The House of Favourite Newspapers

Joto la Mapenzi

0

ILIPOISHIA:

Alimuuliza Mabina kwa ishara wamuamshe Koleta au? Chris alimkataza na kusogea kitandani na kumkuta mzee Mtoe akiwa katika usingizi mzito.“Tummalizeje?” Mabina alimuuliza kwa sauti ya kunong’ona.

SASA ENDELEA…

“Wewe fanya ujuavyo ili tuwahi kuondoka.”

“Huyu hatutumii nguvu nyingi, tutatumia mto tu kumbana pumzi.”

“Poa.”

Bila kupoteza muda Mabina alichukua mto aliokuwa ameegemea mzee Mtoe na kumziba nao usoni kwa nguvu wakati huo Ambe alimshikilia sehemu za miguu ili asikukuruke na kuweza kumuamsha Koleta aliyekuwa kwenye usingizi mzito huku akibembelezwa na muziki mtamu kutoka katika Ipad. Baada ya kumziba pumzi kwa muda mrefu alimuachia alipomuona ametulia kuonesha amefariki.

Walimuacha na kutoka kwa haraka wakimuacha Koleta akiwa amelala fofofo. Walitoka hadi nje ya chumba na kurudishia mlango kama walivyoukuta kisha walitokomea zao nje.Kama kawaida walipanda pikipiki yao na kurudi kijijini kwao wakisubiri taarifa ya kifo cha mzee Mtoe.

***

Majira ya saa tisa usiku muuguzi aliingia chumba alicholazwa mzee Mtoe ili ampatie huduma ya sindano aliyotakiwa kuchomwa saa tisa usiku. Alipofika alimshtua Koleta ambaye alilala kama yupo nyumbani.

“Dada vipi naona unauchapa usingizi?”

“Wee acha, kumuuguza mgonjwa kazi hasa watu wenye vichwa vya panzi kama sisi.”

“Basi nimekuja kumchoma sindano mzee huu ndiyo muda wake.”

“Hakuna tatizo dada yangu,” Koleta alijibu huku akijitengeneza vizuri kwenye kiti na kuyapikicha macho.Muuguzi alisogea hadi kwenye kitanda na kuweka tlei ya vifaa vya matibabu kwenye meza iliyokuwa pembeni ya kitanda. Kisha aliushika mkono wa mzee Mtoe ili amchome sindano ya kwenye mshipa.

Alipoushika mkono wa mzee Mtoe ulikuwa umelegea kitu kilichomshtua. Kingine kilichomshtua alivyokuwa amelala macho yake yalikuwa yanaangalia juu yakiwa yametulia.Alipompima aligundua mabadiliko katika mwili wake, kabla ya kuthibitisha alichokiona alitoka haraka kumfuata daktari wa zamu.Alimkuta amelala kwenye kiti chake alimtikisa kumuamsha huku akimwita.“Dokta kuna tatizo.”

“Tatizo! Tatizo gani?”

“Hali ya mzee Mtoe siyo nzuri.”

“Una maana gani?”

“Kuna hali imenitatiza naomba twende ukamuone.”

“Haya tangulia.”

Wakati daktari akichukua vitendea kazi muuguzi alirudi hadi chumbani na kumkuta Koleta akiwa amepitiwa tena na usingizi. Hakutaka kumuamsha mpaka daktari alipofika.

“Vipi?” aliuliza huku akisogea kitandani, hali aliyoiona ilimshtua sana. Kwa haraka alianza kumpima mzee Mtoe mapigo ya moyo, bado hakukubaliana na vipimo vile aliamua kumpima vipimo vya kiasili navyo vilikuwa na jibu lilelile kuwa mzee Mtoe mzunguko wa damu ulikuwa umesimama pia mwili ulikuwa umeanza kupoa kuonesha hakufa muda mrefu.

“Hamna kitu,” daktari alimwambia muuguzi huku akifuta jasho kwa koti. “Amekufa!”

“Ndiyo.”

“Sasa itakuwaje kuhusu huyu msichana, tumwambie?”

“Hatuna budi lazima tumwambie.”

“Mmh! Sijui itakuwaje?”

“Imeisha kuwa, hatuna jinsi hii ni mipango ya Mungu ambayo wanadamu hatuna uwezo nayo.”Ilibidi wamuamshe Koleta aliyekuwa na usingizi mzito, hali ya kitandani ilimshtua lakini alitulia asikie walicho muamshia.

“Samahani dada.”

“Bila samahani,” Koleta alijibu huku akijiweka vizuri kwenye kiti.

“Kuna nani zaidi yako?”

“Zaidi yangu kivipi?”

“ Huyu si baba yako?”

“Ndiyo.”

“Kwenu zaidi ya mama yako yupo nani?”

“Nipo mimi.”

“Basi hatuna budi kukueleza kinachoendelea kuhusu baba yako.”

“Baba yangu amefanya nini?” Koleta aliuliza huku akinyanyuka na kutupia jicho juu ya kitanda na kushtushwa na shuka iliyokuwa imemfunika mwili mzima.

“Mmh! Baba kafanya nini?” Koleta aliuliza huku akifunua mwili wa baba yake ambao aliukuta haupo katika hali ya kawaida.

“Dokta baba kafanya nini?” Koleta alimshika baba yake ambaye hakuonesha kuwa na uhai.

“Nesi aliyekuja kumchoma sindani ya usiku huu alipokuja alikuta mabadiliko katika mwili wa baba yako na kuja kunipa taarifa baada ya kufika hapa na kuupima hali ya baba yako tumegundua amefakiri.”

“Atiii! Sikubali,” Koleta alipiga kelele huku akiukumbatia mwili wa baba yake.

“Dada wewe ndiye tunakutegemea kama utakuwa hivi mama yako atakufa kabisa na kujikuta unapoteza wazazi wako wawili kwa mpigo.”Kauli ile ilimfanya Koleta anyamaze hasa baada ya kujua presha ya mama yake kwenye matatizo mazito hasa kama msiba tena wa mumewe.“Sasa dokta tutafanyaje?” aliuliza akijikaza kiume.

“Ni kuwataarifu ndugu na jamaa ili mpange jinsi ya kuuhifadhi mwili wa mzee wako.”

“Sijui mama atapokeaje habari hizi?”

“Unatakiwa kumweleza kwa umakini mkubwa.”

“Siwezi lazima atajua kabla sijamwambia.”

“Basi hakuna jinsi lazima aambiwe ili ajue nini kinaendelea.”Kwa vile muda ulikuwa umekwenda na alfajiri ilikuwa ndiyo inaingia. Koleta aliamua kurudi nyumbani ili kujipanga kwa ajili ya msiba wa baba yake. Akiwa njiani alijawa na mawazo mengi kuhusiana na kifo cha baba yake na kujiuliza kimetokana na nini.

Wasiwasi wake ulikuwa kwa Ambe kufanya mauaji yale japo hakuwa na uhakika. Alijiuliza kama yeye aliingiaje pale na kufanya mauaji yale kwa utaalam mkubwa ambapo alifanya tukio hilo bila yeye kusikia. Pamoja na kuwaza yale aliogopa kumhusisha  moja kwa moja mzazi mwenzake kwa vile hakuwa na uhakika na alichokiwaza.

Alipofika nyumbani alikwenda moja kwa moja ndani na kumgongea mama yake mlango. Baada ya kuamka alishtuka kumuona alfajiri ile.

“Koleta mwanangu mbona muda huu mgonjwa umemuacha na nani?”

“Mama…ma…”

“Koleta nini?” mama yake alishtuka kumuona mwanaye akishikwa na kigugumizi.

“Ba…ba…b…ba,” alishindwa kumalizia.

“Koleta…nini mwanangu baba kafanya nini?”

“Mama…babaaa.”

“Kafanya nini?” mama aliuliza kwa sauti kali.

“Ame…me…me…ku…”“Jesus Christ!” mama Koleta alianguka mzimamzima lakini Koleta alimuwahi mama yake ambaye alikuwa amepoteza fahamu. Walimchukua na kumuwahisha hospitali kwani hali yake ilikuwa mbaya sana. Koleta pamoja na kuwa na machungu ya kifo cha baba yake, alikumbuka maneno ya daktari kuwa anatakiwa kusimama kidete ili kuokoa maisha ya mama yake ambayo yanaweza kupotea wakati wowote kutokana na kifo cha baba yake.

Ilibidi asimame kidete kuhakikisha yeye ndiye atakayesimamia kila kitu. Baada ya mama yake kupata nafuu alitolewa hospitali na kufanyika taratibu zote na baba yake alizikwa.

 Je, kilifuatia nini? Usikose Jumamosi ijayo.

Leave A Reply