Kambi ya Yanga Balaa

UPO uwezekano mkubwa wa Kocha Mkuu wa Yanga, Mrundi, Cedric Kaze, kupangua kikosi chake cha kwanza kitakachoivaa Namungo FC, keshokutwa Jumapili kwa kumuingiza kiungo mshambuliaji Carlos Fernandez ‘Carlinhos’.

 

Hiyo ni baada ya kiungo huyo kurejea kikosini akitokea kwenye maumivu ya kisigino aliyoyapata wakati timu hiyo ikiwa kwenye maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania. Yanga inatarajiwa kuikaribisha Namungo FC katika mchezo wa ligi utakaopigwa saa moja kamili usiku kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, kutoka kwenye kambi ya timu hiyo iliyoweka Kijiji cha Avic Town, Kigamboni nje kidogo ya Dar, kocha huyo katika mazoezi yake ameonekana kumuandaa kiungo huyo mwenye uwezo wa kupiga faulo na kona za kuzaa matunda.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kocha amepanga kumtumia kiungo huyo kwa ajili ya kuangalia uwezo ambaye tangu Kaze ameanza kibarua cha kukinoa kikosi hicho hakupata nafasi ya kumuona kwenye mechi za ligi kutokana na majeraha.

 

Aliongeza kuwa kiungo huyo huenda akatumika kucheza namba kumi nyuma ya mshambuliaji mmoja ambaye ni Mghana Michael Sarpong mwenye uhakika wa kuanza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo iliyopo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 24 juu ya Azam FC wenye 25.

 

“Upo uwezekano mkubwa wa Kaze kupangua kikosi chake cha kwanza katika kikosi kitakachocheza dhidi ya Namungo na Carlinhos ndiye mchezaji anayetarajiwa kuingia kikosini.

 

“Hiyo ni baada ya kiungo huyo kupona na kurejea uwanjani kwa ajili ya kuipambania timu yake ya Yanga, kiungo huyo hakucheza mchezo wowote wa ligi tangu kocha huyo akabidhiwe majukumu ya kuifundisha Yanga.

 

“Kocha amepanga kumtumia kucheza namba kumi nyuma yake akiwa na viungo Fei Toto na Tonombe watakaokuwa wanapeleka mashambulizi lango la Namungo katika kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo huo,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Kaze kuzungumzia hilo alisema: “Ninafurahia kumuona Carlinhos akirejea uwanjani kwa ajili ya kuipambania timu yake kwani ni kati ya wachezaji walio bora katika kikosi changu.

 

“Carlinhos ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kukokota mpira, kupiga pasi fupi na ndefu akiwa na mpira, hivyo ninafurahia kuwa na mchezaji wa aina hii katika timu, hivyo ninatarajiwa kumtumia katika mchezo huu na mingine inayofuatia.”

Wilbert Molandi, Dar es SalaamTecno


Toa comment