The House of Favourite Newspapers

KIFO CHA MTOTO NORAH, ALICHOWEKA MTANDAONI MTUHUMIWA INATISHA!

0
Jeneza lenye mwili wa marehemu Norah Mareale.

SIKU chache baada ya kufariki dunia katika mazingira yenye utata kwa mtoto Norah Mareale, mtu ambaye anatuhumiwa kuwa mhusika wa kifo chake, John Msigala, katika mojawapo ya akaunti inayodaiwa ni yake kwenye mitandao ya kijamii, ameweka vitu vinavyoweza kusemwa vinatisha hivyo kuwatisha hata baadhi ya wanaoviona, Uwazi limepekua na kukudondoshea.

ALIANZA SIKU NYINGI ‘KUPOSTI’

Wakati John akiwa anashikiliwa na jeshi la polisi kwa kuhusishwa na kifo cha mtoto Norah ambaye mwili wake ulikutwa ukiwa unaning’inia uani kwao wiki iliyopita, Uwazi limeitembea akaunti yake katika Mtandao wa Kijamii wa Facebook na kukutana na baadhi ya picha alizoweka au kwa lugha ya kimtandao ku-post.

Katika akaunti hiyo, Mei 16, mwaka 2011, John aliweka picha ikimuonyesha mtu aliyevalia kinyago cha kuficha sura, mwilini amevaa tisheti yenye fuvu la binadamu na mifupa huku akiwa ameshikilia kisu mkono wake wa kulia na ule wa kushoto, ameshika kitu kama chombo cha kuchukulia mkaa wa moto kwenye majiko.

AVAA FULANA YENYE MANENO YA UTATA

Kana kwamba haitoshi, miezi mitano baadaye yaani Desemba 4, 2011 alitupia picha akiwa amevaa fulana iliyokuwa na maneno makubwa I’m Confused huku chini yake yakifuatia na maneno madogo yaliyoandikwa… Wait, may be am Not, ambayo kwa tafsiri isiyo rasmi, maneno yale yalimaanisha; ‘Nimechanganyikiwa! Labda siyo hivyo…subiri.

Mtuhumiwa akiwa amevalia sweta lenye maski ya fuvu.

ATUPIA PICHA YA MTU KAVAA KINYAGO

Aidha, John katika akaunti yake hiyo ya Mtandao wa Facebook, Februari mwaka 2012, aliweka picha ya mtu aliyevaa kinyago cha kuficha sura, lakini akiwa amevaa fulana ileile ambayo mtu ameshika kisu huku ameficha sura.

Mwaka huohuo, katika akaunti yake hiyo, ilionekana picha ya kuchorwa ya kijana aliyeonekana akichambua kitu kilichodaiwa ni bangi.

Picha nyingine zilizoonekana kuwekwa katika akaunti hiyo ni pamoja na sanamu za watu wa kutisha, michoro ya watu wanaoonekana wapenzi pamoja na picha za wachezaji wa zamani wa Manchester United, washambuliaji Wayne Rooney na Robin van Persie wakiwa kwenye bango kama la filamu, wakiwa wameshika bastola mbilimbili kila mmoja.

John Msigala na T-Shirt yake….I AM CONFUSED…

MWANASAIKOLOJIA ALONGA

Baada ya kuziona picha hizo, Uwazi lilimtafuta mwanasaikolojia Warren Justin, ambaye baada ya kuelezwa kuhusu mazingira ya kifo cha mtoto Norah, kuhusishwa kwa John na kilichomo katika akaunti yake ya Facebook, alisema;

“Hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya vitu anavyopenda mtu na tabia yake. Mtu anaweza kupenda filamu za kivita na mapigano, lakini nje ya hapo, ni mpole na asiyependa kabisa vurugu.

“Kuna majambazi wengi wamezaliwa kutoka kwa wazazi wacha Mungu kama ilivyo kwa wacha Mungu kutoka katika wazazi maharamia. Ukiangalia vitu unavyoniambia vipo katika akaunti ya John, ni vigumu kumsoma tabia yake moja kwa moja, kwa sababu anaonekana mtu mwenye mambo mengi, siyo rahisi kumhusisha na upande mmoja.

Mtuhumiwa John Msigala.

 

“Mara nyingi mtu mwovu huficha sana hisia zake, ndiyo maana utawaona baadhi ya watu wanashangaa wanaposikia mtu waliyemzoea kama mkimya na mpole awe amefanya jambo tofauti. Inatokea tu, ndiyo maana ninakuambia hizo ‘post’ zake haziwezi kuakisi tabia yake halisi hata mara moja. Inawezekana ni mtu anayependa tu muvi za kivita na mambo kama hayo.”

Norah alifikwa na umauti Jumapili iliyopita baada ya mwili wake kukutwa nje ya nyumba yao Sinza Mori jijini Dar ukiwa na majeraha sehemu za siri na shingoni ambapo John pamoja na mama mdogo wa marehemu walichukuliwa na polisi kwa ajili ya kusaidia kwenye upelelezi wa kifo hicho.

Norah alizikwa Jumatano iliyopita katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, amina.

STORI: Mwandishi Wetu, Dar

 

VILIO, SIMANZI VYATAWALA KUAGWA KWA MTOTO NORAH

Leave A Reply