The House of Favourite Newspapers

JPM na Museveni Kuweka Jiwe la Msingi Ujenzi Bomba la Mafuta

0
Rais Magufuli na Rais Museveni.

 

Tarehe 05 Agosti, 2017 siku ya Jumamosi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wataweka jiwe la msingi la Mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.

 

Mradi huu ni moja ya miradi mikubwa ambayo nchi yetu imeipata na kuanza kutekeleza tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani tarehe 05 Novemba, 2015. Ni mradi ambao uwekezaji wake ni mkubwa wa Dola za Marekani Bilioni 3.5 sawa na takribani Shilingi Trilioni 8 za kitanzania.

 

Urefu wa bomba hili ni kilometa 1,445 na kati ya hizo kilometa 1,115 zinajengwa Tanzania na mafuta ghafi yatakayosafirishwa ni mapipa 216,000 kwa siku.

 

Inatarajiwa wakati wa ujenzi wa mradi huu ajira takribani 10,000 zitazalishwa na Watanzania watakuwa wanufaika wakubwa wa ajira hizi. Nchi zetu za Tanzania na Uganda zitapata manufaa makubwa ya kiuchumi kutokana na kodi na tozo mbalimbali, mrahaba na shughuli nyingine za kibiashara zitakazoambatana na mradi huu.

 

Nachukua fursa hii, kuwaalika Watanzania wote kufuatilia matangazo ya moja kwa moja yatakayorushwa na vituo vya redio, televisheni na mitandao ya kijamii kwa siku hiyo ya Sherehe za uwekaji jiwe la msingi na pia kufuatilia matangazo mbalimbali na machapisho yatayotolewa na vyombo vyetu vya habari na mitandao ya kijamii kuelekea siku hiyo.

 

Kama ambavyo viongozi wa Mkoa wa Tanga wanafanya, tunataraji wananchi wa Tanga watajitokeza kwa wingi kuungana na Rais wao Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika sherehe hii kubwa na kwa mradi huu mkubwa katika nchi zetu.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

28 Julai, 2017

Leave A Reply