Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2021 Yazinduliwa Jijini Dar
IJUMAA Novemba 13, 2020, msimu wa 19 wa mbio maarufu za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2021 umezinduliwa jijini Dar es Salaam huku Serikali ikimwagia sifa mbio hizo kutokana na mchango wake katika ukuaji wa sekta ya Utalii na uchumi kwa ujumla .
Akizungumza katika hafla iliyofana ya uzinduzi huo uliofanyika Hoteli ya Slip Way jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Michezo katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Alex Nkenyenge aliyemuwakilisha mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ally Possi alisema mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zimechangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa sekta ya utalii wa michezo nchini hivyo kupelekea kuongezeka pato la fedha za kigeni.
“Tukio hili ambalo huvutia zaidi ya wageni 25,000 katika mji wa Moshi ambao baadhi yao ni washiriki na watazamaji ambao pia hufurahia vivutio mbalimbali vya kitalii na kupromoti shughuli nyingine za kiuchumi katika mji huu,” alibainisha.
Nkenyenge amewataka wafanyabiashara si tu kuchangamkia fursa zinazoletwa na mbio hizo kwa kutengeneza faida, bali pia wahakikishe wanatoa huduma na kuuza bidhaa zenye ubora.
Aidha ametoa wito kwa waandaaji wa mbio nyingine za marathoni nchini kufuata nyayo za mbio za Kilimanjaro Marathon ambayo imekuwa ikizingatia miongozo ya IAAF na Riadha Tanzania (RT) hivyo kupelekea kukua mwaka hadi mwaka na kuvutia wadhamini na washiriki kutoka ndani na nje ya nchi.
“Serikali itaendelea kushirikiana na waandaaji wa Kilimanjaro Marathon kuifanya iwe bora na bora,” alisema.
Kuhusiana na janga la gonjwa la Covid-19, Nkenyenge alisema serikali itahakikisha kwamba wale wote wanaohudhuria wanapimwa, haswa wale kutoka nje ya nchi.
“Washiriki wa mbio za Kilimanjaro marathoni hawapaswi kuwa na wasiwasi kwa kuwa tutachukua tahadhari zote muhimu katika sehemu zote za kuingilia nchini,” alisema.
Aidha aliwapongeza wadhamini wa mbio za Kilimanjaro ambao wanaongozwa na Kilimanjaro Premium Lager ambao ndio wenye dhamana ya mbio za 42km, Tigo-21km, Grand Malt-5km, pamoja na wadhamini wa meza za maji, Absa Tanzania, Unilever, TPC Limited, Tanga Cement, Kilimanjaro Water na GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel na CMC Automobiles
Kwa upande wake Meneja wa bia ya Kilimanjaro, Irene Mutiganzi ambaye pia ni meneja wa kinywaji cha Grand Malt, alisema wanajivunia kuwa wadhamini wa mbio hizo kwa mwaka wa 19 mfululizo sababu bidhaa zao kujikita kutangaza na kukuza utalii na utamaduni wa Tanzania kwa ujumla wake.
Aidha alisema wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mbio za mwakani ambapo wametenga shilingi milioni 25 kwa ajili ya zawadi za washindi wa kwanza kwa mbio hizo kwa upande wa wanaume na wanawake ambapo washindi watajinyakulia shs milioni 4 kila mmoja na kwa Mtanzania mwanaume na mwanamke wa kwanza watapata shs milioni 1.5 kila mmoja kama motisha.
Hivyo amewataka washiriki kujisajili kushiriki katika mbio hizo kwa kwa wakati kwani tayari usajili umeshafunguliwa rasmi kupitia njia ya mtandao wa www.kilimanjaromarathon.com pamoja na Tigo Pesa kwa kupiga nambari *149*20#.
Aidha Irene pia amewataka wale ambao watapenda kushiriki kwenye mbio za kilometa 5 nao wajisajili mapema kwani nafasi za ushiriki zitakuwa chache kwa mara nyingine tena. Mwaka huo waandaji walilazimika kufunga usajili mapema kwani nambari zote kwenye mbio zote za 42km, 21km na 5km zilikuwa zimeuzwa mapema.
Naye Mkuu wa Huduma za Masoko wa Tigo, William Mpinga alisema, “Kama kampuni ya mawasiliano inayoongoza nchini ikiwa na mtandao mpana zaidi wa 4G, tunafurahi na kujivunia kwa mara nyingine tena kudhamini Tigo Kili Half Marathon 2021 kwa mwaka wa sita mfululizo.”
“Tunawaomba washiriki kujisajili kwenye mbio na kulipia ada zao kupitia Tigo Pesa kwani ni njia rahisi na ya uhakika na kwa wale wakimbiaji ambo hawana laini ya Tigo wanaweza kuwaomba marafiki na jamaa zao kuwasajili. Tunayo matumaini kuwa Tigo Kili Half Marathon 2021 itaendeleza utamaduni wake wa kusheherekea pamoja na jamii.
Na Katika kuongezea juhudi za Serikali za kuzuia Covid 19 kupitia hatua kali katika maeneo yote ya kuingilia nchini, waandaaji wa mbio za Kilimanjaro Marathon watahakikisha kwamba maafisa wake wote ambao wanashughulikia wakimbiaji wakati wa usajili na siku ya mbio, wanafuata miongozo ya kimataifa na watakuwa wamevalia vifaa vya kujikinga (PPE) ikiwa ni barakoa na vitakasa mikono pamoja na kuhakikisha na kunakuwepo kutotangamana kwa watu (Social distancing) kama moja ya vipaumbele vyao.
Hafla ya uzinduzi huo ilihudhuriwa pia na wawakilishi wa Baraza la Michezo la Tanzania (BMT), Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC), Riadha Tanzania (RT), vilabu vya mbio na vyombo vya habari.
Kulingana na waandaaji, msimu wa 19 wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon utafanyika Jumapili Februari 28, 2021 katika Chuo Kikuu cha Ushirika cha Moshi (MoCU). HABARI/PICHA ZOTE NA RICHARD BUKOS