The House of Favourite Newspapers

Kiingereza Ndiyo Lulu ya Utaalam, Kiswahili Lugha ya Minadani!

KIMSIKIA mtu leo mwaka 2017  anaibeza lugha ya Kiingereza,  akakuambia  uachane nayo katika masomo,  utaalam na mawasiliano na walimwengu wengine, akakusisitiza utumie Kiswahili, kwanza muulize mtu huyo iwapo anajua kuisema na kuiandika lugha hiyo.

Akisema haijui kwa lolote, basi achana naye, na iwapo akisema anaijua vyema na ni msomi anayeitumia katika shughuli zake, mtu huyo  atakuwa na ajenda mbaya kwa Watanzania wenzake!

Kwa mabilioni ya watu duniani, hususan waliopitia katika utawala wa Waingereza kama Watanzania, Kiingereza ndiyo njia kuu inayowaunganisha  na mabilioni ya watu wengine duniani katika mawasiliano.

Kiswahili ni muhimu tu kwa kuwaunganisha Watanzania wa Kigoma, Dodoma na Tanga wakati wanacheza bao, wanapovua samaki na kwenye minada.  Basi!  Hakuna umuhimu zaidi ya huo.

Ajabu ya miaka nenda-rudi ni mijadala isiyokwisha inayofanywa hasa na wasomi, wakipuuza matumizi ya Kiingereza mashuleni na vyuoni,  wakitaka kizazi cha sasa kifundishwe masomo yote kwa Kiswahili!  Kisa?

Eti uelewa na  elimu vimeshuka mashuleni na vyuoni. Wanaodai hivyo – wengi wao wakiwa walipata fursa nzuri ya elimu kupitia Kiingereza – wamesahau kwamba kuporomoka kwa uelewa wa Kiingereza na elimu nchini kulianzia mwaka 1966 pale utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, ulipobadili mfumo mzima wa elimu.

Kwanza, ulilifuta darasa la nane lililokuwa miongoni mwa madarasa manne ya shule ya kati yaani ‘middle school’ – kuanzia darasa la tano hadi la nane.  Kilichofuata ni  elimu ya shule za msingi (primary school) na kati (middle school) kuunganishwa, hivyo elimu ya darasa la kwanza hadi la saba ikawa ni elimu ya shule ya msingi!

Kitu muhimu ambacho wengi  ama hawakijui au hawataki  kukumbushwa  ni kwamba tangu wakati huo, mwanafunzi akiingia darasa la kwanza, aliendelea na masomo hadi darasa la saba bila mtihani wowote wa kumkwamisha hapo katikati! Matokeo yake, maelfu ya wanafunzi waliishia darasa la saba na kurejea ‘uraiani’ kwenda kulima na kuchunga ng’ombe,  wachache wakapenya kuendelea na elimu ya sekondari!

Huo  ukawa mwanzo wa kuporomoka kwa elimu nchini.  Kuna mtu au watu waliokuwa wamepanga kwamba: Kikubwa kilikuwa ni kuwawezesha mamilioni ya Watanzania kujua kusoma na kuandika tu halafu watokomee mashambani na mitaani. Kwa wanaokumbuka, masomo tangu darasa la kwanza hadi la nne katika shule za msingi  (primary school)  yalikuwa yakifundishwa kwa Kiswahili likiwemo somo la Kiingereza lililotiliwa mkazo mkubwa.

Punde mtu alipovuka na kwenda shule ya kati (middle school) , masomo yote yalibadilika na kuwa ya Kiingereza hadi anamaliza chuo kikuu. Kwa vile ufundishaji wa lugha ya Kiingereza ulikuwa mzuri, waliokwenda ‘middle school’ hawakupata tatizo lolote katika masomo.

Hii ni tofauti na sasa ambapo masomo yote tangu darasa la kwanza hadi la saba ni Kiswahili ambapo fumba na kufumbua mwanafunzi anapoingia kidato cha kwanza,  masomo yote yanabadilika na kuwa Kiingereza! Hapo ndipo chujio la watoto wa maskini na matajiri huanzia kazi yake.

Watoto wa familia tajiri waliosoma kwa Kiingereza tangu awali, ndiyo huubeba ‘ufalme’ wa elimu nchini; watoto wa familia maskini za Wasukuma na Wazaramo, jua la elimu huwachwea wakiliona, lisiibuke tena! Kushuka kwa elimu na uelewa ni kupuuza Kiingereza ambacho ni chemchemi  ya elimu tangu vitabuni, makongamano hadi  michezoni!

Kwa sasa, kizazi cha matajiri, watoto na wajukuu zao ndicho kinachomiliki neema ya nchi hii kupitia elimu iliyoimarishwa kwa Kiingereza! Wanaodhani Kiswahili kitawafungulia utaalam wa kwenda kwenye Jua usiku bila madhara au kujua iwapo upande wa pili wa Mwezi unang’aa, wanaota ndoto za mchana.

Wanalazimika waamke, wakae, wasimame na kuanza kutembea!  Kiswahili lugha ambayo hata miaka elfu moja haijapita tangu kiingie Mombasa, Zanzibar, Kigoma na kwengineko  kitabakia kuwa lugha ya mitaani na kwenye minada tu! (itaendelea wiki ijayo).

Walusanga Ndaki/GPL

Comments are closed.