Kamwamba: Chichi Mawe Hamalizi Raundi 10
ISRAEL Kamwamba raia wa Malawi ni mpinzani wa Francis Miyeusho ‘Chichi Mawe’ ambaye anarekodi ya kucheza mapambano nane na yote ameshinda, matano yakiwa kwa KO, rekodi zinaonyesha ni moto wa kuotea mbali kufuatia kukaa juu ya ringi kwa raundi 34.
Mabondia wengine watakaopanda ulingoni Julai 22, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Dar Live ni Nasibu Ramadhan ‘Pacman’ atakayezichapa na Benard Mwango wa Zambia wakati Idd Pialali atapanda ulingoni dhidi ya Regin Championi kutoka DR Congo.
Utamu wa mapambano hayo ambayo yatarushwa mubashara na kituo cha Global TV Online hasa kwa upande wa Kamwamba na Chichi Mawe unatokana na utofauti wa staili ya miguu wanaoyotumia mabondia hao, Chichi Mawe ni southpaw yaani anatanguliza mguu wa kulia mbele.
Wakati Kamwamba ‘Israiel Mweusi’ ni orthodox yaani anatanguliza mguu wa kushoto mbele, hivyo hapo ushindani wa kimataifa utaonekana kabisa kwa kuwa kila mmoja anahitaji kuchukua ubingwa huo wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati.
Katika mapambano hayo ya kimataifa, yaliyoandaliwa na Kampuni ya Solid Rock Tanzania, yatasimamiwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO) chini ya rais wake, Yassin Abdallah ‘Ustaadh’.
Kamwamba katika masumbwi hayo yatakayorushwa mushabara na Global TV Online kupitia tovuti yake ya www.globaltvtz.com amefanya mahojiano maalum na Championi Ijumaa na kueleza maandalizi yake kuelekea pambano hilo.
“Na jiandaa vizuri, nataka kazi yangu iwe ya heshima hasa ni kuhakikisha napata ushindi wa aina yake.
“Natambua kuwa nakuja Tanzania kwa ajili ya pambano langu dhidi ya Francis Miyeyusho ni pambano langu la kwanza kubwa la ubingwa ndani ya Tanzania.
“Nalipa nafasi ya umuhimu na ukubwa wake ili niweze kuonyesha kipaji na ubora wangu lakini vilevile litaniweka katika rama ni ya dunia.
“Siyo kitu kidogo kwangu kutimiza hilo licha kuwa ya meneja wangu hufanya kazi mara kibao na mabondia wa Tanzania kama Francis na Cosmas Cheka na Jay Msangi, kwangu ni kitu cha heshima.
“Naamini pambano litakuwa zuri kutokana na maandalizi ambayo naendelea kuyafanya chini ya uongozi wangu, nina rekodi nzuri japo mpinzani wangu kidogo amenizidi ila siwezi kumuhofia.
“Ngumi ndiyo zinanileta Tanzania sasa siwezi kuzembea hasa kutokana na ukubwa wa rekodi yake, kwangu vita popote haijalishi nipo wapi hivyo nitakuja kwa ajili ya kupigana na siyo kucheza Chess.
“Kiukweli niwashukuru waandaaji Global TV Oline kwa hatua hii kubwa ambayo wameamua kuifanya kwa sababu mabondia wapo wengi ila nimechaguliwa mimi, ni kitu cha kujivunia.
“Kutokana na maandalizi ambayo naendelea kuyafanya ni makali kwa kuwa mmoja kati ya mabondia ambao nafanya nao mazoezi yeye atakuwa akielekea Kosovo.
“Watanzania wajue kuwa nakuja kumaliza utawala wa Miyeyusho kwa sababu siogopi uzoefu wake wa muda mrefu aliokuwa nao tena asipokuwa makini nitampiga kabla ya raundi ya nane.
UNAWAAMBIAJE MASHABIKI WA MALAWI KWA KUWA GLOBAL TV ONLINE WATARUSHA LIVE?
“Hiki ni kitu kizuri kwangu na kwao kwa sababu wataweza kuona kazi nitakayokuwa naifanya ulingoni na kujua ubora wa kiwango changu.
“Global TV itawasaidia ndugu zangu na mashabiki nchini kwetu kuweza kuniona wakati nikicheza na nitawaambia mapema njia yao wa kuweza kuona katika chaneli ya Global TV ambayo inapatikana YouTube.
“Wao wanachotakiwa kufanya ni kuhakikisha kwanza wanaingia YouTube na kujiunga (subscribe) katika chaneli ya Global TV Online,” anasema Kamwamba.
Katika hatua nyingine Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Yassin Abdallah ‘Ustaadh’ alisema pambano hilo, halitakuwa na kiingilio na mashabiki wataweza kulishuhudia mubashara kupitia simu zao za mkononi tu, kwani litaonyeshwa na Global TV pekee. Wadau na mashabiki watakaopata nafasi ya kuingia ukumbini wataingia kwa kadi maalum za mwaliko tu.
Ustaadh aliongeza: “Ili kulishuhudia pambano hilo kwa njia ya simu tena bure, hakikisha unajiunga na YouTube chaneli ya Global TV Online sasa hivi ili usipitwe. Ingia YouTube, tafuta GLOBAL TV ONLINE, kisha bonyeza neno subscribe pia bonyeza kikengele kidogo kilichopo pembeni yake ambacho kitakukumbusha kuangalia pambano hilo mara tu litakapoanza.
“Kama wewe ambaye umeshajiunga, basi hakikisha pia umebonyeza kikengele ili usipitwe na kila kinachoendelea Global TV. Pia unaweza kuwapata kupitia mtandao wa www. globaltvtz.com, jiunge sasa na Global TV ili uwe wa kwanza kuona ndondi za kimataifa siku hiyo. Kajiunge sasa kwa kuingia www. youtube.com/user/uwazi1” alisema Ustaadh.