The House of Favourite Newspapers

Sharobaro amfanyia fujo Dk. Magufuli…

0

Richard Bukos, Kilimanjaro

 Wahenga walisema utakiona cha mtema kuni! Ndivyo ilivyomtokea kijana anayedaiwa ndiye sharobaro maarufu eneo la Himo katika Jimbo la Vunjo, Kilimanjaro aliyejitambulisha kwa jina la Steven Charles baada ya kumfanyia fujo mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli katika jimbo hilo wakati akinadi sera  zake.

Katika tukio hilo lililoshuhudiwa na Ijumaa Wikienda lililokuwa eneo la tukio, Dk. Magufuli akiwa anaendelea kumwaga sera katika mkutano huo uliohudhuriwa na umati mkubwa, Steven alidaiwa kuanzisha fujo katikati ya umati huo na kusababisha mkutano kutawaliwa na vurugu huku watu wakishindwa kumsikiliza mgombea huyo.

Vurugu hizo zilipoongezeka, Dk. Magufuli alisimamisha zoezi la kunadi sera zake na kuwaomba wanausalama kumdhibiti kijana huyo aliyekuwa akifanya vurugu wakati akizungumza na wakazi wa eneo hilo.

Baada ya kusikia amri hiyo, kundi la maafande wa FFU almaarufu Fanya Fujo Uone lilikwenda kumchomoa Steven sehemu aliyokuwa akihamasisha vurugu na kumbeba msobemsobe huku wamemkwida shati na kwenda kumtia kwenye karandinga.

Shuruba alizozipata kijana huyo ndani ya dakika kama nne zilitosha kabisa kulinganisha kibano hicho na kilichomtoa khanga manyoya kama isemavyo kauli ya wahenga.

Leave A Reply