The House of Favourite Newspapers

Jokate: Uvumilivu Ndio Kila Kitu Maishani

0

JOKATE Urban Mwegelo, Miss Tanzania namba 2 mwaka 2006, ndiye tunaye leo kwenye ukurasa huu wa Ulipo Mwanamke Tupo.

Yeye anaamini uvumilivu katika safari ya kutafuta mafanikio maishani ndio kila kitu.

UMT: Unatoka kwenye familia yenye ubora kimaisha, huoni kama ni sababu ya wewe kuwa na unafuu kimafanikio?

Jokate: Ni wangapi wametoka kwenye familia bora lakini maisha yao ni ya hovyo? Mafanikio ni namna ambavyo unaiweka akili yako katika kupanga na kufanikisha mambo.

UMT: Umewahi kuumizwa na maisha kwa kiwango cha kupitiliza na kumkufuru Mungu?

Jokate: Maumivu hayakwepeki maishani ndugu yangu. Ukisikia mtu anakwambia hajawahi kuumia maishani ni lazima akapimwe akili upya.

My point on this is (ninachomaanisha hapa ni kwamba) maishani kuna milima, kero na kila aina ya adha, machozi ni lazima, leo hili na kesho lile.

UMT: Japo kona hii inahusu maisha na mafanikio, lakini si vibaya kugusia hata mapenzi kwa kuwa ni sehemu ya maisha na ukizingatia

wewe ni kijana, umewahi kuumizwa mara ngapi?

Jokate: (akiguna na kukaa kimya kidogo) unajua (akilitaja jina la mwandishi) kwa sasa mimi ni public figure (mtumishi wa umma) na siyo celebrity (maarufu wa kawaida) tena, kwa hiyo kuna vitu sipaswi kuvizungumzia kwenye jamii ili kulinda momentum (hadhi) yangu, japo hilo swali lako ni kwamba maumivu yapo na kabla hujapata mwenza au ndoa bora ni lazima ujichanganye kama nilivyokosea kwa kuamini watu huko nyuma na mwisho wa siku nikaambulia maumivu, achana na hayo mambo bwana.

UMT: Kwa sasa uko kwenye masuala ya siasa, vipi kuhusu kampuni yako ya Kidoti na shughuli za urembo?

Jokate: Katika kupambana na maisha unatakiwa kuwa na nyanja nyingi sana za kusaka pesa japo huku kwenye siasa nimefuata uongozi na siyo pesa, kwa hiyo ni kutenga na kupangilia vyema muda wako, Kidoti ni nembo na siyo Jokate tu kwa hiyo kuna watu wanaendeleza na mimi nikiwa mkuu wao, napambana kila mahali.

UMT: Ni nini ushauri wako kwa wanawake wanaopambana na maisha licha ya kukutana na changamoto nyingi?

 

Jokate: Nothing good comes easily (hakuna kilicho chema ambacho hupatikana kwa urahisi) ni lazima uwe tayari kulipa gharama. Unataka kuwa mwalimu? Lipa gharama za kusoma sana ili uwe na nondo za kutosha kichwani na ufaulu utimize ndoto yako.

Uwe tayari kukesha usiku ukisoma, unataka kuwa askari? Lipa gharama za kwenda mafunzoni na ukavumilie shuruba zote.

Watu wengi hususan wanawake wanapenda sana kupata mambo mazuri maishani lakini hawako tayari kulipa gharama.

Siku zote mimi huwa nawaambia watu kwamba gharama pekee ya mafanikio ni jasho, maumivu na wakati mwingine kujitoa rehani, kukubali kujitesa leo ili utimize ndoto zako.

Ushauri wangu kwao ni kwamba wawe na malengo, wapange mikakati kabambe ambayo wanaamini itawafikisha waendako na baada ya hapo sasa waingie kazini kupambania ndoto hizo bila kuangalia nani atasema nini na kwa maneno gani mabaya, wakifanya hivyo na kumwamini Mungu huku wakiwa na nidhamu ya fedha, muda na watu, lazima mafanikio yapatikane.

UMT: Ni nini huwa unafanya unapokumbana na changamoto maishani?

Jokate: Unajua iko hivi, matatizo na changamoto ni kuni za kuchochea moto wa mafanikio.

Kama kuna binadamu hajapitia matatizo hana sifa ya kuishi. Ni lazima uumie kwanza ndipo dunia ikupe kitu kizuri unachokihitaji.

Kwa hiyo mwanamke lazima uwe na ndoto. Uipende na ujiwekee mikakati ya namna gani utaitimiza ndoto yako. Kumuomba Mungu na kufanya yaliyo mema kwa watu.

Kusaidia wasiojiweza na kuwa na moyo wa kusamehe na upendo kwa watu wote.

 

Hakuna sababu ya kuwekeana chuki na visasi. Mtu akikukosea, mwambie ukweli kuliko kuanza kumteta pembeni na kubaki na fundo limekuelemea moyoni, ya nini yote hayo?

Mwambie lakini pia uwe tayari kusamehe haijalishi kama amekuomba msamaha au la, wewe samehe na mengine yote muachie Mungu atatimiza kwa wakati.

Mwisho kabisa nataka niwaambie wanawake wenzangu kwamba, Mungu ametujaalia nguvu na uwezo mkubwa mno.

Tukitumia vyema nguvu tuliyonayo, hakuna kitu kigumu maishani. Mwanamke fanya kazi kwa nguvu, jitume na ujitolee kwa hali na mali kufanikisha ndoto zako.

Mungu amekujaalia uwezo mkubwa wa kufikiri na kufanya mambo, tumia kila kitu ulicho nacho ili upate kila kitu unachokihitaji, hapa namaanisha ufanye kazi zilizo halali, nguvu ya mwanamke ni kubwa mno.

UMT: Sasa hivi tunakuona umejikita zaidi kwenye masuala ya kisiasa, vipi unaachana moja kwa moja na mambo ya burudani?

Jokate: Hapana, siasa ni utumishi na burudani ni kipaji nitafanya vyote lakini muda wangu mwingi nitautumia katika kukitumikia chama, nakipenda sana chama changu (CCM) na sisi kama vijana tunahitajika zaidi kuendeleza pale wazee wetu walipoishia.

UMT: Jokate nakushukuru sana kwa ushirikiano wako, siku nyingine nitakutafuta tena uwape somo wanawake wenzako.

Jokate: Karibu tena.

Makala: Brighton Masalu |  Ulipo Tupo Mwanamke | Gazeti La Amani.

Matukio kama haya na mengine, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers

Android ===>Google Play

iOS ===>Apple Store

VIDEO: DK SHIKA KUWEKA HISTORIA USIKU WA 900 ITAPENDEZA

Leave A Reply