Kazi kwa Ozil Kusuka au Kunyoa

Mesut Özil

MEZUT Ozil amekuwa na wakati mgumu kutokana na kusugua benchi kwa muda mrefu na sasa kumeibuka taarifa kuwa hatakiwi na kocha wake kwenye klabu yake ya Arsenal.

 

Kocha wa Arsenal, Unai Emery amekuwa akikaririwa mara nyingi kwenye vyombo vya habari akidai kuwa Ozil anasugua benchi kutokana na kuwa majeruhi au sababu za kiufundi. Sasa kuna taarifa kuwa Emery anataka Ozil aondoke Arsenal ili kupunguza mzigo wa mshahara wake.

 

Ozil ndiye mchezaji wa pili anayelipwa fedha nyingi kwenye Ligi Kuu England akiwa anapata mshahara wa pauni 350,000 kwa wiki.

Kutokana na hali inayomkuta Ozil kuna watu wenye wanajiuliza kama kweli anastahili mshahara huo mnono. Mjadala wa mshahara wa Ozil unasemekana umeleta mgawanyiko ndani ya kikosi cha Arsenal. Ozil, ambaye aliamua kuachana kuichezea Ujerumani, amekuwa akilaumiwa kwa kutojituma uwanjani na hasa katika mechi ngumu.

 

Aliposajiliwa katika timu ya Arsenal kila mtu alidhani angekuwa mchezeshaji bora kama alivyokuwa staa wa zamani wa timu hiyo, Mholanzi, Dennis Bergkamp. Hata hivyo, amekuwa analaumiwa kwa kushindwa kutumia kipaji chake cha juu kusaidia timu hiyo kutwaa ubingwa.

Ozil ana uwezo wa mkubwa wa kutoa pasi kali, kupiga chenga na kufunga lakini ameshindwa kuonyesha makali yake kila mara.

 

Emery naye ameonyesha wazi hamkubali Ozil na ushahidi wa wazi ni jinsi anavyomtupa kusugua benchi. Taarifa zinaeleza kuwa Mjerumani huyo aliondoka kwa hasira kwenye Uwanja wa mazoezi wa Arsenal, majuzi baada ya kuelezwa hatacheza dhidi ya West Ham, Jumamosi iliyopita.

Emery alikuwa amechukizwa na Ozil kwa kutojituma kwenye mechi dhidi ya Crystal Palace na alimtoa katika dakika ya 68. Tangu wakati huo Ozil amejikuta mara nyingi akisugua benchi au mara nyingine amekuwa akitupwa jukwaani.

 

Ozil aling’ara Arsenal kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 ingawa wachambuzi wa soka wanadai kuwa katika kipindi cha majira ya baridi huwa jamaa huwa hajitumi kabisa. Inaaminika kuwa pamoja na uvivu na uzembe wake lakini Ozil bado alikuwa anabebwa na kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger.

 

REKODI YA OZIL 2018/19 Ozil amecheza mechi 16 za mashindano mbalimbali huku akiwa amefunga mabao manne na kutoa asisti mbili. Hiyo ni rekodi ya Ozil kufuatia kupandishiwa mshahara msimu uliopita baada ya klabu kubabaika kumpoteza kufuatia nyota mwingine wa timu hiyo, Alexis Sanchez kuamua kuondoka mwezi Januari, mwaka jana.

 

Mvutano wa Emery na Ozil unafananishwa na wakati kocha huyo alipokuwa Paris St, Germain ambapo alikuwa haivi na staa wa timu hiyo, Neymar. Hata hivyo, ni wazi Ozil ameshindwa kuendana na mfumo unaofundishwa na Emery katika timu ya Arsenal. Kutokana na hali hiyo, Emery sasa amechukua uamuzi wa kushauri klabu iachane na Ozil ili apate nafasi ya kusajili staa mwenye kuendana na mfumo wake.

 

Kutokana na hali hiyo, Ozil, amejikuta akipitia katika kipindi kigumu ingawa watu walio karibu yake wanadai staa huyo anataka kumaliza mkataba wake na Arsenal hadi utakapomalizika mwaka 2021.

 

Habari za ndani za uongozi wa klabu ya Arsenal umedai kuwa hautaki kumuuza Ozil kwa sababu wanaridhika kuwa yupo tayari kupigania nafasi katika kikosi cha kwanza ndani ya klabu hiyo.

 

Hata hivyo, ana kibarua kigumu kwani itabidi apigane kufa na kupona ili aweze kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Arsenal. Staa huyo pia ana mtihani mgumu pale akiamua kuhama kwani itakuwa vigumu kupata timu ya kumchukua kwani hakuna klabu iliyo tayari kumsajili kutokana na mshahara wake mnono wa pauni 350,000 kwa wiki.

 

Kuna taarifa kuwa mkali huyo hivi karibuni aligomea ofa ya kwenda kucheza barani Asia baada ya kujitokeza klabu iliyokuwa tayari kumlipa kiasi cha Dola milioni moja kwa wiki. Suala la Ozil ni tatizo kwa Emery kutokana na ukweli ni ngumu kwa sasa kupata mnunuzi wa Ozil kutokana na suala la mshahahara wake mkubwa na tabia yake ya kutojituma uwanjani licha ya kuwa na kipaji cha hali ya juu.
LONDON England

Loading...

Toa comment