The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi 60

0

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam kufuatia kupotea mfululizo kwa machangudoa katika mazingira ya kutatanisha. Taharuki kubwa inazuka kwani ndani ya kipindi kifupi tu, zaidi ya machangudoa kumi na moja wanapotea na hakuna anayejua walikopotelea.

Jambo hilo linasababisha jeshi la polisi kuingilia kati. Kinachozidi kuzua utata, wote wanapotea katika mazingira yanayofanana. Mwanaume mmoja asiyejulikana, aliyekuwa anatembelea gari la kifahari aina ya Volkswagen, aliyekuwa akienda eneo hilo usiku wa manane ndiye anayehusishwa na wote wanaopotea.

Upande wa pili, kijana aliyekuwa na mwonekano tofauti na binadamu wa kawaida, Dickson Maduhu au Zinja kama wenzake walivyokuwa wakimtania, amejiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hisia kali za mapenzi zinasababisha kijana huyo aanze kutoka usiku na kwenda kutafuta machangudoa.  Hivyo baadaye anahamishiwa Dar es Salaam.

Baada ya kuwa DCP, Dickson anakutana na msichana aitwaye Pamela, anatokea kuvutiwa naye, anafanya naye mapenzi kwa kumnunua Kinondoni. Kupitia changudoa huyo aliyetoka Arusha, anajikuta akianza kuwaua wanawake wengi jijini Dar es Salaam.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Idadi kubwa ya watu ilikusanyika nje ya gesti ya Mkombothi iliyokuwa Kinondoni jijini Dar. Minong’ono ilisikika kila kona kwamba ndani ya gesti hiyo kulikuwa na msichana aliyekuwa ameuawa.

Kila mmoja aliyesikia minong’ono hiyo alishindwa kuamini hivyo watu wengi kutaka kwenda ndani kujionea wao wenyewe. Wanaume waliokuwa na nguvu ambao ndiyo walikuwa watu wa kwanza kupewa taarifa hiyo walifanya kazi ya ziada ya kuwazuia watu kuingia ndani.

Waliokuwa na simu zenye kamera, kama kawaida yao walikuwa bize kupiga picha, walitaka kuwa wa kwanza kutoa taarifa katika mitandao ya kijamii. Hakukuwa na mtu aliyekumbuka kuwapigia simu polisi, walichokifikiria kwanza kilikuwa ni mitandao ya kijamii tu.

Umati wa watu ulizidi kuongezeka huku kila mtu akiongea lake, baadhi ya wanawake waliopewa nafasi ya kwenda chumbani, waliporudi walikuwa wakilia huku wakisema kwamba mwanamke aliyeuawa kikatili alikuwa Shamila.

“Shamila!” Haiwezekani! Ni jana tu nilikuwa naye!” alisema kijana mmoja huku akionekana kutokuamini kabisa.

Jina la Shamila likaanza kusikika masikioni mwa watu. Walimfahamu msichana huyo, japokuwa alikuwa maarufu kwa kujiuza lakini alikuwa msichana wa tofauti kabisa. Alikuwa mchangamfu na aliyependa kuzungumza na kila mtu, hakuwa msichana wa majivuno, hata kwa kidogo alichokuwa nacho, alikuwa radhi kumpatia hata na mwingine.

“Ni kweli Shamila au nimemfananisha?” aliuliza jamaa mmoja.

“Ni yeye! Ni Shamila kweli!”

Pamela akafika mahali hapo, alipoambiwa kwamba Shamila alikutwa akiwa ameuawa chumbani kwake, hakuamini. Alitaka kujionea kwani usiku uliopita tu alikuwa naye Kinondoni mpaka alipoamua kuondoka kwa sababu alikosa wateja.

Akaruhusiwa kwenda ndani. Hazikuwa tetesi, kile alichokisikia ndicho alichokutana nacho ndani. Mwili wa Shamila ulikuwa kitandani, mdomoni alikuwa na alama zilizoonesha kwamba kabla ya kuuawa alitokwa sana na mapovu mdomoni.

Pamela akashindwa kuvumilia, hapohapo machozi yakaanza kumtoka, picha aliyoiona kitandani ilimsisimua sana hivyo kujikuta akitoka nje huku akilia kwa sauti.

Lilikuwa pigo kubwa kwa machangudoa wengine. Hazikupita dakika nyingi, polisi wakafika katika gesti hiyo na kuingia ndani, mtu wa kwanza kabisa kumshikilia kama mtuhumiwa namba moja alikuwa dada wa mapokezi.

“Jamani sijui chochote kile,” alisema msichana huyo.

“Sawa! Ila twende kituoni, tunataka uisaidie polisi,” alisema polisi mmoja, dada yule wa mapokezi akafungwa pingu, mwili wa Shamila ukatolewa ndani.

Watu walipouona ukitolewa, hawakuamini, wakabaki wakilia, ni kweli, mtu aliyekuwa ameuawa ndani ya chumba kile alikuwa Shamila, hivyo akaacha vilio vikubwa katika mtaa aliokuwa akiishi.

Muuaji hakujulikana, hata dada yule alipoulizwa juu ya muuaji huyo, alishindwa kumfahamu ila kitu pekee alichokisema ni kwamba mwanaume huyo alivalia kofia kubwa ya Marlboro, hivyo hakuweza kumgundua usoni.

“Alivalia kofia ya Marlboro?” aliuliza polisi kana kwamba hakuwa amesikia.

“Ndiyo!”

“Haukuweza kuuona uso wake?”

“Ndiyo afande.”

Maelezo ya dada yule yakawarudisha nyuma kabisa na kukumbuka kwamba wanawake kadhaa waliouawa kipindi cha nyuma, waliuawa na mtu huyohuyo ambaye kila siku alionekana kuvalia kofia kubwa.

Hawakujua mtu huyo alikuwa nani na kwa nini aliwaua wanawake tu. Polisi walichanganyikiwa, hawakujua pa kuanzia kwani hata nyakati za usiku walipokuwa wakitembea kama kufanya doria, walikutana na watu wengi waliovalia kofia za namna hiyo hivyo kuwa na wakati mgumu wa kumfahamu mhusika.

“Ila huyu muuaji ni nani?” aliuliza polisi mmoja, alionekana kuchoka, walizunguka sehemu kubwa jijini Dar kufanya doria lakini hakukuwa na dalili zozote zile.

“Hata mimi sifahamu! Hapa inabidi tuongeze kasi, la sivyo wanawake wengi hapa Dar watauawa,” alisema polisi mmoja.

Wakati polisi wakiendelea na doria yao, upande wa pili Kamanda Dickson alikuwa na mawazo tele, moyo wake ulianza kuridhika kutokana na kile alichokifanya, aliambiwa kwamba mbali na Hadija kulikuwa na wasichana watatu na mmoja alikuwa amekwishamuua na walibaki wawili kabla ya kumalizia na mhusika mwenyewe ambaye ni Hadija.

Usiku wa siku hiyo, alishinda akinywa pombe nyumbani kwake, kichwa chake bado kilikuwa na mawazo tele, kila kitu kilichokuwa kikiendelea, kilimchanganya sana.

Alijiona kuwa na roho mbaya lakini hakuwa na jinsi, alihitaji kuificha siri yake ili aishi kiamani na hakukuwa na kitu kingine cha kufanya kuificha siri hiyo zaidi ya kuua kama alivyokuwa akifanya.

Mara kwa mara alikuwa akiwasiliana na Pamela, japokuwa msichana huyu alikuwa changudoa lakini moyo wake ulimpenda, alikuwa radhi kwa kila kitu, kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya msichana huyo kwake halikuwa tatizo kutokana na uzuri aliokuwa nao, aliona kustahili kufanyiwa mambo yote ili awe na furaha maisha yake yote.

“Wa pili ni huyu Asha, nikimalizana naye, nahamia kwa Anita kisha kumuua Hadija mwenyewe, bila kufanya hivi, najua itakula kwangu tu,” alisema Kamanda Dickson kisha kujitupa kitandani kwake, akili yake ilichoka mno.

Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply