Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-15

Mpenzi msomaji, wiki iliyiopita niliishia pale Dorcas aliyekuwa akizungumza na mama zake, wakati mama yake akichagua mchele aliinjika jikoni sufuri waliyotumia kupikia wali. Je, kilifuatia nini? Endelea mbele…

Siku hiyo kila mmoja wetu alishiriki mapishi ya jioni na chakula kilipokuwa tayari saa mbili usiku mama mkubwa alikiandaa mezani, tukala na kwenda kulala.

Wote tukiwa tumelala kwenye kitanda cha futi sita kwa sita cha mama mkubwa, ilipotimu saa nane usiku nilisikia upepo mkali ukivuma na kutikisa bati la nyumba.

Hali hiyo pia ilisikiwa na akina mama lakini hakuna kati yetu aliyeshtuka sana kwa sababu tulikwishaambiwa na mganga kuhusu tukio hilo, tulitulia mpaka upepo ukatoweka.

“Mmeamini maneno ya mganga?” mama mkubwa alituuliza.

“Nimeamini dada yangu, kweli hii dunia ina mambo sasa nimeanza kuamini,” Dorcas anasema mama yake aliwaambia.

Kufuatia tukio hilo, tulitumia muda mrefu kulizungumzia hadi tulipopitiwa na usingizi, niliposhtuka ilikuwa kwenye saa 12 alfajiri ambapo niliamka ndipo mama mkubwa aliniuliza nilitaka kwenda wapi, nikamwambia shuleni.

“Hapana mwanangu leo usiende utaenda kesho,” mama mkubwa aliniambia.

Nilipomuuliza sababu akaniambia nisiende tu nisubiri mpaka siku iliyofuata, kwa kuwa nilikuwa mtoto sikutaka kumbishia kwa sababu wakubwa wanaposhauri jambo ni vyema kuwasikiliza.

Kwa kuwa ratiba ya kwenda shule haikuwepo, sikutaka kurudi kulala nikataka kutoka nje nikafagie uwanja, kuosha vyombo na kufua nguo.

“Mwenzetu mbona umeduwaa, kwa kuwa huendi shule rudi ulale,” Dorcas anasema mama yake mkubwa alimwambia.

Mama mkubwa aliponiambia hivyo nilimweleza kwa kuwa nilikuwa nimeamka ngoja nikafagie uwanja, kuosha vyombo na baada ya kupata kifungua kinywa ningefua nguo.

Licha ya kumwambia hivyo, alinizuia kwenda kufagia na kunitaka nirudi kulala kwa sababu nje kulikuwa na baridi, nikarudi kulala.

Ilipofika saa moja, tuliamka na baada ya kupata kifungua kinywa, akina mama walinianga kwamba wanakwenda kwenye biashara wakaniachia hela za matumizi, nakumbuka mama aliniambia nikanunue nyama wangerejea na ndizi kwa sababu zilipita siku kadhaa bila kula chakula hicho.

Walipoondoka, niliosha vyombo kwenye saa tatu hivi na nusu nilikwenda sokoni kununua nyama pamoja na viungo, wakati narudi nikiwa nimepita kwenye uchochoro ghafla nilimuona paka mweusi akiwa amesimama mbele yangu, nywele zikanisisimka.

Nakumbuka siku moja tukiwa tunazungumza na akina mama, mama mkubwa aliwahi kusema ikitokea mtu anatembea usiku au mchana halafu akahisi nywele kumsisimka hali hiyo inaashiria hatari ipo mbele yake.

Kutokana na hali hiyo, nilihisi sikuwa sehemu salama, nikapa wazo la kurudi ili nipite njia nyingine, wakati nawaza hivyo yule paka alikuwa amesimama akiniangalia.

Jambo la kushangaza nilipogeuka nyuma ili nirudi kwa lengo la kupita njia nyingine nikashangaa kumuona paka aliyefanana na yule aliyekuwa mbele yangu akiwa amesimama ananiangalia, moyo ukapiga paa!

Kutokana na tukio hilo, niligeuka tena nyuma ili kumwangalia yule paka wa awali, sikumuona nikabaki nikijiuliza alihamaje na kuja kusimama nyuma yangu!

Kwa kuwa lengo langu lilikuwa ni kutoka pale uchochoroni niliamua kusonga mbele, cha ajabu nilipotembea hatua tatu ghala yule paka alitokea mbele yangu.

Tukio hilo ambalo ilikuwa mara yangu ya kwanza kukumbana nalo liliniogopesha sana, nilishindwa kuvumilia nikaanza kupiga mayowe ya kuomba msaada.

Cha kushangaza ni kwamba licha ya kupiga mayowe yule paka hakuondoka mbele yangu, wa kwanza kufika pale uchochoroni walikuwa akina mama wawili, mama Thabi, mama Elisha kisha walitokea vijana watatu na dada mmoja.

“Wewe Dorcas umepatwa na nini?” Dorcas anasema mama Thabi ambaye alikuwa akimfahamu vizuri alimwuliza.

Je, kilifuatia nini? Usikose Alhamisi ijayo. Maoni, ushauri nicheki kupitia namba hizo hapo juu.


Loading...

Toa comment