwenda katika maabara ndogo kwa ajili ya kufanya kazi hiyo, siku hiyo ilipofika, akaelekea huko.

“Mimba haiwezi kutolewa hii,” alisema daktari.

“Kwa nini?”

“Imekaa ndivyo sivyo, kama nikisema niitoe, utakufa.”

“Unasemaje?”

“Huo ndiyo ukweli.”

 

Leave A Reply