The House of Favourite Newspapers

Kerr amshtaki Kiongera Simba

0

Sweetbert Lukonge, Zanzibar
JUZI Jumatatu timu ya Simba iliponea chupuchupu kupoteza mechi yake ya kwanza katika michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea kutimua vumbi visiwani hapa baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Jamhuri ya Pemba.

Katika mechi hiyo, wachezaji wawili wa kimataifa wa timu hiyo, Mkenya, Paul Kiongera na Mganda, Hamis Kiiza, walicheza chini ya kiwango ukilinganisha na wachezaji wengine wa timu hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Kocha Mkuu wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, amewafikisha kwa uongozi wa timu hiyo akiwatuhumu kucheza chini ya kiwango, hali iliyosababisha waambulie pointi moja kwenye mechi hiyo.

Akizungumza na Championi Jumatano, Kerr alisema kuwa hakutegemea kabisa kama nyota hao wangecheza hivyo katika mechi hiyo ambayo timu yake ilipoteza nafasi 19 za kufunga na kuambulia mbili tu.

“Katika hili sipaswi kulaumiwa na uongozi unatakiwa kulijua hilo kwani nilipanga kikosi kulingana na ukubwa wa mechi lakini washambuliaji wangu waliniangusha.

“Katika kipindi cha kwanza, Kiongera hakufanya vizuri lakini pia nilifanya mabadiliko na kumuingiza Kiiza, naye hakucheza kama nilivyotarajia, hivyo sipaswi kulaumiwa juu ya hili, nafikiri hata viongozi wameona hali ilivyokuwa,” alisema Kerr ambaye kwa sasa hana amani klabuni hapo.

Leave A Reply