The House of Favourite Newspapers

Kala: Ashangaa Ndoa Yake Kideoni Kushtua Wengi

0

KALA Jeremiah ni zao la Shindano la Kuibua Vipaji la Bongo Star Search mwaka 2007 ambalo huandaliwa na Kampuni ya Benchmark Production chini ya C.E.O wake, Ritha Paulsen ‘Madam Rita’.

 

Kala ni miongoni mwa mastaa wachache Bongo wanaoshiriki kwenye masuala ya kijamii, hasa kwa kutumia aina ya muziki wake anaoufanya.Pia ni mtu ambaye anajishughulisha na masuala ya kijamii katika harakati za kutafuta haki na usawa kupitia kampeni mbalimbali.

 

Miongoni mwa kampeni hizo ni Kijana Smart ambayo lengo lake ni kumfanya kijana kuwa makini na kushiriki kwenye mambo ya kijamii ndiyo maana akajitolea kuifanya ili kubadili changamoto za kijamii kuwa fursa.Tujuavyo; Kala bado hajaoa ila ana mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka mitano.

Wiki iliyopita kuliibuka sintofahamu baada ya kusambaa kwa picha zake zikimuonesha kuwa amefunga ndoa.

 

Lakini kupitia OVER ZE WEEKEND, Kala anafunguka baada ya ndoa yake anayodai ni ya kideoni kushtua wadau wengi.

 

Habari ya mjini kwa sasa ni ngoma mpya ya Kala aliyomshirikisha Sholo Mwamba inayokwenda kwa jina la Wewe ambayo ndani yake anawapa somo akina dada wanaotarajia kuingia na waliopo kwenye ndoa.Katika mahojiano maalum (exclusive interview) na OVER ZE WEEKEND, Kala anabonga kwamba amefikiria hatua ya kutunga mashairi hayo baada ya kusikitishwa na janga la kuvunjika kwa ndoa nyingi kila kukicha.

 

Kala anasema katika mambo yanayomuumiza roho ni kusikia wanandoa au wachumba wameachana, hali iliyomsababisha kufikiria kisha kutunga mashairi ya ngoma hiyo ambayo anaamini kwa atakayeyasikiliza mashairi yake na kuyafanyika kazi, atakuwa ameinusuru ndoa yake. Kala anasema; “Katika maisha yangu, ukweli ninaposikia wanandoa wameachana na pengine hata wakiwa wachumba, inaniuma sana kama mimi ndiye mhusika, huwa sipendi kabisa itokee hivyo.

 

“Hivyo baada ya kufikiria hilo, nimeona nitoe ngoma hii ambayo naamini kama atakayesikiliza vizuri ujumbe wake, atakuwa ameinusuru ndoa au uchumba wake.“Unajua watu wawili wakishaishi kama mke na mume au wachumba kisha wanaachana, kunakuwa na madhara mengi sana ndiyo maana nikaamua kuwaasa wapendanao wasiachane.”

Kwenye ngoma hii, Kala amemshirikisha mkali wa Singeli, Sholo Mwamba ambaye naye ameitendea haki kwa kuchagiza kwa ladha ya michano yake ya Singeli na kufanya bonge la kitu.

 

Katika ngoma hii, Kala anaonekana ndani ya suti kali huku akiwa na mtoto mzuri wa kiwango cha lami aliyepigilia shela la maana na kuonekana kama walikuwa wakisherehekea harusi baada ya kufunga ndoa, hali iliyowashtua wengi na kuanza kuvumisha kuwa huwenda jamaa huyo alikuwa amevuta kweli jiko na kuamua kuwaonesha mashabiki kifaa chake.

 

Baada ya kuvuja mitandaoni kwa picha za mnato na kichupa cha ngoma hiyo, kama kawaida gumzo lilianza kuenea kwa kasi ya moto wa kifuu, wengine wakisema hiyo ilikuwa ndoa ya kweli huku wengine wakisema hana ubavu huo na huyo aliuza naye tu kideoni.

 

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wapo walioanza kumlaumu Kala kwa kitendo cha kuwa-nyima mnuso huo huku wakiongea mengi ya lawama.

 

Kufuatia hali hiyo, OVER ZE WEEKEND pia imembana Kala juu ya ishu hiyo ambapo ameweka wazi kuwa mrembo huyo aliyemtaja kwa jina la Careen Simba ni rafiki yake mkubwa waliyeshibana muda mrefu na wala si mpenzi wake na hakukuwa na ndoa ya kweli bali ni ujio wa ngoma hiyo.

 

“Kweli najua watu wameongea mengi sana, hata mimi wapo walionipigia simu na kuniuliza baada ya kuona picha hizo, lakini niliwapa ukweli.

 

Yule dada ni rafiki yangu wa karibu kwa muda mrefu sana na tunashirikiana katika mambo mbalimbali yakiwemo masuala ya muziki.

 

“Kutokana na ukaribu wetu ilipotoka audio ya hii ngoma nilimsikilizisha ambapo aliipenda sana na kunipa wazo kufanya ile video na kupangilia mavazi ikiwemo yeye kuvaa shela na mimi kupigilia ile suti ili kutengeneza uhalisia wa ngoma yenyewe.“Namshukuru Mwenyezi Mungu, mawazo yake na yangu yaliendana na kufanikiwa kufanya kitu kizuri ama kile ulivyokiona,” anasema Kala.

 

Kutokana na ubora wa kichupa hicho, baadhi ya wadau wamekuwa wakijiuliza kama kimechukuliwa mamtoni au Bongo, lakini Kala mwenyewe anasema kimechukuliwa hapahapa Bongo, tena pande za Kurasini jijini Dar.

 

Kala anasema maandalizi ya ngoma hiyo kuanzia audio mpaka kichupa chenyewe, kila kitu kimefanyika hapahapa Bongo na kuongeza kuwa hakuona umuhimu wowote wa kwenda kufanyia hayo nje ya nchi wakati Bongo kuna watu wenye uwezo mkubwa wa kufanya hayo na mandhari inaruhusu.

 

Akizungumzia wasanii wanaopenda kufanyia kazi zao nje ya nchi, Kala anasema wapo wanaofanya kazi nzuri na wapo wengine ambao kazi zao zinazidiwa na zile zinazofanyika hapahapa Bongo. “Wengine wanafanya hayo kwa ajili ya ulimbukeni tu, wanakwenda kufanyia kazi zao nje ya nchi, halafu ukiziangalia kazi zenyewe, nyingine zinazidiwa na zinazofanyika hapahapa Bongo,” anamalizia kusema Kala.

Makala: RICHARD BUKOS

Leave A Reply