Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-14

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale mganga alipowaambia mama zake Dorcas kwamba wasihofu kwani kinga atakayowapatia ni kiboko na kwamba yule mchawi kama atarudia kuwachezea angepata balaa.

Je, nini kiliendelea? Songa nayo sasa…

Tukiwa kwa yule mganga alinichanja chale sehemu mbalimbali za mwili wangu akanipaka dawa na kunuwiza kwamba mtu yeyote atakayekuja kunichezea asifanikiwe na uchawi wake umrudie mwenyewe.

“Wanangu, kwa kuwa nyinyi ndiyo wazazi wa huyu binti na mnaishi nyumba moja ni vizuri nanyi niwape kinga kwa sababu wachawi wanaposhindwa kumfikia mtu waliyemkusudia humalizia hasira zao kwa wengine,” mganga aliwaambia akina mama.

Baada ya kutoa kauli hiyo, mama mkubwa ambaye kwa sehemu alikuwa anaelewa mambo ya wachawi alikubali lakini mama alisita, mpaka leo nashindwa kuelewa sijui kwa nini marehemu mama hakupenda mambo ya kishirikina.

Hata hivyo, kwa ushawishi mkubwa wa mama mkubwa na yule mganga mama alikubali ambapo nao walichanjwa na kupakwa dawa ya kinga.

“Wanangu kutokana na hii dawa ya kinga niliyowachanjia leo msioge mpaka kesho jioni,” mganga alituambia.

Mganga huyo aliongeza kuwa, usiku tukiwa tumelala yule mama mchawi akiwa na wenzake watakuja lakini tusiwe na hofu tutakaposikia upepo ukivuma juu ya bati ni kwamba kinga yake itakuwa ikifanya kazi kuwazuia.

Mama mkubwa alimshukuru kwa taarifa hiyo na kumuuliza kama ukizidi tufanye nini, akamwambia tutulie hadi watakapoondoka.

Kabla hatujaondoa kwa yule mganga, mama mkubwa aliuliza kiasi cha fedha alichohitaji ambapo mganga alisema hakuhitaji fedha isipokuwa kuna kitu alihitaji kama angekipata hicho ingekuwa malipo ya kazi yake.

Mama mkubwa alipomuuliza ni kitu gani akasema redio kwani aliyokuwanayo iliharibika na alipenda sana kusikiliza taarifa ya habari na vipindi vingine.

Mganga alipotoa ombi hilo, mama mkubwa ambaye pale nyumbani alikuwa na redio mbili alimwambia angempelekea, mganga alifurahi sana na kabla hatujaondoka alimwita mkewe na kumwambia atufungashie maharage pamoja na mahindi.

“Wanangu nimefurahi sana kunikubalia ombi langu kwani muda sasa nashindwa kusikiliza redio hapa nyumbani,” mganga aliwaambia akina mama.

Mama alimwambia asijali angepata redio hiyo ndipo tuliwaaga ambapo walitusindikiza kidogo kisha wakarudi nasi tukaenda kupanda gari la kwenda Mbeya mjini.

Tulipofika nyumbani kabla ya kufanya kitu chochote tuliketi sebuleni na kuanza kuzungumza mambo ya kwa yule mganga, mama mkubwa alimsifia kwamba alikuwa mganga mahiri na angetusaidia sana.

“Mimi nashukuru alivyoamua kutupa kinga hata sisi, amefanya jambo la muhimu sana,” mama mkubwa alituambia.

Wakati tunazungumza hakuna aliyejua kwamba huko mbele kungekuwa na vita kubwa dhidi yetu na wachawi ambayo ingesababisha mama kupoteza maisha katika mazingira tata.

Kwa upande wangu pia sikujua mikosi ambayo ningekutana nayo likiwemo balaa la kubakwa ambalo limeharibu kabisa maisha yangu.

Tulipopumzika, niliwasha jiko nikainjika maji kwenye sufuria kubwa ambapo mama mkubwa aliniuliza yale maji yalikuwa ya nini, nikamwambia ya kuoga.

“Wewe Dorcas kwani hukusikia alichotuambia mganga kwamba leo hatupaswi kuoga hadi kesho jioni,” mama mkubwa aliniambia.

Aliponieleza hivyo, nilikumbuka ni kweli mganga alitupa sharti hilo nikaishia kucheka na kumwambia nilisahau.

“Hapo kama ungekuwa peke yako ungeoga na kuharibu kinga yote, sisi wazee ndiyo tulitakiwa tusahau lakini siyo wewe,” mama mkubwa akaniambia nikaishia kucheka tu!

Wakati tukizungumza na mama mkubwa, mama alikuwa akiendelea kuchambua mchele nami nilibadili ile sufuria na kuweka ambayo ilikuwa ikitumika kupikia wali.

Je, ni tukio gani la kutisha litawatokea usiku? Usikose Alhamisi ijayo. Maoni, ushauri nicheki kupitia namba hizo hapo juu.


Loading...

Toa comment