The House of Favourite Newspapers

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-37

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Dorcas aliposhangazwa sana na kitendo cha Barton kunywa maji mengi asubuhi baada ya kuamka tu hata bila kupiga mswaki ambapo kijana huyo alimwambia ilikuwa kawaida kufanya hivyo. Je, kilifuatia nini? Songa mbele na mkasa huu wa kuhuzunisha…

Aliponieleza hivyo, akamimina tena maji kwenye glasi na kunywa glasi mbili hivi, akiondoka akiwa anacheka kuelekea kwenye korido sehemu iliyokuwa na viatu akavaa raba.

Barton alipovaa raba, alichukuwa maji kwenye jagi akajongea uwanjani akanawa uso kisha alituaga kwamba anakwenda kwenye mazoezi.

“Hivi akitoka huko jambo la kwanza nikunywa uji yaani anaweza kumaliza hata ukijaa kwenye hii bakuli,” Tabu aliniambia.

Nilibaki kushangaa kwani sikuamini, Tabu alinifahamisha kwamba kwa kuwa nilikuwa mwana familia ile ningeshuhudia kwa macho yangu.

Mama alipoamka na kukuta tumefanya usafi wa mazingira,kupiga deki, kuosha vyombo na kupika uji alifurahi sana na kusema wasichana ndiyo wanavyotakiwa kuwa.

Mama alimwuliza Tabu kama aliweka maji ya kuoga baba bafuni, ambapo alimweleza alikwishayaweka, akasema safi sana ndipo aliingia ndani. Hazikupita dakika nyingi baba alitoka na kutusalimia.

Aliniuliza kuhusu uchovu wa safari nikamwambia nilikuwa vizuri akasema asante kisha akaenda kuoga, alipomaliza mama naye aliingia bafu kwa ajili ya zoezi hilo.

Baba alipopata kifungua kinywa alikwenda kazini, tukiwa tumebaki na mama alituita sebuleni na kutuambia kwambia tulimfurahisha sana kwa jinsi tulivyofanya kazi za nyumbani.

Nilimwambia asijali kwa sababu jukumu hilo lilikuwa letu, tulipomaliza kunywa uji, wakati mimi naosha vyombo Tabu alitoa rundo la nguo chafu tayari kwa kuanza zoezi la kufua.

Kwa kuwa vyombo havikuwa vingi, nilimaliza haraka nikaungana na dada huyo wa kazi kufua nguo ndipo Bite na Monica walipoamka, tulisalimiana nao.

Nilishangazwa na kitendo cha wasichana hao kuamka karibu saa tatu kasoro kisha kupiga mswaki na kwenda kunywa uji wakati wenzao tuliamka mapema na kufanya karibu kazi zote.

Tukiwa tunafua nilimwuliza Tabu kuhusu tabia hiyo, msichana huyo alitabasamu na kuniambia niachane nao kwani alikwisha wazoea.

Nilimwuliza kuwazoea kivipi, akaniambia huwa hawafanyi kazi yoyote labda wakipenda tena zile ndogondogo lakini kazi zote za nyumbani kuanzia kufua, kupika, kuosha vyombo, usafi wa mazingira alikuwa akifanya yeye.

Hakuishia hapo, aliniambia hata kwenda sokoni kununua mahitaji ya jikoni na vitu vingine alikuwa akienda yeye na mama, wao walifanya hivyo mara chache.

Tabu aliniambia niachane nao kwani kuna siku watakuja kuona athari za tabia hiyo ya kudeka na kutegemea kila kitu wafanyiwe na yeye, nikaishia kushangaa.

Nilikaa wiki nzima utaratibu wa kufanya kazi za nyumbani ukiwa kama nilivyoukuta, sikuwa na kinyongo kwani lengo langu kubwa lilikuwa kusoma ili niwe na elimu itakayonikomboa katika maisha yangu.

Siku moja usiku nikiwa nipo chumbani na Tabu, aliniambia kwamba Barton alikuwa muhuni sana kwani mara kwa mara alikuwa akimtongoza lakini alimkataa.

Aliponiambia hivyo, nikamwambia hata mimi amekuwa akiniangalia na kuna wakati ananikonyeza lakini nashindwa kumkaripia kuhofia kumkwaza mama yake.

Tabu akaniambia hiyo ndiyo tabia yake na kuna wakati kama pale nyumbani wengine wanakuwa hawapo akijua Tabu yuko chumbani alikuwa akienda kumgongea mlango lakini alikuwa hafungui.

Taarifa alizonipatia Tabu kuhusu Barton zilinikumbusha kitendo nilichofanyiwa na Evance, nikajikuta nalia na kujiuliza moyoni kwa nini kila ninapokuwa nakutana na majaribu?

Msichana huyo wa kazi ambaye kwa muda mfupi tulipatana sana, aliponiuliza sababu za kulia nilimdanganya kichwa kilikuwa kinauma kwani sikutaka kabisa kumweleza historia yangu.

Kwa upendo aliinuka, nilipomuuliza alitaka kwenda wapi akaniambia kuchukua Panadol, nilimwambia huwa nikinywa maji mengi kinapoa na kumsihi asimwambie mtu yeyote kama nilikuwa naumwa kichwa.

“Kwa nini hupendi niwafahamishe?” Tabu aliniuliza.

Nilimwambia aache tu, nikinywa maji kitapoa na kwamba huwa sipendi hata vitu vidogo kuwaambia watu, Tabu akanielewa na kwenda kuchukua maji ya kunywa.

Nilikunywa maji hayo kwa kumzuga tu Tabu ukweli nilikuwa naujua mwenyewe, nikajikuta naapa moyoni kwamba Barton asingeweza kunibaka kwani siku atakayojaribu kuniletea ujinga wake ndiyo angejua.

“Sitakubali tena kubakwa,siku atakayojaribu kuniletea ujinga wake nitamuua kama kwenda kufia jela nipo tayari,” nilijisemea moyoni.

Tukiwa tunapiga stori na Tabu, akina Bite na Monica waliokuwa wakiangalia runinga waliingia chumbani,tukabadili mazungumzo ambapo haukupita muda mrefu tukapitiwa na usingizi.

Kulipokucha kama kawaida, mimi na Tabu tukawa bize na kazi na ilipofika saa tatu hivi alifika yule dereva tuliyetoka naye Shinyanga, akina Bite, Barton, Monica na Tabu walimchangamkia na kumwita mjomba.

Kufuatia kumwita hivyo nilijua kumbe alikuwa kaka wa yule mama, baada ya salamu aliniuliza nilikuwa naendeleaje nikamwambia safi, wakati huo mama naye alikuwepo.

Mjomba huyo aliponiuliza kama nilianza shule nikamwambia bado, akauliza kwa nini nikamwambia bado mama hakunitafutia.

Kabla hajaendelea kuzungumza, mama alidakia na kumweleza kwamba tayari zoezi hilo lilianza na baba ndiye alikuwa akifuatilia, mjomba akasema hapo sawa.

 

Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo kupitia gazeti hilihili.

Leave A Reply