The House of Favourite Newspapers

Jokate Alipambana na Wazazi Wake Kufikia Ndoto Zake

JULAI 29, 2013 (miaka mitano iliyopita), mwanadada mtangazaji, mjasiriamali, muigizaji, mwanamuziki na mhamasishaji Jokate Urban Mwegelo aliulizwa na mtangazaji wa Kipindi cha Mkasi, Salama Jabir kwamba ni kitu gani kinamtofautisha na wasichana wengeni na hivi ndivyo alivyojibu;

 

“Kinachonitofautisha na wasichana wengine ni kwamba mimi ninapenda kujitegemea. Ninahitaji niwe msaada kwangu mwenyewe, niwasaidie watu wengine na mimi ni mtu wa kupigania ndoto zangu!”

Hivyo ndivyo Jokate, mwanadada wa Kitanzania aliyezaliwa jijini Washington D.C, Marekani miaka 31, iliyopita anaamini kwamba anatofautiana na wanadada wengi ambao ni tegemezi na watu wasiofahamu namna ya kupigania ndoto zao.

 

Hata hivyo, kama alivyosema ni kweli, Jokate amekuwa ni mwanadada wa kujisimamia na kujitegemea. Anamiliki Kampuni iitwayo Kidoti inayohusika na masuala ya mavazi, nywele, mabegi, ndala na bidhaa nyinginezo!

Kutokana na juhudi zake katika shughuli zake binafsi na shughuli mbalimbali za kijamii mwaka jana (2017), Jarida la Forbes Africa, lilimtaja kama mwanadada mwenye ushawishi Afrika kwa wanadada wenye umri ndani ya miaka 30!

 

Kama haitoshi, mwaka huohuo aliorodheshwa kwenye Tuzo ya African Youth, ambayo iliwakutanisha wanadada 100, wenye ushawishi zaidi Afrika wakiwania tuzo moja ya mwanadada anayewahamasisha zaidi vijana wadogo kupigania ndoto zao. Alipewa pia Tuzo ya Mwanamke wa Nguvu na Kampuni ya Clouds Media Group. Bila kusahau kupata madili kutoka kwenye makampuni makubwa ya SportPesa na Juisi ya Shake & Sippy.

ALIANZAJE KUFIKA HAPO?

Swali hili wanaweza kujiuliza watu wengi ambao wanahitaji kupigania ndoto zao na kufika kwenye mafanikio aliyonayo. Kuhusu alifanya jambo gani mpaka kufika mahali hapo alipo, wakati fulani alipotembelea Zanzibar, na kuzungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar alisema hivi;

“Kiukweli haikuwa rahisi. Kwanza nianze kusema kwamba nimezaliwa katika familia ya wazazi walioamini kupitia elimu ambapo shule ya msingi nilisoma katika Shule ya Mtakatifu Antony, sekondari nilisoma Shule ya Loyola na chuo nilisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo nilisoma masomo ya Political Science (Sayansi ya Siasa).

“Hata hivyo pamoja na kuweka juhudi kubwa shuleni nilikuwa na ndoto zangu. Sasa ili kuzitimiza, nilichoamua kufanya, jambo la kwanza ilikuwa ni kujitofautisha na wanafunzi wengi ambao husoma ili kufaulu mtihani. Nikaamua kuitumia nafasi ya elimu kama mkombozi kwenye ndoto zangu.

“Mbali na darasani nikaanza kujichanganya kwenye nafasi mbalimbali za uongozi, kwenye makundi mbalimbali ili kuweza kujiongezea ufahamu zaidi. Na baada ya kumaliza chuo niliweza kuanzisha kampuni yangu ya Kidoti baada ya kuingia kwenye masuala ya urembo!”

NINI ILIKUWA CHANGAMOTO KWAKE?

Kwenye kila mafanikio ni lazima mtu atakuwa anakutana na changamoto. Kwa Jokate, changamoto kubwa walikuwa ni wazazi wake. Amewahi kuweka wazi kwamba baada ya masomo wazazi wake walipenda apate kazi yenye ‘security’ wakiamini ndiyo namna pekee ya kumkomboa kimaisha.

Amewahi kueleza kwenye mahojiano ya redio kwamba; “Binafsi ndoto zangu zilikuwa ni zaidi kuliko ‘option’ yao hiyo. Kwa hiyo ikabidi nipambane kwa nguvu ili kuweza kuwaaminisha kwamba nilichoamini kilikuwa ni bora zaidi kuliko mawazo yao na kuna muda nilikuwa mpaka natofautiana nao. “Lakini Mungu ameweza kunisimamia kampuni yangu ya Kidoti imeweza kufanikiwa kiasi cha kushirikiana kibiashara na makampuni mengi mpaka ya Kichina.”Ni balozi wa mchezo wa mpira wa kikapu

Jokate pia amekuwa akijituma kwenye michezo ambapo amejenga uwanja wa mpira wa kikapu katika Shule ya Sekondari Jangwani na ni balozi wa mchezo huo Tanzania.

 

KUHUSU UIGIZAJI

Mwaka 2007, Jokate alionekana kwenye filamu ya Fake Pastor akiwa na Vincent Kigosi ‘Ray’, Lisa Jensen na wengineo. Ameonekana pia kwenye muvi za From China With Love, Chumo na mwaka 2011 alishinda Tuzo ya ZIFF (Zanzibar International Film Festival). Mwaka uliofuata alishinda tuzo ya NEA (Nigeria Entertainment Award), pia alionekana kwenye ‘sirizi’ ya Siri ya Mtungi bila kusahau muvi ya Mikono Salama aliyoshiriki akiwa kama Ndekwa.

 

MUZIKI

Jokate ni mwanamuziki pia amewahi kutoa ngoma akimshirikisha prodyuza Lucci iitwayo Dada Kaka, ngoma ya Leo Leo aliyomshirikisha mwanamuziki Ice Prince kutoka Nigeria, lakini pia amewahi kushirikishwa kwenye wimbo uitwao Kings and Queens na mwanamuziki Ambwene Allen Yessayah ‘AY’.

Makala: Boniphace Ngumije

Comments are closed.