Jini Mweusi 48

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam kufuatia kupotea mfululizo kwa machangudoa katika mazingira ya kutatanisha. Taharuki kubwa inazuka kwani ndani ya kipindi kifupi tu, zaidi ya machangudoa kumi na moja wanapotea na hakuna anayejua walikopotelea.

Jambo hilo linasababisha jeshi la polisi kuingilia kati. Kinachozidi kuzua utata, wote wanapotea katika mazingira yanayofanana. Mwanaume mmoja asiyejulikana, aliyekuwa anatembelea gari la kifahari aina ya Volkswagen, aliyekuwa akienda eneo hilo usiku wa manane ndiye anayehusishwa na wote wanaopotea.

Upande wa pili, kijana aliyekuwa na mwonekano tofauti na binadamu wa kawaida, Dickson Maduhu au Zinja kama wenzake walivyokuwa wakimtania, amejiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hisia kali za mapenzi zinasababisha kijana huyo aanze kutoka usiku na kwenda kutafuta machangudoa.  Hivyo baadaye anahamishiwa Dar es Salaam.

Mara baada ya kufanikiwa kuwa DCP, Dickson anajikuta kwenye wakati mgumu mara baada ya kumnunua changudoa, walipokuwa hotelini na kugundulika na changudoa yule kwamba ni yeye, anaamua kumuua na mwili kwenda kuuzika porini. Wakati anauzika, kulikuwa na mzee ambaye aliona kila kinachoendelea.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Uzuri wake uliendelea kuwa gumzo, machangudoa wengine waliogopa kwa kuwa kila alipokuwa, hakukuwa na biashara nzuri kwa upande wao. Kila mteja ambaye alifika mahali hapo na kumuona Pamela, hakutaka kumuacha, alimfuata na kumnunua kisha kuondoka naye au wakati mwingine kumaliza shida zake katikati ya makaburi.

Machangudoa wengi walimuonea wivu na wengine kumkasirikia, ili biashara zao ziende kama inavyotakiwa ilikuwa ni lazima Pamela aondoke mahali hapo kwani uwepo wake uliwaletea shida sana.

Baadhi ya machangudoa wakakutana na kuanza kumjadili kwamba ilikuwa ni vizuri kumfukuza au wamuache. Katika kushauriana huko, wengine wakaona ilikuwa ni lazima aendelee kubaki kwani kwa wakati huo Pamela alikuwa kivutio, wanaume wengi walifika na walipomkosa, waliwachukua machangudoa wengine.

Maisha yaliendelea kila siku, thamani yake ikaanza kupanda, akawa msichana mwenye bahati, alitengeneza kiasi kikubwa cha fedha mpaka pale alipokuja kukutana na mwanaume aliyemfuata huku akiwa na kofia kubwa kichwani, mteja aliyekuwa na muonekano wenye fedha ambaye kwake alijitambulisha kama muuzaji wa nafaka kutoka vijijini aliyejiita kwa jina la Mandingo.

“Mandingo!” alisema kwa mshangao.

“Ndiyo! Mimi ni Mkurya, huwa nasafirisha nafaka kutoka huko vijijini kuja huku mjini,” alisema mwanaume huyo.

“Aisee! Kumbe nipo na bosi!”

“Yeah! Nipo hapa kwa ajili ya kutumbua hela, zinaniwasha sana. Kwanza gharama yako inakwendaje?” aliuliza mwanaume huyo.

“Kwa sababu wewe ni mfanyabiashara mkubwa, mwenye fedha, nitakufanyia laki mbili kwa usiku mmoja,” alisema Pamela.

“Mmmh! Hakuna tatizo, kwa ajili yako, kwa jinsi ulivyo, nipo tayari,” alisema mwanaume huyo.

Huyo hakuwa mfanyabiashara kama alivyojitambulisha, alikuwa Dickson ambaye aliamua kubadilisha kiwanja cha kuchukua machangudoa na kuhamia Kinondoni Makaburini. Alipomuona Pamela kwa mara ya kwanza, moyo wake ukafarijika, alifurahia moyoni mwake kwani kwa kipindi kirefu alichokitumia kununua machangudoa, hakuwahi kukutana na changudoa aliyekuwa na umbo zuri, sura nzuri kama alivyokuwa Pamela.

Staili yake ilikuwa ileile, hakutaka kujulikana, kichwani alikuwa na kofia kubwa ya Marlboro huku kukiwa na mwanga hafifu ambao hata ulipompiga usoni, hakuonekana vizuri.

“Unaishi wapi?’ aliuliza Pamela.

“Naishi Msasani, ila hatutoweza kwenda nyumbani,” alijibu Dickson.

“Kwa hiyo tutafanyia wapi? Garini?”

“Hapana. Tutakwenda kuchukua chumba katika gesti moja uswahilini.”

“Mmmh!”

“Nini sasa?”

“Umejisifia mfanyabiashara mkubwa, halafu tuchukue gesti! Kweli jamani baby? Kwa nini tusichukue hoteli kabisa?” aliuliza Pamela huku akionekana kushtuka kwa mbali.

“Hahaha! Si unajua sisi wengine watu maarufu Tanzania, tukionekana, siyo poa kabisa,” alijitetea Dickson.

“Basi sawa. Cha msingi hela tu,” alisema Pamela.

Hakukuwa na muda wa kupoteza tena mahali hapo, alichokifanya Dickson ni kuliondoa gari mahali hapo na kuelekea katika gesti moja iliyokuwa Manzese Midizini. Hakutaka kwenda katika hoteli kubwa kwa kuwa alijua fika kwamba kugundulika ilikuwa rahisi sana tofauti na gesti bubu za mitaani.

Huko, aliamini kwamba hakukuwa na ulinzi wa kutosha, wahudumu hawakuwa na umakini wowote ule kwa wageni waliokuwa wakiingia, zaidi, wao waliangalia fedha tu. Hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kutokugundulika katika kila gesti aliyokwenda kule Mwananyamala.

Garini alikuwa mzungumzaji mkubwa, alitaka kuzoeleka kwa msichana huyo ili hata watakapofika chumbani kusiwe na maswali mengi. Hapohapo garini ndipo Dickson alipomwambia Pamela kwamba hakukuwa na kitu alichokichukia kama kufanya mapenzi katika chumba kilichokuwa na mwanga mkali wa taa.

“Kwa nini?”

“Basi tu, unajua sisi wengine tunakuwa na aibu kubwa sana.”

“MmmH! Kweli makubwa, halafu si kwako tu, mpo wengi wa namna hiyo, sijui huwa mnaogopa nini,” alisema Pamela.

Maneno hayo yakawa ahueni kwa Dickson, alijiona kuwa mshindi, kitendo cha Pamela kumwambia kwamba yeye hakuwa mmoja wake akawa na uhakika kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kuzima taa ya chumbani na hatimaye kufanya mapenzi kama alivyokuwa amepanga.

Hakuwa na hofu tena, alijua jinsi ya kucheza na wanawake hao, kuua, wala hakuogopa, alitaka kuona mambo yake yote yanakwenda sawa kama inavyotakiwa hivyo kunapotokea kizuizi chochote cha kuitunza siri ile, hakuhofia kuua hata kidogo.

Waliendelea na safari mpaka walipofika katika gesti hiyo iliyokuwa Manzese Midizini, tena kwa kuingia ndani kabisa. Walipofika, akasimamisha gari na kisha kuteremka. Katika kipindi chote hicho alihakikisha kofia yake haitoki kichwani mwake.

Vijana waliokuwa wamekaa pembeni mwa gesti hiyo walibaki wakimwangalia Pamela ambaye alikuwa akipiga hatua kuelekea ndani ya jengo hilo na Dickson ambaye hawakuwa wamemtambua kabisa.

Umbo lake liliwaacha midomo wazi, hawakuamini kama kulikuwa na mwanamke aliyekamilika kama alivyokuwa Pamela. Sura nzuri na yenye mvuto, umbo namba nane, hipsi kubwa ambazo vijana wa mitaani walipenda kuziita kwa jina la pisto.

“Nahitaji chumba.”

“Vipo. Show time au mpaka asubuhi?” aliuliza dada wa mapokezi.

“Mpaka asubuhi.”

“Elfu sita.”

“Hakuna tatizo,” aliitikia Dickson, akalipia, wakapewa ufunguo na kuelekea huko chumbani. Wakati Pamela akifikiria fedha, hakujua kama alikuwa katika mikono ya mtu muuaji. Endapo angejua, asingekubali kuelekea gesti na mwanaume huyo.

Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.


Loading...

Toa comment