The House of Favourite Newspapers

Kapombe, Manula rasmi miaka miwili Simba SC

0

Mwandishi Wetu | Dar es Salaam

RASMI sasa wachezaji wa Azam, mlinzi Shomari Kapombe na kipa, Aishi Manula msimu ujao wataonekana ndani ya jezi za Simba baada ya nyota hao kusaini mikataba ya kuitumikia timu hiyo kwa muda wa miaka miwili.

Kapombe na Manula walikuwa sehemu ya mapendekezo ya kocha wa kikosi cha Simba, Joseph Omog, raia wa Cameroon, kwa kutaka wachezaji walio tayari kwa ajili ya kupambana kwenye michuano ya kimataifa ambapo wao watakuwepo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Kapombe kwake ni sawa na kurejea ndani ya kikosi hicho baada ya kukitumikia kwa mafanikio makubwa kwa msimu wa 2011/12 kabla ya kwenda kujaribu bahati yake nchini Ufaransa ndani ya kikosi cha Cannes ambacho kinashiriki Ligi Daraja la Pili huku Manula yeye ikiwa ndiyo mara ya kwanza kujiunga na timu hiyo.

Beki huyo ametua kama mchezaji huru huku akichota milioni 35 kama sehemu ya ada ya uhamisho wake huku Manula yeye akisubiri hadi Julai 31, ambapo ndiyo atakuwa mchezaji rasmi wa timu hiyo baada ya kumaliza mkataba wake na Azam ambapo anatajwa kuikamua timu hiyo kiasi cha milioni 30 hadi 40.

Taarifa za ndani ambazo zimelifikia Championi Jumatatu ni kuwa wawili hao walisainishwa jana Jumapili kwa nyakati tofauti na wameridhia kujiunga na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.

“Ni kweli Shomari Kapombe na Aishi Manula wamesaini jana Jumapili na kuwa wachezaji halali wa Simba, baada ya kuingia makubaliano ya miaka miwili kila mmoja na watakuwa sehemu ya kikosi chetu kwa msimu ujao.

“Usajili huu unaenda kwa maelekezo ya kocha kupitia ripoti yake ambayo ameiacha akitaka tusajili wachezaji walio tayari kwa ajili ya msimu ujao ambao kama unavyojua tutakuwa na kibarua cha kucheza michuano ya kimataifa.

“Hapo ni mwanzo bado kuna wachezaji ambao tunatarajia kumalizana nao na kuwapa mikataba kwa ajili ya kukifanya kikosi kiwe bora zaidi na hilo litaendelea kadiri siku zinavyokwenda,” alisema mtoa taarifa huyo.

Championi Jumatatu, lilimtafuta Kapombe ambaye alifunguka kuwa kila kitu wameshamalizana na Simba na jana ndiyo ilikuwa siku rasmi kwa yeye kusaini mkataba na timu hiyo baada ya kufikia makubaliano.

“Kila kitu kimeenda sawa kama ambavyo tulikubaliana katika mazungumzo yetu na jana (Jumapili) ndiyo ilikuwa siku ya mimi kusaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo kwa mara nyingine,” alisema.

Mkataba wa Manula ambao gazeti hili liliunasa jana, unasema kipa huyo atakuwa akilipwa mshahara wa Sh milioni tatu kwa mwezi, hivyo kwa miaka miwili Msimbazi atavuna jumla ya mshahara wa Sh milioni 72, lakini amesajiliwa kwa dau la Sh milioni 50 ambapo atapewa Sh milioni 25 kwanza, halafu baadaye atapewa milioni 5, kisha watamalizia milioni 20. Hivyo jumla atakomba mil 122.

Kwa upande wa Kapombe, licha ya mkataba wake kutoonekana, taarifa zinasema naye atakula mshahara wa Sh milioni tatu kwa mwezi, na dau lake la usajili ni mil 35, hivyo atamaliza mkataba Msimbazi akiwa amevuna Sh milioni 107.

Habari nyingine zinathibitisha kuwa tayari John Bocco naye ameshasaini rasmi mkataba wa miaka miwili kuichezea Simba.

Leave A Reply