The House of Favourite Newspapers

JUKATA Wakomaa na Rais Magufuli Kuhusu Maandamano ya Katiba

0

JUKWAA la Katiba (Jukata) limemuomba Rais John Magufuli apokee maandamano ya amani kushinikiza kufufua mchakato wa Katiba mpya.

Jukata limefikia maamuzi ya kufanya  maandamano hayo ya amani nchi nzima kutokana na makubaliano ya mkutano mkuu wa dharura wa jukwaa hilo uliofanyika Septemba 29 mjini Dodoma ambao pamoja na mambo mengine ulikubaliana kuyafanyia kazi maoni ya wananchi ambayo yamekuwa yakisisitiza kuwapo kwa mchakato wa Katiba mpya.

Hata hivyo hivi karibuni Kurugenzi wa Mawasiliano ya Rais ilizitaarifu taasisi za umma na zisizo za umma zinazomualika Rais Magufuli kutotangaza ushiriki wake hadi zipate uthibitisho kutoka Ofisi ya Rais.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumamosi, Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda alisema maandamano hayo ya amani yatafanyika nchi nzima Oktoba 30.

Amesema tayari wamemuandikia  barua Rais Magufuli  ya kutaka ayapokee maandamano hayo ya amani wakiwa na ujumbe mahususi kwake.

Amefafanua sababu ya kumuomba Rais apokee maandamano hayo ni kumkumbusha kuwa mambo yote mazuri anayoyafanya ikiwamo kupiga vita rushwa, kusimamia matumizi mabaya ya mali za umma, yanaweza yasilete tija na maendeleo endelevu na ya muda mrefu kwa sababu mengi yanakosa msingi wa kikatiba.

“Akumbuke kuwa yeye siyo Rais wa kudumu, kama asipojenga mifumo imara anayefuata anaweza kuyafuta kirahisi masuala yote mazuri na kuirudisha nchi kwenye hali mbaya kama ambavyo amekuwa akidai.”

“Katiba ndiyo suluhisho la kulinda mazuri yote anayoyafanya na kujenga mifumo thabiti isiyoruhusu nchi kuchezewa na watu wachache kwa manufaa yao,” amesema.

Amesema kuna umuhimu wa kuyaweka masuala yote yanayofanyika sasa  katika Katiba kutokana na ukweli kwamba Katiba ndiyo sheria mama na dira ya nchi.

“Imethibitika bila shaka,  nchi zenye Katiba bora ustawi wa Taifa huwa wa hali ya juu kuliko nchi zilizokuwa na migogoro kutokana na kukosa Katiba zenye misingi ya uongozi,” amesema Mwakagenda.

Mwakagenda alifafanua kuwa  maandamano hayo katika ngazi ya kitaifa yatafanyika jijini Dar es Salaam na yataanzia kwenye ofisi za Jukata na kumalizikia viwanja vya Mnazi Mmoja.

Amesema kwa upande wa mikoani nje ya Dar es Salaam kila wilaya ya Tanzania wameshapeleka taarifa kwa wakuu wa Polisi wa Wilaya kuwafahamisha kuhusu njia yatakapopita maandamano hayo ya amani.

“Lengo la taarifa hiyo mikoani ni kuwaomba wakuu wa wilaya ambao ni wawakilishi wa Rais kwenye wilaya husika kuyapokea,” amesema Mwakagenda.

Mwakagenda alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kushiriki kwenye maandamano hayo ya amani.

Amesema maandamano ni njia mojawapo ya wananchi kuwasiliana na viongozi wao ambao wamepewa dhamana ya kuongoza Taifa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Ameeleza Jukata wana imani watapata ushirikiano wa kutosha kutoka Jeshi la Polisi nchini ili maandamano hayo yafanyike katika hali ya amani na utulivu.

Amesema ana imani wananchi pia watapokea kwa mtizamo chanya kusudio la kufanya maandamano hayo yenye lengo la kurudisha hamasa ya wananchi kushiriki kwenye michakato ya kidemokrasia.

“Hamasa imepungua, iwapo wananchi watapoteza hamasa hiyo kabisa, ipo hatari huko mbele michakato mingine kama uchaguzi kukosa ushiriki  kutokana na wananchi wengi kutoona umuhimu wa kushiriki mambo muhimu ya nchi yao,”amesema.

Amesema Tanzania itakuwa nchi ya viwanda ikiwa kipaumbele kitakuwa Katiba mpya yenye mifumo imara ili kusafiri katika njia sahihi wananchi waitakayo.

“Bila Katiba mpya na bora ni sawa na kujenga nyumba nzuri juu ya mchanga ambayo inaweza kuangushwa hata na upepo, ” amesema Mwakagenda.

Leave A Reply