The House of Favourite Newspapers

POLISI TANGA YAELEZEA KUCHOMWA MOTO BASI LA SIMBA COACH

Linalodaiwa kuwa basi la Simba Coach likiteketea kwa moto sehemu ambayo haijajulikana vizuri leo.

JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limetoa ufafanuzi kuhusu tukio la kuchomwa moto kwa basi la Simba Coach.

Taarifa zinaeleza basi hilo limechomwa leo na wananchi wenye  hasira  baada ya dereva wake kumgonga dereva wa bodaboda.

Kamanda wa  Polisi Mkoa wa  Tanga, Edward Bukombe, amefafanua kwamba ni kweli amesikia taarifa za kuchomwa  moto basi hilo lakini halijachomewa mkoani Tanga kama inavyoelezwa na  baadhi ya watu.

Picha ya karibu ikionyesha moto ulivyolizingira basi hilo.

Amesema baada ya kuona taarifa za kuchomwa basi  hilo waliamua kufuatilia lakini wamejiridhisha kwamba  hilo halikutokea  kwenye mkoa wao bali nchini Kenya.

Amesema basi hilo lilikuwa linatoka Mombasa,  Kenya,  na taarifa walizonazo ni kwamba lilichomwa hukohuko Kenya  kwani lilikuwa halijaingia kwenye mipaka ya Tanzania na hasa mkoani Tanga.

Alipoulizwa iwapo anafahamu namba za basi  hilo na dereva aliyekuwa analiendesha, alijibu wanaendelea kufuatilia kwa polisi wa nchini Kenya na watatatoa  taarifa kuufahamisha umma.

“Tunaendelea kukusanya taarifa na kwa kuwa limechomwa huko Kenya tunawasiliana na polisi wa huko ili tuwe na  uhakika wa taarifa kamili za tukio hilo.  Hatujapata namba za  basi.  Wananchi wasubiri tutaeleza kwa usahihi tutakapokamilisha kupata  ukweli zinazohusu tukio hilo, ” amesema Bukombe.

Mapema asubuhi  leo katika mitandao ya kijamii zilianza kuzagaa picha  zinazonyesha basi linaungua moto, na ikaelezwa  lilichomwa na wananchi wenye hasira mkoani  Tanga lakini haikuonyesha ni sehemu gani hasa.

Ilidaiwa basi lilichomwa kwa vile dereva wake  alimgonga dereva wa pikipiki na hivyo wananchi wakaonyesha hasira zao kwa  kulichoma moto.

Chanzo: Michuzi

Kilichomkuta Huyu Msanii Baada ya Kuposti Picha za Utupu!!

Comments are closed.