The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi 53

0

Alijijengea heshima kubwa nchini Tanzania kutokana na utendaji kazi wake mkubwa aliokuwa akiufaya katika jeshi la Polisi nchini Tanzania. Kutokana na umahiri wake, akajikuta akipandishwa vyeo na mwisho wa siku akijikuta akiwa Kamanda Mkuu Kanda ya Dar es Salaam, DCP.

Heshima yake inakuwa kubwa, kila anayemuona anamheshimu kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi. Pamoja na heshima zote hizo, mwanaume huyu aliyeitwa Dickson alikuwa mtu mwenye sura mbaya ambapo huko shuleni kipindi cha nyuma aliitwa kwa jina la Zinjathropus, yaani binadamu wa zamani.

Hakuwa na mchumba, hakuwa na mpenzi, alichokifanya ni kuanza kununua machangudoa. Alifanikiwa sana, alilala na wengi. Alipofika Dar es Salaam, akaendelea kulala nao ila kwa kila ambaye alimuona sura yake na kumgundua, alimuua, alitaka suala la kununua machangudoa liwe siri maisha yake yote.

Upande wa pili kuna mwanamke mrembo aitwaye Pamela, msichana huyu mwenye umbo matata amefika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya kazi ya uchangudoa. Anapofika huko, kutokana na uzuri wake, anawapata wanaume wengi, anamtetemesha kila mtu, si wanaume tu, hata wanawake wenzake.

SONGA NAYO…

Do not cross’ (usivuke) yalikuwa maneno machache yaliyoandikwa katika viplastiki mfano wa kamba zilizozunguka sehemu hiyo ambayo kulikuwa na kazi maalum ya kufukua sehemu ambayo watu walisema kulikuwa na mwili uliofukiwa.

Polisi walikuwa bize kulifukua shimo hilo, hakukuwa na kazi kubwa kwani ardhi ililowa kwa kiasi kikubwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku. Baada ya dakika kadhaa, wakaufikia mwili huo, wakayaweka makoleo pembeni kisha kuanza kufukua kwa mikono.

“Mungu wangu!”

Kila mmoja alishtuka, mwili wa mwanamke ukatolewa katika shimo lile, baadhi ya wanawake waliokuwa mahali hapo wakashindwa kuvumilia, wakaanza kulia, waliumia mioyo yao, kile kilichokuwa kikionekana, kilikuwa ni ukatili wa hali ya juu.

“Utoeni kabisa, hakikisheni hamgusi sehemu zile zinazotakiwa kufanyiwa uchunguzi,” alisema polisi mmoja ambaye alionekana kuwa kiongozi wa polisi waliokuwa mahali pale.

Mwili wa Magreth ukachukuliwa na kupelekwa pembeni kabisa, watu wengine hasa wanawake wakashindwa kubaki mahali hapo, wakaondoka huku wakiwa wenye nyuso za huzuni.

“Mmewapigia simu?” aliuliza kamanda.

“Akina nani?”

“Watu wa uchunguzi.”

“Ndiyo! Wamesema wanakuja mkuu!”

Zilipita dakika kumi na tano, gari jingine likafika mahali hapo, wanaume wanne waliokuwa na mavazi maalum na glavu mikononi mwao wakateremka na kuanza kupiga hatua kule kulipokuwa na polisi wale wengine ambao walikuwa na mwili wa Magreth pembeni.

Mara baada ya kuzungumza nao kidogo, wakaanza kuuchunguza mwili ule palepale, lengo lao likiwa ni kutaka kubaini alama za vidole, waliporidhika, wakaubeba na kuupandisha ndani ya gari na safari ya kuelekea hospitalini kuanza.

“Hii ni hatari sana…”alisikika polisi mmoja.

*     *     *

‘Mwili wa Mwanamke wakutwa Msituni’, Muuaji aibuka jijini Dar’, Dar Yageuka Machinjioni’, hivyo vilikuwa vichwa mbalimbali vya habari katika magazeti yaliyotoka siku moja baada ya mauaji ya msichana Magreth.

Kila mtu aliyeyaona magazeti yaliyokuwa na vichwa hivyo vya habari hiyo, alishtuka, si kwamba hawakuwa wakijua kama kulikuwa na mauaji ya chinichini yaliyokuwa yakiendelea bali kitendo cha kukutwa msichana mwingine akiwa ameuawa msituni ndicho kilichowashtua zaidi.

Waandishi wa magazeti hayo waliandika habari ndefu ambayo ilionekana dhahiri kwamba muuaji wa mauaji yote hayo alikuwa mtu mmoja. Walianza na taarifa ile ya kwanza kabisa, mauaji ya msichana ambaye aliuawa katika Msitu wa Pande, taarifa zilisema kwamba muuaji huyo alivalia kofia kubwa ili kuuficha uso wake.

Shuhuda pekee wa tukio lile, mzee Gombana ambaye ndiye alimuona muuaji huyo na kusema kwamba alivaa kofia kubwa, mwisho naye alikufa katika kifo kilichojaa utata mkubwa baada ya kutoka katika kituo cha polisi kutoa maelezo.

Ukiachana na mzee huyo, pia alizungumziwa msichana mwingine aliyekuwa akiishi Mwananyamala, msichana huyo ambaye alikuwa akifanya kazi katika gesti bubu moja aliuawa bafuni wakati anaoga huku vijana ambao walimuona muuaji huyo wakisema kwamba alivalia kofia kubwa ambayo iliwapa ugumu kuuona uso wake.

Muuaji alikuwa nani? Kwa nini aliua? Hayo yalikuwa maswali yaliyokuwa vichwani mwa watu wengi, hakukuwa na mtu aliyekuwa na jibu lolote lile. Watu waliendelea kujiuliza juu ya muuaji lakini bado vichwa vyao viliendelea kuwa na giza.

“Ni lazima muuaji apatikane,” alisema polisi wa Kituo cha Mbezi.

“Sawa mkuu! Tutafanya hivyo!”

Ilikuwa ni lazima taarifa hizo zifikishwe makao makuu ya polisi jijini Dar ambapo ndipo muuaji, kamanda Dickson alipokuwa. Ndani ya dakika arobaini, tayari taarifa za mauaji yale zilikuwa mezani kwa kamanda Dickson ambapo baada ya kuzisoma, akapigwa na mshtuko na kujiuliza ni kwa namna gani watu walifahamu kule alipouzika mwili ule usiku kwani aliamini kwamba hakukuwa na mtu aliyemuona.

“Ni nani alimuona muuaji akiingia msituni?” aliuliza kamanda Dickson.

“Taarifa zinasema ni wawindaji.”

“Mmh! Waliweza kumuona wakati anachimba shimo na kuufukia mwili?” aliendelea kuuliza, alitaka kupata jibu.

“Hapana ila walisema waliliona gari likiingia msituni, wao wakakimbia kujificha…”

“Baada ya hapo?”

“Gari lilipoondoka ndipo walipokwenda kuona kulikuwa na nini, wakahisi kwamba kulikuwa na mwili umefukiwa, hivyo wakatoa taarifa,” alisema polisi mmoja.

“Sawa, unaweza kwenda.”

“Asante mkuu,” alisema polisi huyo kisha kupiga saluti kama heshima, akaondoka zake. Kamanda Dickson akabaki ofisini akiwa na presha kubwa.

Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply