The House of Favourite Newspapers

Kifo cha Magufuli na Zawadi Aliyowaachia Watanzania

0

 

IJUMAA Machi 26, 2021 wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watampumzisha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Dkt John Pombe Magufuli katika makazi ya milele huko Chato mkoani Geita wakiwa na huzuni na majonzi makubwa kumpoteza kiongozi wao aliyedumu madarakani kwa miaka mitano na siku 114.

 

 

Licha ya masikitiko yaliyowatawala, Rais Magufuli amewaachia zawadi pomoni na ndoto za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo itadumu kwa miaka mingi maishani mwao.

 

 

Kutamalaki kwa miradi iliyokamilika na inayoendelea kujengwa nchini humo na maelfu ya wananchi wakipanga barabarani, kujaa viwanjani huku vilio vikisikika sehemu mbalimbali kunaleta taswira pana juu ya uongozi wa Rais Magufuli jinsi ulivyowagusa baadhi ya wananchi hivyo vilio vyao ni kulilia tumaini lao.

 

 

Je, ni zawadi gani ambazo Rais Magufuli amewaachia wananchi wa Tanzania?

Ni kwa kiasi gani kiongozi huyo ataweza kukaa kwenye mioyo ya wananchi wake?

Zifuatazo ni zawadi ambazo Watanzania wameachiwa na Rais Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

 

Reli ya kisasa (SGR)

Tarehe 14 mwaka 2018 Rais John Magufuli aliasisi ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa kwa kuweka jiwe la msingi la kipande cha pili cha mradi huo kilichoanzia mkoani Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma.

 

 

Kipande hicho chenye urefu wa kilometa 422 kitagharimu kiasi cha shilingi trilioni4.3, ambapo ni sehemu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kati wa kuanzia Dar es salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilomita 1,219. Ujenzi wa kipande cha kutoka Dar es salaam hadi Morogoro unaelezwa kuwa umekamilika kwa asilimia 80. Hii ni zawadi aliyoacha Magufuli kwa Watanzania.

 

Mpango wa elimu bure

Serikali ya Magufuli ilitekeleza mpango wa kutoa elimu bure kutoka shule za Msingi hadi sekondari na kuwezesha maelfu ya wananchi kuwapeleka shule watoto wao.

 

Elimu ni nyenzo ya kuinua maisha ya wananchi na juhudi za serikali kuwaelimisha wananchi wake zimeonekana ndani ya miaka mitano ya Magufuli. Wananchi wamepunguziwa mzigo ambao uliwaelemea kwa miaka mingi kuanzia vijijini hadi mijini hivyo kuwa na uhakika wa kupata elimu.

 

 

Vitambulisho vya Wamachinga

Julai 3, 2017 Rais John Magufuli akiwa jijini Mwanza alisema hapendi kuwaona Wafanyabiashara wadogo nchini Tanzania maarufu kama Wamachinga wakisumbuliwa na kushindwa kufanya biashara zao.

 

Ahadi yake ya kuhakikisha Wafanyabiashara hao wanafanya kazi zao kwa uhuru ndizo kiini cha kupatikana kwa vitambulisho na huo ukawa mwanzo wa uhuru wa Wamachinga na Wajasirimali wadogo kufanya biashara maenero mbalimbali.

 

 

Aidha, uhuru waliopewa Wajasirimali wadogo umetokana na mpango wa mpango wa MKURABITA, ambapo unainisha umuhimu wa kurasimisha biashara zisizo rasmi mfano Mama Lishe, saluni, wamachinga na wafanyabiashara wengine wenye mitaji ya chini ya shilingi milioni moja.

 

 

Serikali ya Rais Magufuli ilitumia mpango huo vizuri na kupata mafanikio kwa kusajili vijana wengi waliojihusisha na biashara ya umachinga.

 

 

Utekelezaji wa mpango wa mradi wa umeme wa Bonde la Mto Rufiji ni miongoni mwa zawadi kubwa waliyoachiwa Watanzania. Uamuzi wa kutekeleza mpango wa mradi wa umeme wa Bonde la Mto Rufiji nao umetajwa kuwa ni mafanikio kwa serikali hiyo ambao utaongeza tija katika uzalishaji wa umeme. Kabla ya Magufuli kufufua mradi huo ulisuasua kwa miaka 40.

 

 

Utekelezaji wa sera ya viwanda

Sera ya viwanda SIDP (Sustainable Industrial Development Policy) ya mwaka 1996 inabainisha kuwa Tanzania hadi mwaka 2015 ilitakiwa kuwa na viwanda vya kati. Sera hiyo ilipitishwa na serikali ya awamu ya tatu ya serikali ya rais Benjamin Mkapa na Waziri wa Viwanda na Biashara wa wakati huo alikuwa Dkt. Abdallah Kigoda.

 

Hata hivyo sera hiyo imepigiwa upatu na serikali ya Magufuli na kuwezesha ujenzi wa viwanda mbalimbali vya uzalishaji, kutengeneza ajira, kukuza uchumi na pato la taifa.

 

Ununuzi wa ndege

Kwa mujibu wa Ilani ya CCM ya 2015-2020 imeelezea suala la matengenezo ya viwanja na kufufua Shirika la Ndege (ATCL). Jumla ya ndege 11 zimenunuliwa na mamlaka za Tanzania.

Hili ni eneo jingine lililompa sifa Rais Magufuli na kuwaachia zawadi ya kipekee Watanzania. Matarajio ya ndege hizo ni kuongeza kiwango cha biashara ya utalii nchini humo pamoja na shughuli zingine za kiuchumi.

 

 

Ang’arisha sekta ya afya

Magufuli ameacha zawadi ya zaidi ya vituo 400 vya afya ndani ya miaka mitano. Hospitali za wilaya zaidi ya 70, Hospitali za rufaa za mikoa zaidi ya 10, Hospitali za rufaa za Kanda ni tatu. Magufuli ameacha zawadi ya upandikizaji wa figo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tangu mwaka 2017 huku zaidi ya wagonjwa 70 wamepatiwa huduma hiyo.

 

 

Hospitali ya Uhuru itakuwa kumbukumbu nyingine ya Magufuli kwa wananchi wa Tanzania. Hospitali hiyo imeanza kutoa huduma kwa wakazi wa Dodoma kwa baadhi ya magonjwa.

 

 

Baadhi ya viongozi wa karibu na aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wamemwambia mwandishi wa makala haya kuwa mojawapo ya eneo ambalo lilimkera Rais Magufuli ni kuona raia wake wakimiminika kwenda kutafuta matibabu nje ya Tanzania hivyo alisisitiza lazima huduma za afya zipatikane kwa urahisi nchini humo.

 

 

Mahakama ya Mafisadi

Rais Magufuli alipiga vita rushwa na ubadhirifu tangu akiwa waziri hadi alipochukua mamlaka ya kuongoza Tanzania mwaka 2015. Hatua madhubuti alizochukua ni pamoja na kuanzisha mahakama maalumu ya kusikiliza kesi za ufisadi unaotendwa na watu mbalimbali nchini mwake. Atakumbukwa kwa kupiga vita kivitendo.

 

 

Marekebisho ya Mikataba ya Madini

Serikali ya Tanzania ilidhibiti makinikia yaliyokuwa yanasafirishwa na kampuni ya madini ya Acacia ambayo inamilikiwa na Barrick Gold. Makinikia ni mchanga uliokuwa unasafirishwa kwenda kuchenjuliwa nje ya nchi jambo ambalo halikukubaliwa na uongozi wa Magufuli.

 

 

Majadiliano yaliyoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Palamagamba Kabudi yaliwezesha kupatikana mwafaka ambapo pande zote zilionesha kuridhia makubaliano mapya ya kupata faida zaidi katika sekta ya madini. Uongozi wake unasifika kwa kulinda rasilimali za nchi.

 

Nguvu ya jiji la Dodoma

Wazo la aliyekuwa rais wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere la kuhamisha makao makuu ya nchi kutoka Dar es salaam kwenda Dodoma halikufanyika katika awamu tatu za marais wa nchi hiyo hadi ujio wa Rais Magufuli aliyetangaza uamuzi wa kuhamisha makao hayo.

 

 

Halmashauri Kuu ya TANU (sasa CCM) ilipitisha mpango wa kuhamia Dodoma chini ya Mwalimu Nyerere, lakini serikali hiyo haikuweza kutekeleza hadi ilipoondoka madarakani mwaka 1984. Serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin William Mkapa ilijaribu kuhamisha makao makuu kwa kuzihamisha Wizara ya Kilimo na Ushirika jijini Dodoma lakini hazikudumu huko, baadaye zilirejeshwa Dar es salaam.

 

 

Rais Magufuli akitumia mamlaka aliyopewa na Katiba Rais Magufuli alivunja iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), alisaidia kuondoa kero za ardhi zilizokuwa kilio kwa wananchi. Baadaye alipandisha hadhi ya Dodoma na kuwa Jiji hatua ambayo imeubadilisha mji huo na kuwa kivutio kwa wengi.

 

 

Tayari soko kubwa la kisasa limeshajengwa ambalo linaitwa Soko la Job Ndugai ambalo linatarajiwa kuwavutia wengi na kuufanya Dodoma kuongeza nguvu za kiuchumi.

 

 

Mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato-Dodoma ni zawadi nyingine aliyoacha Magufuli na ambayo inaaminika Rais mpya Samia Suluhu Hassan atakamilisha ndoto hiyo. Vilevile ndoto ya ujenzi wa mradi wa barabara ya njia nne ya kilomita 112.3 ambayo inatarajiwa kupamba jiji la Dodoma.

 

 

Ujenzi wa uwanja wa michezo wa kisasa wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 80,000 unatarajiwa kuwa kimbilio la watu wengi ndani na nje ya nchi. Upanuzi wa Ikulu ya Dodoma wenye eneo la mita za mraba 34,000 ni mradi mwingine ambao utakumbukwa kufanywa na Magufuli nchini mwake. Ingawa bado haujakamilika lakini ni miongoni mwa zawadi ambazo wameachiwa Watanzania.

 

 

Lugha ya Kiswahili

Uamuzi wa kutumia lugha ya Kiswahili katika hotuba zake popote alipotembelea barani Afrika ni zawadi nyingine. Katika moja ya ziara zake nchini Afrika kusini alipokwenda kuhudhuria sherehe za kuapishwa rais Cyril Ramaphosa alishawishi nchi hiyo kuchukua wataalamu wa kufundisha Kiswahili kutoka Tanzania.

 

Katika ziara zote alikipigania Kiswahili kuhakikisha kinatumika kama lugha rasmi na hivyo kuongeza idadi ya wazungumzaji.

 

 

Hadi sasa Kiswahili ni lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika mashariki,Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

 

 

Magufuli atakumbukwa kwa ushirikiano na nchi kama vile Ethiopia,Afrika kusini na Morocco ambazo zilihitaji wataalamu wa lugha hiyo ili kutoa elimu kwa wananchi wao. Alisaini makubaliano na Afrika kusini ya kutoa wataalamu wa Kiswahili.

 

 

Mfupa wa Mtwara Corridor

Mradi huo ambao tangu miaka 2000 umekuwa ukipitia hatua kwa hatua, lakini serikali ya Rais Magufuli ilipokea kijiti kutoka kwa rais mstaafu Jakaya Kikwete imehakikisha unakamilika ili kuunganisha mikoa ya Mtwara na Ruvuma. Ikumbukwe akiwa waziri wa ujenzi nyakati tofauti Magufuli alisimamia ujenzi wa Daraja la Mkapa ambalo liliunganisha mikoa ya Pwani na Kusini ikiwa ni sehemu ya mpango wa Mtwara Corridor.

 

 

Aidha, ujenzi wa barabara ya Masasi-Songea-Mbinga. Awamu ya tatu ya sasa ni kukamilika ujenzi wa kipande cha Mbinga hadi mji wa Mbamba Bay ambao ni bandari inayounganisha nchi za Malawi na Msumbiji hivyo kusisimua uchumi wa wananchi wa nchi hizo.

 

 

Kwenye ziara yake nchini Malawi Rais Magufuli aliwasilisha ombi kwa mwenyeji wake rais wa zamani Peter Mutharika na wananchi wa nchi hiyo kufanya biashara na ushirikiano mwema kwa sababu miundombinu ilikwishaboreshwa na kutumia vizuri bandari ya Mbamba Bay mkoani Ruvuma.

 

Miundo mbinu chekwa

Hadi mwaka 2017 pekee serikali ya Magufuli ilifanikiwa kuunganisha mamlaka za Wilaya takribani 117, vituo vya polisi 129,ufungaji wa taa za barabarani zinazotumia nguvu za jua,kukarabati barabara zenye urefu wa kilomita 2,571 na ujenzi wa madaraja.

 

 

Magufuli alisimamia ilani ya CCM (2015-2020) iliyosisitiza ukarabati na ujenzi wa viwanja vya ndege katika mikoa mbalimbali. Wakati wa uongozi wake mradi wa Mabasi ya Mwendokasi ulianza kutumika na kuwavutia maelfu pamoja na kutengeneza ajira kwa wananchi wake. Utengenezaji wa vivuko vya maeneo mbalimbali nchini.

 

 

Aidha, ujenzi wa vituo vipya vya mabasi vya kimkakati wa kupanua miji vimejengwa katika mikoa mbalimbali. Vituo hivyo vinatajwa kuwa miongoni mwa zawadi kubwa ambazo Magufuli amewaachia Watanzania kuanzia mikoa ya kusini hadi kaskazini, kati hadi magharibi na pwani ambako imetengeneza fursa za ajira na biashara.

Leave A Reply